Raila ailiwaza Kenya baada ya kupigwa na Algeria

Muktasari:

  • Mchezo unaofuata, Kenya itashuka dimbani Alhamisi hii, kuwavaa majirani zao Tanzania, kabla ya kukutana na Senegal, Julai mosi.

Cairo. Misri. Waziri mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga amewatembelea wachezaji wa timu ya taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’, kwa lengo la kuwapa moyo, kufuatia kupoteza mchezo wao wa kwanza kwenye fainali za mataifa ya Afrika, dhidi ya Algeria.

Stars, jana ilifungwa mabao 2-0 na Algeria katika mchezo wa pili wa Kundi C, uliopigwa kwenye Uwanja wa Jeshi la Cairo, kwa mabao ya haraka haraka kipindi cha kwanza kutoka kwa Baghdad Bounedjah aliyefunga kwa mkwaju wa penalti baada Dennis Odhiambo kumkwatua Atal, na la pili likifungwa na kiungo wa Manchester City, Riyad Mahrez.

Akiongozana na Waziri wa michezo, Balozi Amina Mohammed, Katibu wa Wizara ya michezo, Kirimi Kaberia na Balozi wa Kenya nchini Misri, Joff Otieno, Raila alijumuika na timu kupata kifungua kinywa, aliwataka wachezaji kutokatishwa tamaa na matokeo ya jana.

“Ningependa kuwapongeza kwa kuonyesha mchezo mzuri hasa katika kipindi cha pili, siku zote tukumbuke kuwa haijalishi mtu umeanguka mara ngapi, kinachojalisha ni jinsi utakavyosimama baada ya kuanguka, jana tuliteleza lakini bado tunayo nafasi," alisema Raila na kuendelea.

“Siku ya Alhamisi tunakutana na Tanzania. Tunajuana nao, na tukijiamini kama tulivyojiamini kipindi cha pili, najua tutapata matokeo na kusonga mbele. Nafasi bado tunayo, tunachopaswa kufanya kusahihisha makosa ya jana," alisema

Kenya sasa inakabiliwa na mtihani mgumu wa kupata ushindi dhidi ya Tanzania ambao nao wanahitaji ushindi baada ya kupigwa mbili na Senegal, kisha kumaliza shughuli, Julai mosi dhidi ya Simba wa Teranga. Msimamo wa Kundi C, unaonesha Algeria wako kileleni wakifuatiwa na Senegal, wote wakiwa na pointi 3, huku Kenya na Tanzania wakishika nafasi ya tatu na nne mtawalia, bila pointi hata moja.