RT yatoa kibano wanariadha watatu Kenya

Muktasari:

  • RT imewahi kuzuia zawadi kwa washindi wa mbio za Bagamoyo Marathoni mwaka jana baada ya washindi hao kutoka Kenya kutofuata taratibu za ushiriki kutoka kwenye Shirikisho la Riadha la Nchi hiyo (AK).

SHIRIKISHO la Riadha Tanzania (RT) limewapiga marufuku wanariadha watatu kutoka Kenya kutoshiriki mbio zozote nchini.
Wanariadha hao ni  Denis Kemboi, Limo Peter na Karbolo Tatiyia walioshiriki bila ruhusa mbio za Kimondo marathoni hivi karibuni.
Katibu Mkuu wa RT, Wilhelim Gidabuday alisema wanariadha hao hawataruhusiwa kushiriki mbio zozote za Tanzania hadi watakapojadiliana kwa kina na Shirikisho la Riadha la Kenya (AK).
"Tayari tumewaandikia AK na wameonyesha nia njema ya majadiliano," alisema Gidabuday huku akiwasisitiza waandaaji wa marathoni nchini, kufuata sheria na taratibu na RT.
Alisema Shirikisho hilo limeanza kuchukua hatua kwa wale ambao hawataki kufuata taratibu, kanuni na sheria katika uandaaji na ushiriki wa mbio mbalimbali za marathon nchini.
"Kwa muda mrefu baadhi ya waandaaji wa mbio hizo na washiriki kutoka nje ya nchi, wamekuwa kwa makusuidi wakivunja taratibu kwa maslahi binafsi, bila kujali maslahi mapana ya maendeleo ya mchezo wa riadha hapa nchini.
"Mfano ni waandaaji wa Kimondo Marathon iliyofanyika hivi karibuni mkoani Songwe, mbio iliendeshwa kinyume cha sheria, taratibu na kanuni za RT pamoja na Baraza la Michezo la Taifa (BMT),".
Alisema licha ya jitihada za RT kutuma mjumbe wa Kamati ya Ufundi, Lwiza John, ili kuwafahamisha waandaaji kwamba wanariadha wa nje ya nchi hawaruhusiwi kukimbia bila ruhusa ya Vyama vya Riadha vya nchi zao, lakini imedaiwa kutotii na wanariadha hao watatu waliotoka nje ya nchi kushiriki.
"Kwa tafsiri rahisi ni kwamba, ubabe ulitumika kwa kisingizio cha mkuu wa mkoa amesema," alisema Gidabuday.
"Pia tunafahamu kwamba, tuna tatizo kubwa la Mawakala ambao wanawaleta wanariadha wa nje ili wapate asilimia 15 ya fedha wanazoshinda, tutalipeleka suala hili BMT na kwa Waziri mwenye dhamana ya Michezo.
"Waandaaji wa Marathoni wanapaswa kuwa wazalendo kwa kufuata sheria za RT ambazo pia ni za Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF), pia wathamini fedha wanazopata kwa wadhamini ambao ni kampuni na taasisi za kitanzania, zisiende nje ya nchi yetu kiholela sababu hizi ni kodi zetu,".
Alisema anafahamu mbio za Kimondo Marathon zimeanzishwa kwa nia njema, lakini hawajui walikuwa na masilahi gani na wanariadha wa Kenya ambao hawakuwa na ruhusa.