Prisons yatibua rekodi ya Simba

Prisons imevunja rekodi ya Simba ya kutopoteza mchezo tangu kuanza kwa Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya  kuifunga bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika kwenye Uwanja wa Nelson Mandela Rukwa.

 

Simba ilianza ligi kwa kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ihefu, kisha ikatoka sare ya bao 1-1 na Mtibwa Sugar,ikaichapa Biashara United mabao 4-0, ikaifunga Gwambina mabao 3-0  na kisha ikainyuka JKT Tanzania mabao 4-0.

 

Prisons imeharibu rekodi hiyo ya Simba na sasa ni timu mbili tu Yanga na Azam ambazo ndizo pekee hazijapoteza mchezo hadi sasa kwenye Ligi Kuu bara.

 

Simba leo iliathiriwa na kukosekana kwa nyota wake watano wa kikosi cha kwanza wakiwemo  Pascal Wawa, Clatous Chama, John Boco, Meddie Kagere na Chris Mugalu waliokuwa wakikabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwemo majeruhi.

 

Simba ilikosa nguvu hasa eneo la ushambuliaji kwani Luis Miquissone alionekana kuhangaika peke yake huku Bernard Morrisons na Charles Ilanfya wakionyesha kiwango cha kawaida na kushindwa kuwa na madhara katika lango la Prisons.

 

Pia hata safu ya kiungo ya Simba leo ilionekana kupwaya kwani Jonas Mkude hakuwa katika ubora wake wakati Larry Bwalya alijitahidi lakini alidhibitiwa na viungo wa Prisons walioongozwa na Jumanne Elifadhil na Ezekiel Mwashilindi.

 

Bao lililowapa pointi tatu Prisons lilifungwa na Samson Mbangula kwa kichwa dakika ya 48 akimalizia mpira wa krosi uliopigwa na beki Michael Ismail.

 

Ushindi huo unaifanya Prisons kufunga Simba mwa mara ya kwanza kwenye Uwanja wao wa nyumbani baada ya miaka minne kupita tangu ilipofanya hivyo Novemba 8, 2016 ilipoichapa mabao 2-1 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya.

 

Katika msimu mitano mfululizo tangu mwaka 2015 kabla ya mchezo wa leo, Prisons ilikutana na Simba kwenye uwanja wake wa nyumbani Sokoine Mbeya mara tano , huku ikishinda mara mbili sawa na Wekundu wa Msimbazi huku timu hizo zikitoka sare mara moja.