Polisi wajishtukia, wapeana siku 10 zaidi

Muktasari:

Ugonjwa wa corona uliogundulika katika mji wa Wuhan, China umedaiwa kuua zaidi ya watu 49,000 duniani, huku kesi za maambukizi ikiwa ni  zaidi ya  960,000.

SIKU moja tu tangu walipotangaza wamewaita wachezaji wao ili kuwapima kabla ya kuanza mazoezi, mabosi wa Polisi Tanzania wamejishtukia na kuwaongezea siku 10 nyingine wachezaji wao ili kufanya mazoezi makwao wakati wanaisikilizia hali ya ugonjwa wa corona.
Hata hivyo wachezaji hao hawajatoka patupu kwani walipewa elimu zaidi juu ya kujikinga na ugonjwa huo, huku wakiendelea kuzitumia siku hizo za nyongeza kujifua kusudi wakirejea wawe fiti na kuliamsha dude kama kawaida kwenye Ligi Kuu Bara iliyosaliwa na mechi za raundi 10.
Uongozi wa Polisi umeamua kuchukua hatua hiyo baada ya kuona hali ya kuenea virusi vya corona ikizidi kusambaa kwa kasi huku upande wa Prisons wao wakiunda kundi la WhatsApp kwa ajili ya kuendesha programu zao kwa kipindi hiki.
Makamu Mwenyekiti wa Polisi Tanzania, Robert Munisi alisema baada ya kuona hali hiyo, juzi walikutana na wachezaji kwa muda kisha kuwaruhusu kurejea kila mtu kwao.
"Polisi ni taasisi ambayo hufanya kazi kwa kuzingatia maelekezo mbalimbali, hivyo kuna baadhi ya wachezaji wetu ni raia na wanaishi na jamii huko waliko.
"Tuliona ni vyema wakapata elimu ambayo itawasaidia wanakoishi pamoja na kuwapa elimu majirani zao na hiyo ndio njia ya kuweza kuutokomeza ugonjwa huu kama watu watakuwa na elimu ya kutosha," amesema Munisi.
"Hatuwezi kufanya mazoezi kwa kificho maana hii ni timu ya taasisi na kila hatua uongozi wetu lazima ufahamu kwa maana hiyo ni vigumu wachache kufanya maamuzi yao."
Wakati huohuo, Katibu Mkuu wa Tanzania Prisons, Adamu Kifukwe alisema wachezaji wao baada ya kutawanyika alitengeneza kundi WhatsApp ambalo linatumika kuelimisha wachezaji.
"Baada ya kuvunja kambi, wachezaji wakawa wanapewa kila siku elimu ya kujikinga na corona kwa njia ya WhatsApp kupitia wataalamu tuliokuwa nao."
Prisons ambayo inakamata nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 40, imewapa wachezaji wake mapumziko ya siku 30 kama agizo la serikali lilitolewa  awali.