Pogba na Mahrez walivyopikwa pamoja huko Ufaransa

Muktasari:

  • Cheki hapa orodha ya wanasoka mastaa walioibukia kwenye akademia ya Le Havre.

PARIS, UFARANSA .MANCHSTER United ilishitua ulimwengu wakati ilipolipa Pauni 89 milioni kunasa huduma ya kiungo Paul Pogba kutoka Juventus.

Jambo hilo lilishtua kwa sababu miaka minne nyuma, Pogba alikuwa mchezaji wa Man United na aliondoka bure kabisa Old Trafford kwenda kujiunga na Juventus na kilichofanywa na wababe hao wa Turin ni kulipa tu fidia ya Pauni 400,000 kwa sababu Man United walimkuza mchezaji huyo na alikuwa akitumia vifaa vyao vya michezo.

Kitendo cha Pogba kununuliwa kwa pesa nyingi iliyovunja rekodi ya uhamisho kwa wakati huo liliwafurahisha Le Havre kwa sababu ni mchezaji aliyewahi kupita kwenye akademia yao.

Hata hivyo, Pogba si mchezaji pekee aliyekuja kuwa maarufu kwenye soka la dunia, ambaye alipita kwenye akademia ya Le Havre kwani pia yupo Riyad Mahrez, Dimitri Payet na wengine kibao.

Cheki hapa orodha ya wanasoka mastaa walioibukia kwenye akademia ya Le Havre.

Paul Pogba

Pogba ni mchezaji ambaye hakika Le Havre wamekuwa wakimtumia kama mfano kwa makipa wao katika kuwahamasisha kwamba hakuna kisichowezekana kama utaweka bidii ya jambo fulani.

Pogba alijiunga na Le Havre mwaka 007, na licha ya kwamba alidumu kwa misimu michache kwenye timu hiyo, lakini kiwango chake kwenye akademia kilikuwa muhimu kiasi cha kumfanya kuwa mchezaji mkubwa akienda kujiendeleza huko Manchester United kabla ya kwenda Juventus na kisha kurudi tena Man United.

Lassana Diarra

Kama ilivyo kwa wachezaji wengine mahiri, Diarra alikumbana na wakati mgumu kupata nafasi kwenye soka kwa sababu akademia nyingi zilimwona kuwa mwili mdogo na dhaifu. Lakini, Le Havre waliamua kumpa nafasi katika msimu wa 2003/04. Baaada ya kupewa nafasi ya kucheza, Diarra alianza kuonyesha uwezo mkubwa wa soka kiasi cha kumvutia kocha kama Jose Mourinho na kuamua kumjumuisha kwenye kikosi chake cha Chelsea.

Diarra alipita kwenye timu nyingi kubwa ikiwamo Real Madrid na PSG na hivyo kusahau kabisa yaliyokuwa yakimtokea huko nyuma ambako alikuwa akionekana kuwa na mwili mdogo na uliogoigoi.

Florent Sinama Pongolle

Sinama Pongolle alizaliwa katika kisiwa cha Réunion, lakini alijiunga na Le Havre ikiwa ni sehemu ya ushirikiano na Saint-Pierroise, klabu inayopatikana katika visiwa hivyo na hilo lilifanyika wakati akiwa mdogo sana.

Alikuwa kwenye akademia hiyo ya Le Havre kwa miaka sita kabla ya kwenda kujiunga na Liverpool sambamba na binamu wake Anthony Le Tallec, licha ya kwamba alicheza mechi chache sana. Lakini, wachezaji hao wote walirudi Le Havre kwa mkopo wa miaka miwili kama ilivyokuwa kwenye makubaliano ya dili lao.

Steve Mandanda

Wengi wanamtambua kama kipa matata zaidi akiwa na kikosi cha Marseille, lakini ukweli ni kwamba Steve Mandanda alicheza zaidi ya mechi 70 akiwa kwenye kikosi cha Le Havre kabla ya kwenda kujiunga na timu kubwa.

Alidaka bila ya kuruhusu bao kwenye mechi yake ya kwanza ya Le Havre, kitu ambacho kilitoa ishara kubwa kwamba atakwenda kuwa kipa mahiri na kufanya hivyo kwa muda wote aliokuwa na Marseille, ambako aliondoma pia kwenda Crystal Palace na kisha kurudi tena.

Mamadou Niang

Licha ya kutumikia utoto wake kwenye kikosi cha Le Havre, walikuwa Troyes ndio waliomfanya Niang kuwa mwanasoka wa kulipwa. Lakini, hilo halijatokea kwa haraka hadi hapo alipojiunga na Strasbourg ambako alionyesha kiwango bora kabisa na kisha kinaswa na Marseille alikokwenda kufanikiwa zaidi.

Iwe acheze pembeni au kati, Niang alikuwa mchezaji mahiri na mwenye mvuto kumtazama. Baada ya kupita katika nchi za Uturuki na Qatar, Niang alirudi zake Ufaransa kujiunga na Arles-Avignon na alitangaza kustaafu baada ya kuachwa Julai 2015.

Guillaume Hoarau

Hoarau alifanya safari kutoka Saint-Pierroise hadi Le Havre, lakini ilimbidi kusubiri kidogo kabla ya kuanza kupata nafasi kwa sababu klabu hiyo ilikuwa ikimwona mwembamba sana kuanza kumtumia kwenye mechi.

Baadaye Hoarau alianza kupata nafasi na mkataba wake wa kwanza wa soka la kulipwa alisaini akiwa na umri wa miaka 20. Ilimchukua muda mwingine pia kabla ya kujitengenezea namba ambapo fowadi huyo alipita chini ya makocha wanne na timu kadhaa za mikopo kabla ya kuanza kufunga mabao kiasi cha kuwavutia Paris Saint-Germain na kuja kumsajili.

Dimitri Payet

Jina la Payet lipo juu sana. Staa huyo alikuwa kwenye kikosi cha West Ham United kabla ya sasa kukipiga kwenye chama la Olympique Marseille. Kama ilivyo kwa Hoarau na Sinama Pongolle, alihama kutoka kwenye kisiwa cha Réunion kwenda Le Havre ikiwa ni sehemu ya ushiriki wao.

Payet alisikitika sana baada ya kushindwa kuwamo kwenye kikosi cha Ufaransa kilichokwenda kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018 na kubeba ubingwa. Huko Marseille huduma yake ni muhimu na panga pangua amekuwa hakosi kikosini. Katika msimu wa 2017-18 alifunga mabao sita na kuasisti mara 13 katika mechi 31 alizocheza kwenye ligi.

Carlos Kameni

Baada ya kuisaidia Cameroon kushinda medali ya dhahabu kwenye Olimpiki ya 2000 akiwa na umri wa miaka 16, kipa Kameni alisajiliwa na Le Havre na kwenda kuwa mrithi wa Alexander Vencel, ambaye kwa wakati huo alikuwa kwenye umri wa miaka 30.

Hata hivyo, Kameni alishindwa kupata namba kwenye kikosi cha kwanza na hivyo akaachwa aende Espanyol, huku Mandanda akiibukia kutoa kwenye academia ya Le Havre. Hakika, Kameni anahesabika kama mmoja wa makipa mahiri zaidi waliowahi kutokea kwenye Bara la Afrika na amewahi kucheza kwenye vikosi vya Fenerbahce na Malaga.

Riyad Mahrez

Mahrez kiufundi kahuanzia kwenye academia ya Le Havre. Alicheza Quimper na kuwa profesheno huko kabla ya kwenda kujiunga na klabu hiyo ya Ufaransa. Lakini, akiwa na Le Havre ndipo mahali alipoanza kuonyesha makali yake makubwa kwenye soka na ndipo hapo alipowavutia Leicester City na kwenda kumsajili.

Mahrez alishinda tuzo ya Mchezaji Bora wa England katika msimu wa 2015/16 baada ya kuwasaidia Leicester City kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England. Huduma yake bora ilimpatia ulaji zaidi baada ya kusajiliwa na Manchester City kwa ada ya Pauni 60 milioni.

Benjamin Mendy

Mendy ni staa mmoja kati ya wengi walioanzia maisha yao ya soka katika kikosi cha Le Havre kabla ya kwenda kujiunga na Marseille. Hakika Mendy anahesabika kama mmoja wa mabeki bora kabisa wa kushoto kuwahi kutokea kwenye soka la ulimwengu na huduma yake bora iliwafanya Monaco kulipa Pauni 10 milioni kumsajili.

Kiwango bora kwenye kikosi cha Monaco kilimpa nafasi Mendy ya kuonekana na Manchester City na hivyo kumsajili kwa uhamisho wa Pauni 52 milioni na sasa anawashika kwenye Ligi Kuu England akitamba na kikosi hicho cha Etihad.

Jean-Alain Boumsong

Boumsong aliwahi kuzichezea pia Newcastle United, Juventus na Lyon katika kipindi cha maisha yake ya soka, lakini Le Havre ndiko mahali alikoanzia soka lake, alipotua Ufaransa akiwa na umri wa miaka 14.

Boumsong aliondoka Le Havre baada ya kushuka daraja na kwenda zake kushinda taji la Coupe de France akiwa na kikosi cha Auxerre na baadaye Lyon. Alibeba pia ubingwa wa Ligi Kuu Scotland na Ligi Kuu Ufaransa katika kipindi cha maisha yake kwenye mchezo huo wa soka.

Vikash Dhorasoo

Si jina linalokumbukwa na kila mtu, lakini asikwambia mtu, Dhorasoo alivutia sana wakati mpira ulipokuwa kwenye miguu yake. Bingwa wa kukokota mipira huyu aliyewahi kutokea kwenye Ligue 1.

Alizaliwa karibu na Le Havre, hivyo haikuwa kitu cha ajabu baada ya kumwona akianzia maisha yake ya soka kwenye timu hiyo kabla ya kujitengeneza na kuwa mchezaji mkubwa kwenye soka. Alitamba zaidi na Lyon, ambako alishinda mataji mawili ya Ligue 1.

Souleymane Diawara

Diawara alicheza zaidi ya mechi 100 za ligi akiwa na kikosi cha Le Havre kabla ya kushuka daraja na hivyo akatimkia zake Sochaux.

Alikuwa kwenye sehemu ya kikosi kilichoshinda ubingwa wa Coupe de Ligue msimu wa 2003/04 na alikwenda kushinda taji hilo mara tatu zaidi alipokuwa na vikosi vya Bordeaux na Marseille, ambako alishinda pia ubingwa wa Ligi Kuu akiwa na timu hizo zote mbili.