Pogba: Mbona Barca sio ishu

Tuesday September 11 2018

 

PAUL Pogba amekiri amekuwa na matatizo na kocha wake, Jose Mourinho, lakini jambo ambalo halijawahi kuwa ishu kwake ni kutaka aachane na Manchester United ili akajiunge na Barcelona kama inavyovumishwa.

Staa huyo Mfaransa jina lake lilihusishwa na Barcelona karibu kwa kipindi chote cha usajili wa dirisha la majira ya kiangazi huko Ulaya kabla ya staa huyo kubaki Old Trafford huku kukiwa na ripoti nyingine huenda akaenda kutua Nou Camp kwenye dirisha la Januari.

Ugomvi wake na Mourinho umeelezwa kumfanya kiungo huyo ghali kabisa kwenye Ligi Kuu England kuhusishwa pia na mpango wa kurudi Juventus, huku ripoti za karibuni zikidai kuna dili la kubadilishana na Paulo Dybala linaweza kufanyika.

Lakini Pogba mwenyewe alisema hawezi kuzungumzia mambo ya usajili kwa sababu yupo kwenye mkataba wa Man United.

“Sawa kumekuwa na mambo mambo na kocha, uhusiano wetu bado upo vilevile wa kocha na mchezaji.

“Tuna malengo yaleyale ya kushinda. Hivyo kwa kadiri mnavyoniona sipo kwenye jezi za Barcelona, kwa sababu nipo Manchester United na hayo mambo mengine siku zote ni ishu za uvumi tu,” alisema.

Pogba alitua Man United kwa mara ya pili mwaka 2016 akitokea Juventus ambapo saini yake iliwagharimu wababe hao wa Old Trafford kiasi cha Pauni 89 milioni.

Advertisement