Pochettino kanaswa na mshauri wa Woodward

Thursday February 13 2020

Pochettino kanaswa na mshauri wa Woodward,Ole Gunnar Solskjaer ,Ligi Kuu England ,Manchester United,

 

LONDON, ENGLAND. MAMBO yamenoga. Bila ya shaka, Ole Gunnar Solskjaer kwa sasa presha itakuwa imepanda akifikiria kibarua chake. Majuzi tu hapo, Mauricio Pochettino alisema kuhusu mpango wake wa kubaki England na kutafuta timu nyingine ya kuinoa kwenye Ligi Kuu England huku jina lake likihusishwa na Manchester United.

Lakini sasa presha inapanda zaidi kwa Ole, ambaye ndiye anayeinoa Man United baada ya Kocha Pochettino kuonekana akiwa na mshauri mpya wa bosi kubwa wa miamba hiyo ya Old Trafford, Ed Woodward.

Pochettino na mshauri huyo wa Ed, Neil Ashton walipigwa picha wakiwa pamoja katika mechi baina ya Brentford na Leeds United na walionekana kuwa na mazungumzo jambo lililoibua mjadala mzito, huenda ni mwanzo wa kusuka mpango wa Muargentina huyo kwenda kunasa kibarua cha kuinoa Man United.

Pochettino hana muda tangu alipofutwa huko Tottenham, Novemba mwaka jana, lakini tangu wakati huo amekuwa akihusishwa na kiti hicho cha Old Trafford kinachokaliwa na Solskjaer. Na baada ya picha ya pamoja na Poch na mshauri wa Woodward imezua mjadala mzito na kuonekana, huenda mwisho wa msimu kukatokea dili hilo matata huko kwa Mashetani Wekundu.

Taarifa zimekuwa zikidai, Ashton alikwenda kwenye mechi hiyo kama mgeni wa Brentford na si kama alikuwa kwenye majukumu yake. Hata hivyo, wengine wanadai kunaweza kukawa na mazungumzo kidogo kuhusu dili la kwanza Man United baada ya wawili hao. Pochettino aliandamana na msaidizi wake, Jesus Perez walipokwenda kwenye mechi hiyo Griffin Park, ambako imedaiwa ni marafiki wa karibu wa Kocha wa Leeds, Muargentina Marcelo Bielsa.

Poch alisema: “Ningependa kufanya kazi kwenye Ligi Kuu England. Itakuwa shughuli pevu, nafahamu hivyo, lakini hebu tusubiri tuone kitakachotokea.”

Advertisement

Advertisement