Pluijm azitupia dongo Simba, Yanga

Muktasari:

Alisema kwa Afrika Mashariki dabi ya Kariakoo ndio yenye msisimko zaidi lakini hiyo haitoshi kwa ukubwa wa klabu hizo, wanatakiwa kushindana anga za kimataifa.

Dar es Salaam. Kocha wa zamani wa Yanga, Hans van der Pluijm amesema umefika wakati kwa wakongwe, Simba na Yanga kutunishiana misuli katika mashindano makubwa Afrika na Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA) pekee.

Wakati joto la mchezo wa watani wa jadi likianza kushika kasi baada ya hapo jana Simba na Yanga kucheza michezo yao ya Ligi Kuu Bara, Pluijm alisema zikifikia hatua hiyo ndio zitaongeza msisimko kwenye mechi za dabi barani Afrika.

Alisema kwa Afrika Mashariki dabi ya Kariakoo ndio yenye msisimko zaidi lakini hiyo haitoshi kwa ukubwa wa klabu hizo, wanatakiwa kushindana anga za kimataifa.

“Nilisikia Simba wamepiga hatua katika mabadaliko, Yanga wanafuata ni hatua kubwa kwao, wanatakiwa kuwa na mifumo ambayo itawafanya kuwa juu kiuchumi kulingana na ukongwe wao.

“Wanatakiwa kuonyesha ushindani katika michuano ya kimataiafa, hapo watazidi kuwa imara na haitokuwa ajabu kuona wakikutana katika Ligi ya Mabingwa au Shirikisho Afrika katika hatua za juu. Inawezekana,” alisema kocha huyo.

Pluijm, ambaye ana makazi yake nchini Ghana alisema kubweteka kwa kuangalia mafanikio ya ndani ni kujidumaza. “Kazi yetu ni kuwakumbusha hivyo, ni vyema kuondokana na yale yale mawazo mgando.”

Kocha huyo ambaye pia aliwahi kuzinoa Azam na Singida United, alisema kama wakiwa na mipango makini basi basi ushindani wao ukahamia anga za kimataifa.