Picha limewachenjia

SOKA ni mchezo pendwa sana duniani lakini una mambo ya kikatili ikiwemo furaha, karaha, utani, majonzi, burudani na huzuni pasi kusahau faida na hasara zake.

Miongoni mwa vitu viliyopo kwenye soka ni mchezaji ama wachezaji kutamba kwa kipindi fulani kisha wakaangukia pua. Hili limekuwa likiwatokea sana mastaa wengi duniani na hapa Bongo pia.

Mwanaspoti linakuletea orodha ya nyota waliowika msimu uliopita 2019/20, lakini msimu huu ikiwa tayari zimechezwa mechi zaidi ya 7 kwa kila timu inaonekana hali kwao ni tete meza imewapindukia vibaya.

WAZIR JUNIOR (YANGA)

Licha ya timu yake ya msimu uliopita (Mbao) kutofanya vizuri na kushuka daraja, Waziri JR aliibuka shujaa klabuni hapo akifunga mabao 12 na mengine mawili akifunga kwenye Kombe la FA na hapo Yanga wakamnasa.

Tangu ajiunge na wananchi hao wa Jangwani msimu huu, mambo yanaonekana kutokwenda vizuri kwake kwani ameshindwa kupata namba ya uhakika mbele ya Michael Sarpong na Yocouba Sogne. Lakini, juzi aliibeba Yanga kwa kuifungia bao la ushindi dhidi ya KMC.

BENARD MORISSON (SIMBA).

Moja kati ya nyota walioongeza utamu kwenye Ligi Kuu Bara msimu uliopita ni Morrison. Ndani ya kikosi cha Yanga alionekana kuwa mkombozi huku staili yake ya udambwidambwi ikiwapa mzuka mashabiki. Ghafla tu akaibukia Msimbazi ambako licha ya utata wa usajili wake, lakini jamaa anaonekana kama amepotea.

Msimu huu akiwa Simba, Morisson hajaonesha makali yake kama alivyokuwa Yanga licha ya kuwa watu na wadau mbalimbali wa soka walimtabiria kufanya makubwa, lakini mpaka sasa mambo hayapo vizuri.

PETER MAPUNDA (DODOMA JIJI)

Huyu jamaa msimu uliopita alikuwa ndiye nahodha wa Mbeya City akicheza kwa ubora mkubwa licha ya kuwa timu yake ilikuwa kwenye hatari ya kushuka daraja.

Msimu huo Mapunda alifunga mabao 12 ma kuisaidia timu yake kutokushuka daraja na msimu huu ameibukia Dodoma Jiji ambayo imepanda daraja Ligi Kuu, lakini mpaka sasa hajaonyesha makali yake akiwa ndani ya uzi wa walima zabibu hao wa makao makuu, Dodoma.

AWESU AWESU (AZAM)

Moja kati ya wachezaji waliobarikiwa kipaji cha soka, Awesu Awesu msimu uliopita alikuwa Kagera Sugar ambako aling’ara akicheza katikati sambamba na viungo wenzake kina Zawadi Mauya na Abdallah Sesseme.

Msimu huu amejiunga na matajiri wa Dar es Salaam, Azam FC na hajaonyesha makali yake uwanjani kwani, mechi nyingi amekua akikaa benchi huku dimbani wakicheza viungo kama Mudathir Yahya, Salum Abubakar, Ally Niyonzima na Frank Domayo.

GERALD MDAMU (BIASHARA UNITED)

Msimu uliopita huyu jamaa aliuwasha moto huko Mwadui akicheza kwa kiwango bora huku akiwalaza na viatu mabeki wa timu pinzani.

Kocha wa Biashara, Francis Baraza alipomuona akamvuta Kanda Maalumu na kumpa mkataba, lakini sijui nini kimemkumba. Mdamu hajaonyesha shughuli kama alivyotarajiwa na amekuwa akikaa benchi huku Kelvin Friday, Omary Daga na Mpapi Nasibu wakisimama mbele ya lango la adui.

SAID JUMA MAKAPU (YANGA)

Hiki ni chuma ambacho kipo stoo ya Yanga tangu kitambo, lakini msimu uliopita Makapu alipata nafasi ya kuwika chini ya kocha Luc Emael (alifukuzwa), ambaye alimtumia kama beki wa kati akicheza sambamba na Lamine Moro jambo lililowapa imani mashabiki kuwa gari la jamaa limewaka kutokana na kazi nzuri aliyokuwa akiifanya uwanjani. Msimu huu ameonekana kuutumia sana akiwa benchi huku Bakari Mwamnyeto ‘Nondo’ akisimama kulinda ukuta wa Yanga.

ISMAIL AZIZ (AZAM)

Moja kati ya mawinga tishio ambao mabeki msimu uliopita waliteseka sana. Huyu ni Ismail Aziz, ambapo akiwa na Tanzania Prison alikuwa moto kwelikweli. ana soka la kasi, kontroo na akili kubwa ya kucheza soka, lakini tangu asajiliwe na Azam FC msimu huu meza imempindukia na kushindwa kufiti kwenye mfumo wa Kocha kocha Aristica Cioaba.

PAUL NONGA (GWAMBINA)

Mkongwe huyu kwanye Ligi Kuu msimu uliomalizika alikua mkoani Iringa akipeperusha bendela ya Lipuli huku akifunga mabao 11, kabla ya timu hiyo kushuka daraja na yeye kutua zake Gwambina.

Akiwa huko Gwambina bado hajaonesha makali yake uwanjani huenda ikawa majeraha yanayomuandama ndiyo sababu ya kuwa nje ya uwanja karibu nusu ya michezo waliyocheza vijana hao wa wilayani Misungwi.

IBRAHIM AME (SIMBA)

Moja kati ya sajili za kimafia zilizofanyika kwenye dirisha la usajili msimu huu, ilikua ni hii ya Ame. Beki kitasa kabisa aliyesainishwa na mabosi wa Simba wakati huo akiwa na ofa ya Yanga, Polisi na Coastal wenyewe walitaka kumpa dili jipya.

Lakini, wakati huo akiwa Coastal Union msimu uliopita alitengeneza pacha moja matata sana akiwa na Mwamnyeto hadi kupelekea watu wa mkoani Tanga kuwabatiza jina la ukuta wa chuma.

Baada ya kujiunga na Simba, Ame amekosa nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza ambapo vitasa kina Joash Onyango, Pascal Wawa na Kennedy Juma wamekuwa wakisimama kama walinzi wa kati kwenye michezo ya wekundu hao wa msimbazi.

SHABAN KADO (MTIBWA)

Ukizungumzia makipa wakongwe kwenye Ligi Kuu waliodumu kwenye ubora wao kwa muda mrefu basi huwezi kukosa kumtaja Shaban Kado wa Mtibwa Sugar. Msimu uliopita Kado alisimama langoni kwa wakata miwa hao wa Turiani, Morogoro na kufanya makubwa sana ikiwemo kuisaidia timu kukwepa kushuka daraja kulingana na mwisho mbaya waliokuwa nao.

Msimu huu meza imempindukia baada ya Kinda Aboutwalib Msheri kupona majeraha na kurejea uwanjani akiwa na ubora wa hali ya juu jambo linalomfanya kuwa chaguo namba moja la kocha mkuu wa timu hiyo Vicent Barnabas hata kwa Zuber Katwila kipindi bado anainoa timu hiyo kabla ya kuhamia Ihefu FC ya Mbarali, Mbeya.

FRANCIS KAHATA (SIMBA)

Kiungo mbinifu wa Simba mwenye jina lake huko Kenya, Kahata. Wakati anatua kutoka Gor Mahia, kila mmoja alisema Simba imelamba dume kutokana na staili yake ya uchezaji uwanjani. Kahata huwa hashikiki wala hakabili kirahisi hasa anapokuwa sambamba na winga Liuz Miqssone na kiungo fundi Cloatus Chama. Hata hivyo, msimu huu ameibuka Larry Bwalya na Morrison ambao majina tu yanawapa uhakika wa kumtuliza benchi. Kahata huenda akashindwa kuonyesha makali yake kama zaidi.