Pellegrino awagomea Waturuki, TFF yasogea mezani

MZANZIBAR anayetikisa kwa sasa barani Ulaya, Amahl Pellegrino ameigomea kweupe ofa ya kujiunga na Gazisehir Gaziantep inayoshiriki Ligi Kuu Uturuki huku akisema kuwa bado yupo yupo kwanza.

Mshambuliaji huyo ambaye anaongoza orodha ya wafumania nyavu huko Norway akiwa na Kristiansund BK, alisema anajiona mwenye furaha hivyo ndio maana ilikuwa rahisi kuigomea Gaziantep.

“Nilielezwa na viongozi wa klabu yangu kwamba kuna ofa kutoka Uturuki, walitaka kujua kama nipo tayari kuondoka, kiukweli najiona mwenye furaha hapa na sina maana kwamba sitaondoka. Muda ukifika, hakuna ambacho kitatatiza lakini sio kwa sasa.

“Tumekuwa na msimu bora nahitaji kuhakikisha naisaidia klabu yangu kufikia malengo ambayo kila shabiki wetu alikuwa akitamani kuona tukiyafikia, nataka kuwa sehemu ya historia,” alisema.

Mshambuliaji huyo anaongoza orodha ya wafumania nyavu wa Norway akiwa na mabao 19 aliyofunga katika michezo 20 huku akifuatiwa na Philip Zinckernagel na Jens Hauge (wote wa Bodo) wakiwa na mabao 14, wamezidiwa mabao matano kila mmoja.

Shauku ya Pellegrino mwenye miaka 30 kwa sasa ni kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya. Alionyesha hilo wakati ilipokuwa ikipangwa droo ya makundi ya michuano hiyo mikubwa barani Ulaya.

Aliposti picha kwenye sehemu ya ‘Insta story’ kwenye ukurasa wake wa Instagram kwa kusema ipo siku ndoto yake itatimia huku akiweka matokeo ya droo ilivyochezeshwa huko Uswisi.

Wakati huo huo, inasemekana vigogo wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wamefanya mawasiliano na mashambuliaji huyo mwenye asili ya Zanzibar ili aitumikie timu ya taifa la Tanzania ‘Taifa Stars’.

Tangu kuwepo kwa mawasiliano hayo, Pellegrino amekuwa mfuasi mpya wa mitandao ya kijamii ya shirikisho hilo la soka la Tanzania.