Pato aipotezea Yanga kama haijui

Saturday August 17 2019

 

By Olipa Assa

YANGA ilijikuta ikiambulia kichapo cha ba0 2-0 katika mechi ya kirafiki na Polisi Tanzania, mbele ya nyomi ya mashabiki ambao wamejitokeza kuwaunga mkono, ikiwa kwenye maandalizi ya kuelekea mechi ya marudiano na Township Rollers.
Ushindi ni raha asikuambie mtu, ndivyo alivyofurahia nyota wa zamani wa Yanga ambaye yupo Polisi Tanzania, Pato Ngonyani kwamba inawajengea ujasiri na kuendelea kujiamini kwa mechi zinazokuja mbele yao za kirafiki na ligi kuu Bara, itakayoanza Agosti 23.
Ngonyani alikuwa mchezaji wa zamani wa Yanga, ambapo ataitumikia Polisi Tanzania kwa mkataba wa mwaka mmoja, amedai kazi yake ni kucheza hivyo atakapokutana na timu yoyote ni kuonyesha ushindani.
"Tunachofanya kwa sasa kinaleta picha kamili ya nini tutakifanya kwenye ligi kuu inayokuja, lazima tuanzie kwenye maandalizi haya mfano mechi tunazocheza,"anasema.
Amesema ndani ya uwanja hakuna kujuana kwa madai kila mchezaji anakuwa anapigania ndoto ya timu yake, jambo analoamini ndilo lililotokea wakati wa mechi ya kirafiki na Yanga.
"Baada ya dakika 90 tunapiga stori kama kawaida na washikaji ila ndani ya uwanja kila mmoja anatetea ugali wake na kuheshimisha kiwango chake, hivyo nisingeweza kucheza kwa ulegevu kisa Yanga nimeichezea," amesema.
Pia anaamini Yanga ipo vizuri kila idara, kikubwa anawashauri wachezaji kujiamini ili kwenda kuwafunga Township Rollers kwao.

Advertisement