Papy Tshishimbi: Kuna Niyonzima mmoja tu duniani

Thursday June 18 2020
Niyonzima pic

SIO kitu cha ajabu, lakini ukeli ni kwamba kuna wakati kama mchezaji unaweza kujikuta unamshangaa mchezaji mwenzako. Kitu kitakachokufanya kumshangaa ni ubora alionao. Unafurahia zaidi hasa pale unapokuta kipaji chake kinasaidia kazi yako pia sehemu uliyopo.

Sikusafiri na timu hivi karibuni katika mechi mbili ya Mwadui na ile leo (jana) dhidi ya JKT Tanzania pale jijini Dodoma, lakini acha niizungumzie sana ile mechi ya pale Shinyanga dhidi ya Mwadui.

Mechi ile niliiangalia nikiwa nyumbani nimepumzika. Kama mnavyojua nipo katika siku za mwisho tangu nipate maumivu ya mguu wangu. Nilifurahia sana mchezo ule kwani hakuna kitu kilinivutia kama ubora wa kiungo Haruna Niyonzima. Mlimuangalia vyema katika mchezo ule?

Yule ndiyo Niyonzima ninayemuona yupo mmoja tu duniani na bahati nzuri zaidi alizaliwa kuichezea Yanga na sio klabu nyingine labda atoke kwenda huko Ulaya walikopiga hatua zaidi.

Niyonzima alikuwa katika ubora wake mkubwa alisambaza mipira anavyyotaka alizunguka karibu uwanja mzima lakini mwiso kila pasi aliyopiga ilinisisimua na kutamani ningekuwa mshambuliaji kisha niwe ndani ya uwanja niweze kufunga, alikuwa zaidi ya kiungo.

Mwisho wa mchezo nilitamani kila wakati niwe shabiki na kumuangalia Niyonzima akiwa uwanjani. Inawezekana ni ukongwe wake na ubora wake wa kuuchezea mpira anavyotaka ndio vitu vinamsaidia kwani jamaa ni mtu bora sana.

Advertisement

Niyonzima nimekutana naye wa aina mbili kuna yule aliyekuwa Simba wakati nafika hapa lakini kuna Niyonzima nimekutana naye Yanga msimu huu. Hawa ni watu wawili tofauti. Ngoja nifafanue zaidi muweze kunielewa.

Niyonzima alipokuwa Simba pengine hakupata bahati nzuri kwani sikuona kama ni mtu hatari sana. Kuna muda mrefu hakuwa anacheza lakini kidogo nilikuja kuona makali yake katika ule mchezo wa Simba dhidi ya AS Vita hapa Dar es Salaam pale alionyesha ukomavu mkubwa.

Uwepo wake ndani ya uwanja kati yake na Clatous Chama uliibeba Simba katika mchezo ule. Nakumbuka hata Vita mpaka wanaondoka walinitajia jina lake kwamba Niyonzima ndiye aliyebadili mchezo ule na hata kuisaidia Simba kuwaondoa kwenye mashindano.

Baadaye nikaja kumuona Niyonzima wa Yanga. Rafiki zangu wengi wananiambia huyu ndiye mwenyewe na anaweza kuendelea kucheza hivi kwa muda zaidi hakika unafurahia ukimuona anavyocheza uwanjani.

Ninapokuwa nacheza kiungo wa chini hakuna kitu nafurahia kama kumpa mpira Niyonzima hasa akiwa ameshavuka au anakaribia kuvuka nusu ya uwanja wa eneo letu. Hapo anakuwa hatari sana. Ni kiungo ambaye anaweza kuonekana kama anakwenda kulia lakini kumbe anaona kila kitu upande wa kushoto na akigeuka kuna pasi ya madhara anaweza kuipiga.

Nilianza kumuelewa sana pale tulipocheza dhidi ya Simba na kushinda bao 1-0. Kuna wakati nilitamani kumwambia mdogo wangu Feisal Salum wakati tukiwa uwanjani kwamba kama akipata mpira tu haraka amsukumie Niyonzima kisha mmoja kati yetu asogee juu kumsaidia alikuwa bora pia mchezo ule.

Bahati nzuri sana hapa Yanga mashabiki wengi wanampenda na yeye anajua kuwapa kile wanachotaka hasa akiwa uwanjani. Uzoefu wake umekuwa msaada mkubwa hata kuwakumbusha majukumu mbalimbali uwanjani wenzake na hapo ndipo uzoefu wake unapokuwa na tija ndani ya Yanga.

Kuna safari ndefu sana kwa viungo wengi wachezeshaji. Wanatakiwa kujifunza anachokifanya Niyonzima na haitakuwa hatua mbaya kama utaiga mazuri yake kisha kuamua kujibadilisha taratibu. Kiungo mchezeshaji lazima anapogusa mpira awe tishio na sio rahisi kutabirika kwa kile atakachofanya.

Yapo ambayo najifunza kwake kama elimu, siku zote elimu haijawahi kuwa na mwisho. Shida kubwa wachezaji wengi hatupendi kuwa wa kweli kwa kile kizuri ambacho mwenzako anacho. Hatua hiyo ni ngumu kuweza kuwa na nafsi ya kujifunza kitu kisha nawe ukanufaika.

Bahati nzuri Niyonzima yupo Yanga nafurahia uwepo wake ndani ya kikosi chetu, lakini kama ambavyo wanachama na mashabiki wanafurahi nami nafurahia kazi yake. Ni wakati wa washambuliaji wetu kutulia na kuhakikisha wanatumia pasi zake kupeleka vilio kwa wapinzani mbali-mbali tutakaokutana nao huko mbele.

Advertisement