PARREIRA: Kocha asiyecheza soka, mwenye maajabu yake

MAAJABU yapo katika kila fani ya maisha na hali hii pia inaonekana katika michezo mbalimbali.

Katika soka mara nyingi pakisimuliwa maajabu waliyofanya baadhi ya makocha mashuhuri wa soka, jina la kocha maarufu wa zamani wa Brazil, Carlos Alberto Gomes Parreira haliwezi kuachwa.

Hii inatokana na kocha huyo kuwa miongoni mwa makocha mashuhuri wazuri kwa miaka 30 tangu mwanzoni mwa miaka ya 1980.

Kocha huyo ameacha rekodi nzuri ya kuwepo katika fainali sita za Kombe la Dunia - mara mbili na Brazil 1994 na 2006 na vikosi vya Kuwait (1982), Falme za Nchi za Kiarabu (1990), Afrika Kusini (1994, 2006 na 2010) pamoja na Saudi Arabia (1998).

Parreira ambaye sasa ana miaka 71 ni mwanachama maarufu wa klabu ya Fluminense ya Brazil na mpaka leo ikiwa na mchezo mkubwa hufika uwanjani kuishangilia.

Aliiongoza klabu hiyo kuwa mabingwa wa Brazil mwaka 1984 na mabingwa wa Ligi Daraja la Tatu mwaka 1999.

Parreira alizaliwa Februari 27, 1943 na aliiongoza Brazil kushinda Kombe Dunia 1994, Copa América (2004) na Kombe la Shirikisho (2005).

Kocha pekee aliyewahi kuzifundisha timu mbili tofauti na kushinda Kombe la Asia.

Maajabu makubwa ya kocha huyo ni kwamba hakuwahi kucheza soka, lakini aliupenda sana mchezo huu kama mtazamaji.

Tangu alipokuwa mdogo alipenda kuangalia wenzake wanacheza na mara nyingi timu yake ilipocheza alikwenda kutoa ushauri wakati wa mapumziko.

Pereira mbali ya kuzifundisha timu za mataifa mbalimbali, pia alizifundisha klabu kubwa na ndogo katika nchi za Amerika Kusini, Bara la Ulaya, Uarabuni, Asia na Afrika.

Miongoni mwa klabu maarufu za Brazil alizozifundisha ni São Cristóvão (1967), Vasco da Gama (1969) na Fluminense (1970–1974).

Safari yake ya kuelekea kuwa kocha maarufu duniani ilianza mwaka 1967. Wakati ule, akiwa na miaka 23 alikuwa mwanafunzi wa elimu ya viungo katika chuo kikuu kimoja cha Rio de Janeiro, Brazil na kuonekana mwanafunzi mzuri.

Ghana ilikuwa inatafuta kila pembe ya dunia kocha wa soka na ilipoulizia Wizara ya Mambo ya Nje ya Brazil ilipata habari za Perreira aliyekuwa hana uzoefu, lakini ni mtaalamu.

Baada ya kupokea ombi la kwenda Ghana, Pereirra alikubali kwa masharti kwamba siasa zisiingizwe kwenye timu wala kiwanjani.

Hata hivyo, hakukaa Ghana muda mrefu baada ya kuona wanasiasa wanamuingilia katika kazi yake.

Alijiuzulu na kuamua kwenda Hanover, Ujerumani kuendelea na masomo ya ukocha wa soka na kufaulu vizuri sana.

Matokeo hayo yalisababisha kutakiwa awe kocha wa mazoezi ya viungo ya kikosi cha Kombe la Dunia cha Brazil cha kina Pele, Jairzinho na Tostao cha fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Mexico 1970.

Brazil ilibeba kombe hilo na hasa kwa kuwa na kikosi kizuri sana katika fainali hizo.

Kilichowashangaza wengi ni mwaka 1978, Kuwait ambayo timu yake ya taifa ilikuwa dhaifu sana ilipomtaka aende kuifundisha na kukubali.

Alipokubali makocha wenzake na waandishi mashuhuri wa michezo walisema alikuwa kaamua kupoteza heshima yake.

Naye alisema timu mbovu ndio aliokuwa akiitaka kwa sababu ataweza kuifinyanga na kuipandisha chati na kwa kweli alifanikiwa.

Alibadilisha mpango wa mazoezi na kuipangia michezo baada ya kila siku chache na wachezaji wake kupanda kiwango na kwa mshangao ikafanikiwa kukata tiketi ya Fainali za Kombe la Dunia za 1982.

Parreira mara nyingi alikata maombi ya kuifundisha tena Brazil kati ya mwaka 1998 na hatimaye alikubali mwaka 2002 kwa mashindano ya Kombe la Dunia.

Hii ni baada ya kutaka kocha wa Brazil wa wakati ule, Luiz Felipe Scolari alitimuliwa baada ya Brazil kufungwa na Mexico na Honduras.

Wakati wa kuelekea Fainali za Kombe la Dunia za 1990 Pereirra alizusha balaa alipomtoa katika kikosi chake mshambuliaji maarufu Romario de Souza Faria kwa maelezo kwamba alikuwa anaringa.

Baada ya kubembelezwa sana akamrudisha na Romario alipunguza maringo na kuwaheshimu wenzake.

Baada ya fainali hizo za Dunia za 2002 Parreira aliifundisha timu hiyo pamoja na Mario Zagallo.

Lakini baada ya Brazil kufungwa 1-0 na Ufaransa katika robo fainali vyombo va habari vya Brazil vikaongoza kampeni ya kutaka atimuliwe na hilo likafanyika.

Alijiuzulu kufundisha Juni 25, 2010 na kueleza kwamba hataki tena kazi ya kufundisha na ameamua kufurahia mchezo kama mtazamaji.

Carlos Alberto Parreira amewekwa na Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) kama mmoja wa makocha 50 bora walioshuhudiwa duniani.