Ozil anaachia ngazi majembe yanashuka

Tuesday June 11 2019

 

LONDON,ENGLAND.MESUT Ozil amebakiza siku chache sana za kuendelea kubaki kwenye kikosi cha Arsenal. Kinachosemwa huko Emirates ni kwamba kwa sasa wanatafuta mnunuzi tu wa kumchukua mchezaji huyo, hata kama wa kuchangia mshahara nusu.

Arsenal imechoshwa na shughuli ya kulipa mshahara wa Pauni 350,000 kila wiki, wakati Ozil mwenyewe siku hizi amekuwa hana maajabu kabisa uwanjani.

Wanachokifanya katika dirisha hili la majira ya kiangazi ni kutafuta timu ambayo itamsajili Mjerumani huyo hata kama kwa mshahara kiduchu, wao wataongezea mshahara mwingine ili tu aondoke kwenye kikosi chao kuliko kulipa wao yote Pauni 350,000 kwa wiki.

Wakati Arsenal ikijiandaa kuchana na Ozil, hii hapa orodha ya mastaa 10, ambao kama Kocha Unai Emery atawageukia, basi atakuwa ameziba pengo la Mjerumani huyo bila ya matatizo yoyote na maisha yataendelea kuwa matamu Emirates.

Yannick Carrasco (Dalian Yifang)

Kinachozungumzwa kwa sasa Yannick Carrasco anataka kuachana na soka la China na kurudi Ulaya. Arsenal imeshafahamu hiyo na kuchangamkia huduma yake ili aende akakipige kwenye kikosi chake.

Advertisement

Carrasco ni mmoja kati ya wachezaji wabunifu uwanjani na hakika Arsenal itakuwa imepata mtu mwafaka kama itamchukua akazibe pengo litakaloachwa na Ozil atakapofunguliwa mlango wa kutokea kwenye kikosi hicho.

Kocha Emery atakuwa amepiga bonge la bao kwa kumpata mchezaji huyo ambaye kwanza atakuwa anamlipa mshahara mdogo tofauti na pesa ndefu anayotoa kila wiki kulipia huduma ya hovyo kutoka kwa Ozil.

James Rodriguez –Real Madrid

Staa wa Colombia, James Rodgriguez anachoripotiwa ni kwamba ataondoka katika kikosi cha Real Madrid.

Kwa miaka miwili alikuwa akicheza kwa mkopo huko Bayern Munich, lakini sasa atarudi kwenye klabu yake ya Real Madrid, akienda kukutana na kocha yuleyule aliyemwondoa, Zinedine Zidane.

Arsenal inataka mchezaji wa kurithi mikoba ya Ozil itakapoamua kumfungulia milango ya kutokea rasmi na jambo hilo linamfanya Rodriguez kuwa mchezaji mwafaka kwenye nafasi hiyo.

Staa huyo amekuwa na uwezo mkubwa wa kucheza kama namba 10, eneo ambalo amekuwa akitumika pia Ozil huko kwenye kikosi cha Arsenal. Juventus nayo inaripotiwa kumtaka mchezaji huyo.

Isco – Real Madrid

Ujio wa Eden Hazard kwenye kikosi cha Real Madrid unamweka Isco kwenye wakati mgumu wa kuendelea kutamba katika kikosi hicho cha Los Blancos.

Wababe hao wa Bernabeu bado hawajamaliza usajili na pengine watanasa viungo wengine matata zaidi jambo litakalomfanya Isco kutafuta mlango wa kutokea ili kwenda kujiunga na timu itakayompa nafasi ya kucheza.

Arsenal inaweza kuchangamkia huduma yake hasa katika kipindi hiki ambacho inataka kuachana na Ozil baada ya kuona ubora wake wa uwanjani umeshuka kwa kiwango kikubwa sana.

Hata hivyo, Isco kama atakuwa anauzwa na Real Madrid basi saini yake itazipiganisha timu nyingi.

Cristian Pavon –Boca Juniors

Huko nyuma, Arsenal ilihusishwa na mpango wa kumsajili staa wa Boca Juniors, Cristian Pavon. Katika kipindi hiki ambacho wababe hao wa Emirates wanahusishwa na mpango wa kuachana na Ozil, basi wanaweza kukimbilia kwa Pavon kumwingiza kwenye timu yao kwa sababu ni aina ya wachezaji ambao wamekuwa na ufundi mkubwa sana wa kucheza timu anapokuwa uwanjani. Muargentina huyo ataifanya Arsenal kuwa na uwezo mkubwa wa kutumia fomesheni ya 4-3-3, ambapo atasimama kwenye fowadi sambamba na wakali Pierre-Emerick Aubameyang na Alexandre Lacazette.

Pavon ni mjanjamjanja sana anapokuwa uwanjani.

Pablo Fornals – Villarreal

Kiungo mshambuliaji wa Villarreal, Pablo Fornals ni mmoja kati ya wachezaji wanaosakwa sana huko Ulaya kwa sasa hasa ikizingatia huduma yake inaweza kupatikana kwa bei ya chini na pia ni bora.

Licha ya kwamba timu yake imekosa kidogo tu kushuka daraja, shukrani kwa kazi nzuri ya Santi Cazorla, Fornals bado anabakia kuwa mchezaji aliyecheza kwa kiwango kikubwa sana kwenye kikosi hicho na hilo halina mjadala.

Msimu uliopita hakuwa na makali sana kama ilivyokuwa msimu uliotangulia, lakini Arsenal kama itafanikiwa kuinasa huduma ya mchezaji huyo, basi watakuwa wameongeza kitu cha tofauti katika kikosi chao ambacho bila shaka msimu ujao kitaingia uwanjani kushindana.

Leon Bailey –Bayer Leverkusen

Bailey kwa upande wake ameweza kuonyesha kiwango kizuri huko kwenye Bundesliga. Huduma yake ya ndani ya uwanja ilizifanya klabu nyingi kufukuzia saini yake hasa ukizingatia umri wake bado mdogo sana.

Kuna wakati Chelsea ilikuwa ikihitaji saini yake Bailey, ambaye ameripotiwa anaweza kupatikana kwa ada ya Pauni 80 milioni.

Katika kipindi hiki ambacho Arsenal inaweza kuachana na Ozil, Kocha Emery anaweza kukimbilia kwa Bailey kupata huduma yake kwa sababu ni mchezaji ambaye atampa kitu cha ziada kwenye timu akienda kuunda ile safu ya washambuliaji watatu matata kabisa pamoja na Pierre-Emerick Aubameyang na Alexandre Lacazette.

Julian Draxler – PSG

Baada ya kupewa nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha PSG mwanzoni mwa maisha yake klabuni hapo, Julian Draxler sasa amejikuta kwenye wakati mgumu akilazimika kusubiri benchi kutokana na usajili wa wakati Neymar na Kylian Mbappe kikosini hapo.

Staa huyo wa kimataifa wa Ujerumani amekuwa akihusishwa na timu mbalimbali zinazohitaji saini yake huko PSG wenyewe wakiripotiwa kuwa tayari kumpiga bei ili kuweka sawa uwiano wa matumizi yao na mapato kwenye kikosi wasikumbwe na rungu na Uefa. Arsenal inaweza kuwa kwenye mikono salama kama itaamua kumchukua Draxler kuchukua mikoba ya Ozil.

Wilfried Zaha –Crystal Palace

Shida kubwa iliyopo kama Arsenal itakuwa na bajeti ya kutosha kuweza kumudu saini ya Wilfried Zaha.

Lakini hakuna ubishi kama wataamua kumsajili staa huyo wa Crystal Palace kwenda kuziba pengo la Ozil kwenye timu yao basi watakuwa wamefanya bonge moja la usajili, ambapo muda mfupi mashabiki watamsahau Ozil.

Uzoefu wake wa kucheza kwenye Ligi Kuu England utawafanya Arsenal kutokuwa na presha yoyote kama Zaha ataweza kumudu mikikimikiki ya ligi hiyo.

Uzuri wa kuwa na Zaha ni kwamba kocha anakuwa na wigo mpana wa kutumia fomesheni tofauti kwa msimu ujao ikiwamo ile ya 4-2-3-1, akimpanga upande wa kushoto.

Pablo Sarabia – Sevilla

Ubora wa Pablo Sarabia huko kwenye kikosi cha Sevilla kwa msimu uliomalizika hivi karibuni haukuwa wa shaka.

Staa huyo alikuwa na msimu bora kabisa akifunga mabao 12 na kuasisti mara 13 wakati akiisaidia timu yake kumaliza nafasi ya sita katika msimamo wa La Liga.

Bila ya shaka, Sevilla haitakubali kumwaachia kirahisi staa huyo aondoke kwenye kikosi chake. Lakini uzuri ni kwamba huduma yake inaweza kupatikana kwa Euro 18 milioni tu kutokana na mkataba wake, pesa ambayo bila ya shaka itakuwa ipo kwenye bajeti ya Arsenal kwenye usajili wa mwaka huu. Real Madrid ilihusishwa pia kuhitaji huduma yake.

Nabil Fekir –Olympique Lyon

Liverpool ilishindwa kumsajili kwenye dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana, huku mwaka huu ikidaiwa inataka kurudi tena huko Lyon kufanya usajili wa supastaa wake, Nabil Fekir.

Lakini, mchezaji huyo ataifaa zaidi Arsenal hasa katika kipindi hiki ambacho kinapiga hesabu za kumfungulia milango ya kutokea Ozil.

Fekir ni mmoja ya mastaa wa Ufaransa wenye uwezo mkubwa sana wa kuuchezea mpira ndani ya uwanja na hakika kama Arsenal ikifanikiwa kuinasa saini yake, basi washambuliaji wake Aubameyang na Lacazette watakuwa bize kufunga kutokana na uwezo wa staa huyo katika kipiga pasi za mwisho zitakazowakuna mashabiki wa timu hiyo.

Advertisement