Ole Gunnar atema cheche kinoma kambini Manchester United

Muktasari:

  • Kocha, Solskjaer amemwambia Pogba kwamba asidhani kwamba Man United wanakosa usingizi au kuwa na presha tu kwa sababu yeye anataka kuondoka, wawazii na wala hawana mpango wa kuwaza juu ya jambo hilo, kwa sababu hawana kawaida ya kuuza wachezaji wao nyota.

PERTH, AUSTRALIA. Kumenoga huko Perth, Australia kwenye kambi ya Manchester United. Kocha, Ole Gunner Solskjaer ameripotiwa kwamba anawapeleka mchakamchaka mastaa wake kwa mazoezi makali. Ripoti zinadai kwamba kuna mastaa kibao wanaomba poo kutokana na mazoezi makali ya kocha huyo.

Wakati anachukua kibarua cha kuinoa timu hiyo Desemba mwaka jana kutoka kwa Jose Mourinho, Solskjaer alisema kikosi cha Man United kilikuwa na tatizo la wachezaji wake kutokuwa fiti. Lakini, sasa tizi analowafanyisha wachezaji huko Perth limewatisha watu kwamba kuna hatari ya kuwafanya wachezaji hao waishie kuchoka zaidi kabla ya msimu mpya wa 2019/2o kuanza.

Kumedaiwa pia kuwa na malalamiko kutoka kwa wachezaji wa kigeni kitokana na kocha huyo kufundisha zaidi soka la Kingereza, kwamba mastaa wake wawe fiti zaidi kimwili kuliko kuwa na ujuzi wa kuucheza mpira. Hiyo ndiyo mikwara ya Solskjaer huko kwenye mazoezi ya timu hiyo.

Lakini, nje ya hapo Ole amepiga mikwara mingine. Si unakumbuka Arsenal ilishindwa na tatizo la kujiimarisha kutokana na kuwapiga bei mastaa wake wa maana kwenye kikosini? Iliuza mastaa wake matata kama Samir Nasri, Cesc Fabregas, Alex Hleb, Robin van Persie, Thierry Henry, Patrick Vieira na hata Alexis Sanchez, waliyumba sana. Arsenal ililegea wakati mastaa hao walipotaka kuachana na timu hiyo.

Basi kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi huko Ulaya, Man United imekumbwa na shida hiyo ya wachezaji wake mastaa kutaka kuondoka. Paul Pogba, Romelu Lukaku ni baadhi ya wachezaji hao, huku Marcus Rashford, David De Gea, Alexis Sanchez na wakali wengine kutaka kuelekea mlango wa kutokea huko Old Trafford, lakini Solskjaer amewaambia hivi, Manchester United haiuzi wachezaji wake mastaa.

Kocha, Solskjaer amemwambia Pogba kwamba asidhani kwamba Man United wanakosa usingizi au kuwa na presha tu kwa sababu yeye anataka kuondoka, wawazii na wala hawana mpango wa kuwaza juu ya jambo hilo, kwa sababu hawana kawaida ya kuuza wachezaji wao nyota.

Akimaliza hilo la Pogba, Ole amemwambia mshambuliaji Lukaku, kwamba asahau mpango wa kwenda Inter Milan na badala yake atulize daluga zake Old Trafford kugomea namba msimu ujao. Solskjaer, ambaye alifanya kila aliloweza kuhakikisha Marcus Rashford anasaini dili jipya la kubaki kwenye timu hiyo, alisena amaamini hata De Gea anasaini mkataba mpya wa kubaki kwenye timu kabla ya msimu mpya kuanza.

Kuhusu Sanchez, Ole alisema anamwaaminia mshambuliaji huyo kwamba atakuwa fiti kwa ajili ya kufanya mambo makubwa kwenye timu hiyo msimu ujao, hivyo asifikirie kabisa mambo ya kuondoka kwenye timu hiyo, huku wababe hao wa Old Trafford wakimbakiza pia kiungo wao fundi wa mpira kutoka Hispania, Juan Mata.

"Hatujapokea ofa yoyote ya wachezaji wetu zaidi ya ile ya Paul na kwamba wachezaji wetu wengi wana mikataba mirefu na sisi ni Manchester United, huwa hatuuzi mastaa wetu," alisema.