Okwi anogesha kurudi kwa Mo

Muktasari:

  • Mshambuliaji Okwi alifunga bao moja katika ushindi wa mabao 3-0 waliopata Simba dhidi Stand United ikiwa ni siku mbili tangu kupatikana kwa bilione MO aliyekuwa ametekwa.

KUREJEA kwa mwekezaji mkuu na mwanachama wa klabu ya Simba kumeifufua upya timu hiyo na hilo limejidhihirisha kwenye mchezo wa jana dhidi ya Stand United.

Mabao matatu ambayo moja lilikuwa la kiufundi la kiungo Clatous Chama na lile la Emmanuel Okwi katika kipindi cha kwanza na bao la kujifunga kipindi cha pili yalitosha kuonyesha wazi dhamira na kiu ya Simba kuibuka na ushindi dhidi ya Stand United kwenye Uwanja wa Taifa jana jioni.

Huku ikifahamu fika kuwa ushindi dhidi ya Stand United sio tu ungewapa pointi tatu muhimu bali pia ungemfuta machozi mwekezaji wao Mohammed Dewji ambaye wiki moja iliyopita alitekwa na watu wasiojulikana kabla ya kutelekezwa Viwanja vya Gymkhana, Simba ilionyesha mapema dalili za kusaka ushindi kwenye mchezo huo wa jana kabla hata haujaanza.

Namna benchi la ufundi la Simba lilivyopanga kikosi kilichoanza kwenye mechi ya jana ilitoa ishara kuwa ina kiu sio tu ya kupata ushindi bali pia wa idadi kubwa ya mabao.

Kocha Patrick alianzisha idadi kubwa ya wachezaji ambao kiasili ni washambuliaji kuanzia kwa namba sita ambayo alimpanga Said Ndemla ambaye mara kwa mara hucheza kama kiungo mshambuliaji ambaye mbele yake kulikuwa na Shiza Kichuya, Chama, Emmanuel Okwi, Meddie Kagere na Mohammed Ibrahim.

Kikosi hicho kilionekana kuongeza kitu kwenye eneo la ushambuliaji ambalo lilifanya mashambulizi ya mara kwa mara langoni mwa Stand ambayo yangeweza kuipatia idadi kubwa ya mabao kwenye mchezo huo.

Hata hivyo, kikwazo kwa Simba kilikuwa ni kipa Mohammed Makaka ambaye alifanya kazi ya ziada kuokoa mashuti mengi ya ana kwa ana yaliyoelekezwa langoni mwake hasa na Kichuya, Okwi, Chama na Kagere.

Dakika ya 29 Simba walifunga bao kupitia kwa Kagere lakini mshika kibendera Rashid Zongo kutoka Iringa alilikataa akidai kuwa mfungaji alikuwa ameotea kabla ya kufunga.

Kukataliwa kwa bao hilo hakukuikatisha tamaa Simba ambayo iliendelea kushambulia kama nyuki na kupata bao la kuongoza dakika mbili baadaye kupitia kwa Chama ambaye alitumia uwezo binafsi wa kumtoka beki mmoja wa Stand United upande wa kushoto na kuupiga mpira kwa staili ya kuzungusha ambao ulimshinda kipa Makaka na kujaa wavuni.

Baada ya kufunga bao hilo, Chama alikimbia moja kwa moja hadi kwa kocha wake, Patrick Aussems na kumkumbatia kwa furaha.

Kuingia kwa bao hilo kuliwashtua Stand United ambao waliamua kufanya mabadiliko kwa kumtoa Pastory Juvenile na kumuingiza Chinonso Charles ambayo hata hivyo hayakuweza kuwasaidia kwani katika dakika za nyongeza kabla ya mapumziko, Okwi aliipatia Simba bao la pili akiunganisha vyema pasi ndefu ya Ndemla.

Katika hali iliyotarajiwa mashabiki wa Simba kila timu yao ilipokuwa inafunga bao walishangilia kwa nguvu huku wakitaja jina la Dewji ambaye alipatikana Jumamosi alfajiri baada ya kushikiliwa mateka kwa wiki nzima.

Bao la tatu, beki wa Stand aliyekuwa katika harakati za kuokoa kona lakini beki ukamzidi na kumbabatiza kipa wake, Makaka na kujaa wavuni.

Aussems akomaa

Kama unadhani Kocha wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems ametuliza akili basi utakuwa unajidanganya kwani, jamaa anapanga na kupangua mikakati yake kila kukicha ikiwa ni mkakati wa kusaka tiba na kuhakikisha anatetea ubingwa msimu huu.

Kwa sasa Asseums ametangaza utaratibu mpya kwa wachezaji wake akitaka ufuatwe, ambapo kwa sasa wanakabiliwa na ratiba ngumu ya kula, kufika mazoezini na ukichelewa kwa dakika tano basi mshahara wako unapigwa panga.

Ratiba mpya ambayo amekuja nayo Aussems na ameanza kuitumia jana kwenye mechi dhidi ya Stand United ni kuwa, wachezaji wanaotakiwa kuingia kambini ni wale watakaotumika kwenye mechi husika huku wengine wakiendelea kufanya mazoezi na kurejea majumbani kwao Pia, Aussems amewambia mastaa wake kuwa kuanzia sasa wachezaji ambao wataingia kambini ni 18 au 20 kulingana na mahitaji ya mechi husika huku watafanya mazoezi asubuhi na jioni kuwatazama wenzao uwanjani.

“Huu ni utaratibu tu kama zilivyo taratibu nyingine ndani ya timu, tulianza kuutumia hapo awali lakini wachezaji wanapokuja kuelewa wanajua namaanisha kitu gani,” alisema Aussems.

Beki wa Simba Yusuph Mlipili, alisema huo ni utaratibu ambao Aussems ameuweka ili kila mchezaji aweze kuonesha na kushindana wakiwa mazoezini au kwenye mechi ili kuwepo katika wale 18 au 20 ambao wataingia kambini.

“Sijapata nafasi ya kucheza chini ya Aussems na ni miongoni mwa wachezaji ambao, hatupo kambini kwa kuwa sipo kwenye orodha ya wachezaji ambao, aliwatumia katika mechi ya jana,” alisema Mlipili.