OVYOO: Mourinho alipotumia Pauni 400 milioni kuingia Top Four mara 1 tu Man United

Monday July 8 2019

 

MANCHESTER, ENGLAND, YAMEKUWA maisha magumu sana kwenye Ligi Kuu England kwa kikosi cha Manchester United tangu alipoondoka gwiji Sir Alex Ferguson.

Tangu mara ya mwisho Man United ilipobeba ubingwa wa Ligi Kuu England msimu wa 2013, imefanikiwa kumaliza ndani ya Top Four mara mbili tu. Majanga.

Tangu wakati huo, alichukuliwa Kocha David Moyes akaondoka, akaja Louis van Gaal naye akaondoka bila ya mafanikio yoyote.

Man United ilihamia kwa kocha mwenye mafanikio zaidi, Jose Mourinho na kumpa kazi ya kuinoa timu yao. Mreno huyo alipata sapoti zote, ikiwa ni pamoja na kupewa pesa za kusajili wachezaji aliowataka.

Jambo hilo lilimshuhudia Mourinho akitumia kama Pauni 400 milioni hivi kunasa mastaa 11, lakini bado hakuna mafanikio yoyote kwenye Ligi Kuu England, ambayo timu hiyo ilifanikiwa zaidi ya mara moja tu kumaliza ndani ya Top Four.

Na sasa Mourinho ameondoka akiacha rekodi ya kushinda taji la Europa League na Kombe la Ligi katika kikosi hicho, lakini ameshindwa kutengeneza timu ya ushindi kwenye Ligi Kuu England.

Advertisement

Hawa hapa ndio wachezaji ambao Mourinho alitumia Pauni 400 milioni kuwasajili huko Man United na ameshindwa kufanya kweli kwenye Ligi Kuu England hadi alipofutwa kazi Desemba mwaka jana.

Eric Bailly

Ada: Pauni 30 milioni

Ametoka: Villarrael

Mwaka: 2016

Bailly alionekana kama ni bonge la beki wakati aliponaswa na Man United mwaka 2016. Man United ilikuwa na mpango wa kuboresha safu yake ya ulinzi baada ya kuondoka kwa mabeki wake wa kati Rio Ferdinand na Nemanja Vidic, pacha ilikuwa matata kwelikweli huko Old Trafford.

Lakini Bailly alikwenda kupata shida huko Old Trafford ameshindwa kufikia malengo huku akiandamwa sana na majeraha. Ameletewa pacha wake Victor Lindelof wakipige.

Zlatan Ibrahimovic

Ada: Bure

Ametoka: PSG (Huru)

Mwaka: 2016

Straika, Zlatan Ibrahimovic amekuwa na uwezo wa kufunga mabao katika timu anayokwenda kucheza. Ametamba Uholanzi, Sweden, Italia, Ufaransa na alitamba pia England. Kwenye msimu wa kwanza Ibra alifunga mabao 17 katika mechi 28 za ligi. Licha ya kwamba alikuwa na umri wa miaka 34, Ibra alitamba kwenye kikosi hicho alibeba taji la Europa League, Ngao ya Jamii na Kombe la Ligi kabla ya kuachana na timu hiyo kutimkia zake Marekani.

Henrikh Mkhitaryan

Ada: Pauni 38 milioni

Ametoka: Borussia Dortmund

Mwaka: 2016

Baada ya msimu bora wa 2015/16 ambako alifunga mabao 11 na kuasisti mara 15 katika mechi 31 za Bundesliga, Mkhitaryan alinaswa na wababe wa Old Trafford. Staa huyo wa Armenia alitarajiwa kufanya mambo makubwa kwenye kiungo ya Man United, lakini mambo yamekuwa tofauti baada ya kutua kwenye Ligi Kuu England. Msimu wake wa kwanza alicheza mechi 24 na kufunga mabao manne tu na kuasisti mara moja kabla ya kupelekwa Arsenal akibadilishana na Alexis Sanchez.

Paul Pogba

Ada: Pauni 89 milioni

Ametoka: Juventus

Mwaka: 2016

Kiungo Paul Pogba alinaswa kwa ada iliyoweka rekodi kwenye klabu hiyo ya Old Trafford baada ya kuonyesha kiwango bora huko Juventus. Lakini, baada ya kutua Man United, kiwango cha Pogba kimekuwa cha kupanda na kushuka kama homa za vipindi na hivi sasa anapiga hesabu za kuachana na timu hiyo. Alitibuana na Kocha Mourinho na hivi karibuni amedaiwa kuwa na uhusiano wa hovyo na Solskjaer. Huenda akaondoka Old Trafford mwaka huu.

Victor Lindelof

Ada: Pauni 31 milioni

Ametoka: Benfica

Mwaka: 2017

Lindelof alisajiliwa na Mourinho na kuingia moja kwa moja kwenye kikosi cha Man United msimu ulipoanza. Staa huyo wa Sweden aliishia kucheza mechi 17 na kuanza kukabiliana na maisha magumu kwenye soka la Ligi Kuu England. Msimu wa 2018/19, licha ya kwamba Man United ilimaliza nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi, Lindelof alikuwa sehemu muhimu ya kikosi hicho akicheza mechi 30. Kwa pesa aliyosajiliwa bado hajafanya kile ambacho watu walitaraji angefanya.

Romelu Lukaku

Ada: Pauni 75 milioni

Ametoka: Everton

Mwaka: 2017

Lukaku alikuwa na kiwango bora kabisa huko Everton. Mabeki walipata shida sana kumdhibiti, ndipo Man United ilipokwenda kunasa huduma yake kwa Pauni 75 milioni. Kwenye kikosi cha Everton, alifunga mabao 53 katika mechi 110 alizocheza kwenye ligi. Msimu wake wa kwanza Old Trafford alifunga mabao 16, lakini msimu uliopita alifunga mara 12 tu. Kwa sasa anapiga hesabu za kuondoka baada ya Marcus Rashford kuchukua nafasi yake kwenye kikosi cha kwanza.

Nemanja Matic

Ada: Pauni 40 milioni

Ametoka: Chelsea

Mwaka: 2017

Matic aliondoka Chelsea kwenda kujiunga na Man United kwa dili la Pauni 40 milioni. Jose Mourinho aliamua kumvuta kiungo wake aliyetamba naye huko Stamford Bridge na kuhamishia Old Trafford. Matic amekwenda kuimarisha safu ya kiungo ya Man United na kuonekana kuwa na uhai katika kipindi cha Mourinho na alifanya hivyo chini ya Solskjaer. Bila ya shaka huduma yake itaendelea kuwa muhimu kwenye kikosi hicho kwa msimu ujao.

Alexis Sanchez

Ada: Kubadilishana wachezaji (Pauni 30 milioni)

Ametoka: Arsenal

Mwaka: 2018

Watu walishtuka wakati Sanchez alipoamua kufuata nyayo za Robin van Persie kwa kuihama Arsenal na kwenda kujiunga na Manchester United. Aliondoka Emirates kwa dili la kubadilishana wachezaji lenye thamani ya Pauni 30 milioni, ambapo Henrikh Mkhitaryan aliondoka Old Trafford kwenda kujiunga na Arsenal. Sanchez bado hana alichokifanya cha maana Man United akiteseka chini ya Mourinho na Solskjaer. Msimu ujao ni wa Sanchez kuonyesha ubora wake.

Diogo Dalot

Ada: Pauni 19 milioni

Ametoka: Porto

Mwaka: 2018

Hakuna makubwa yaliyotarajiwa kutoka kwa Dalot wakati alipowasili huko Manchester United. Beki huyo wa kulia ndio kwanza alikuwa amecheza msimu mmoja mzima kwenye kikosi cha FC Porto baada ya kupandishwa kutoka kwenye kikosi cha watoto cha timu hiyo. Alicheza mechi 16 kwenye kikosi cha Man United msimu uliopita na kuna mambo mazuri aliyafanya kuwapa mashabiki wa timu hiyo imani juu yake. Dalot ni uwekezaji wa muda mrefu.

Fred

Ada: Pauni 50 milioni

Ametoka: Shakhtar Donetsk

Mwaka: 2018

Kiungo wa Kibrazili, Fred alikuwa mmoja kati ya wachezaji walionaswa kwa pesa nyingi na Kocha Mourinho, ambaye alitarajiwa kuja kutamba kwenye sehemu ya kiungo na viungo wengine Nemanja Matic na Paul Pogba. Lakini, mambo hayakuwa mambo kwani staa huyo aliishia kucheza mechi 17 tu. Alicheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kwenye hatua ya 16 bora wakati Man United ilipoichapa PSG na kutinga robo fainali. Anatazamiwa kutamba msimu huu.

Lee Grant

Ada: Pauni 1.5 milioni

Ametoka: Stoke City

Mwaka: 2018

Kipa veterani, Lee Grant alicheza mechi moja tu ya Kombe la Ligi kwa msimu wote uliopita. Kipa huyo mwenye umri wa miaka 36 alisajiliwa kwa ajili tu kama makipa wengine, namba moja David De Gea na namba mbili, Sergio Romero mmoja wao atakuwa majeruhi. Grant ataendelea kubaki kwenye kikosi hicho cha Old Trafford hadi sasa wakati kikosi hicho kikiwa chini ya Kocha Ole Gunnar Solskjaer ambaye anatarajiwa kukijenga upya.

Advertisement