Nyoni ana mzuka balaa

Muktasari:

Nyoni amekuwa miongoni mwa wachezaji muhimu katika safu ya ulinzi ya klabu ya Simba

BEKI wa klabu ya Simba, Erasto Nyoni amesema licha ya kupewa mapumziko baada ya ligi kumalizika, ameendelea kujifua na mazoezi kuelekea kuanza kwa Ligi Kuu 2020/21.

Nyoni moja ya mabeki bora katika Ligi Kuu Tanzania Bara, amekuwa na msaada mkubwa kwa timu yake katika mafanikio ya kutwaa mataji matatu iliyoyatwaa msimu uliopita kombe la Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho la Azam (FA), pamoja na Ngao ya jamii.

Nyota huyo aliambia Mwanaspoti kuwa, mbali na kupewa mapumziko hayo ya wiki mbili amehakikisha anayatumia vyema ili kuzidi kujiweka fiti kabla ya kurejea katika majukumu ya pamoja na wenzake.

"Tulipewa wiki mbili za kupumzika, mara baada ya kumaliza mechi yetu ya FA na Namungo, ila wiki hizi nimehakikisha nazitumia vilivyo kujiweka vizuri, siunajua mchezaji huwezi kukaa tu bila mazoezi kwa kuwa mazoezi ni sehemu yetu ya kazi,"

Alisema ana mazoezi yake maalum ambayo anayafanya kwa asubuhi na jioni kama kukimbia na kuruka kamba, ili hata akirejea kambini katika mazoezi na wenzake asijepata shida.

Nyoni alisema, mafanikio ambayo wameyapata msimu uliopita watahakikisha wanapambana ili wayapate na msimu ujao wazidi kuweka rekodi zaidi.

"Uwezo na nia tunayo ya kufanya kama tulivyofanya msimu uliopita cha msingi ni umoja na mshikamano kutoka kwa wanasimba wote hakuna kitakachoshindikana,"

Wakati huo huo Meneja wa kikosi hicho, Patric Rweyemamu aliliambia Mwanaspoti kuwa, kikosi chao huenda kikaanza mazoezi rasmi Jumatatu kwa ajili ya msimu ujao.

Rweyemamu amesema mpaka kesho atajua vizuri ratiba ya kuanza kwa mazoezi ya kikosi hicho kuelekea mchezo wa Ngao ya jamii Agosti 29 dhidi ya Namungo sambamba na Ligi Kuu inayotarajiwa kuanza Septemba 6.