Nyika afichua kilichojiri kabla ya kifo cha Mwalusako

Muktasari:

Nyika aliwahi kufanya kazi na Mwalusako katika timu ya Yanga.

ALIYEWAHI kuwa mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Yanga, Hussein Nyika amesema marehemu Lawrence Mwalusako alikuwa anataka kuongea kitu kabla ya mauti yake lakini alishindwa.
Akizungumza na Mwanaspoti Online leo Jumatatu nyumbani kwa Marehemu Mwalusako, Kimara Kibo, Nyika alisema alipoenda jana kumuangalia alimkuta ameshapata fahamu lakini upande wa kuzungumza ni changamoto.
"Mimi licha ya kwamba nafahamiana na Mwalusako lakini pia ni shemeji yangu, Mwalusako amezaa na dada yangu kwahiyo tulipoenda kumuangalia ni kama vile alitaka kuongea kitu kwa dada lakini alishindwa,".
Nyika amesema wakati wakifanya kazi pamoja yeye akiwa kama mjumbe wa kamati ya usajili Yanga huku Mwalusako akiwa Katibu Mkuu, walikuwa wakifanya kazi vizuri.
"Mwalusako ni mtu ambaye alikuwa anapenda ushauri, na alikuwa anafanya kazi na kila mtu yaani muda wote alikuwa anapenda kujifunza" alisema.
Aliongeza kwa kusema soka la Tanzania limepata pigo hasa upande wa Yanga kwa kumkosa Mwalusako