Nyika: Usajili wa Yondani balaa, ngumi nje nje

KATIKA sehemu mbili za kwanza mdau na kiongozi wa zamani wa Yanga, Hussein Nyika, aliyehudumu katika nyadhifa za Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano na Mjumbe wa Kamati ya Usajili iliyokuwa chini ya Abdallah Bin Kleb na Seif ‘Magari’ Ahmeid, alielezea filamu kamili ilivyokuwa walipowaliza Simba katika usajili wa kiungo Feisal Salum. Endelea...

Tambo za fedha zipo

“Nakumbuka kuna wakati niliwahi kusikika nikisema kwamba tuna fedha na hakuna mchezaji tutakayempoteza. Nakumbuka wakati huo kuna wachezaji wetu muhimu wakati huo walikuwa wamemaliza mikataba mfano Juma Abdul alikuwa amemaliza mkataba, Dante (Andrew Vicent) na Kelvin Yondani naye alikuwa amemaliza. Maswali kutoka kwa wanachama na mashabiki wetu yakawa mfululizo. Kila saa unapokea simu unaambiwa hao ndio mabeki wetu inakuwaje wote wanaondoka? Klabu itakuwaje?

“Hatuwezi kukosa fedha na hata tukakosa mkwara au hata busara ya jinsi ya kuongea na wachezaji wetu. Nikawaita wote nikawaambia natambua mnamaliza mikataba yenu lakini Yanga ni klabu kubwa fedha inayo na wote mtabaki hapa endeleeni kujituma katika timu.

“Kitu kibaya zaidi mikataba yao ilikuwa inamalizika wakati ambao timu iko vitani tunatafuta ubingwa. Kuacha kuzungumza nao ni kama kuwavunja moyo. Ikumbukwe tulikuwa tayari tumeshampoteza Chirwa (Obrey) ambaye mkataba wake naye ulimalizika muda mrefu, sasa kilichofuata tukaanza kuongea na mmoja mmoja. Tukamuita Abdul tukamsainisha, akafuata Dante naye akasaini na wote walisaini bila kupewa hata shilingi moja.”

Vita ya usajili wa Yondani sasa

“Baada ya kumalizana na hao akabaki Yondani na wakati huo kulikuwa na klabu zinajipanga kuhakikisha zinaibomoa Yanga kwa kumchukua huyu beki. Tukasema hapana, huyu naye lazima tumbakishe, wanachama hawatatuelewa.

“Tulipomfuata Yondani akagoma kuongea na sisi akasema mambo yote ya usajili tuongee na kaka yake Sunday. Tukaanza maongezi na kaka yake taratibu haikuwa kazi rahisi.

“Kuna siku kaka yake akatupigia simu akituambia kuna klabu zimekuja na fedha zinataka kumsajili mdogo wake akacheze sasa kama Yanga inataka kumbakisha imalize haraka. Wakati huo Yondani mwenyewe alitupa kipaumbele sisi Yanga kabla ya uamuzi mwingine. Ugumu ukaja, wanaotoa pesa ni walewale tunajuana, sasa inabidi urudi kwa akili kuongea na wenzako kumaliza usajili wa mchezaji.

“Nakumbuka mwishowe sasa inafikia siku ya mwisho ya usajili kiasi ambacho Yondani anakitaka kilikuwa hakuna na usajili umebakisha saa kadhaa tu dirisha kufungwa. Tukaitana na wajumbe wenzangu mapema tukajipanga, tukamuita kijana (Yondani) akasema hawezi kuja asubuhi atakuja usiku. Kweli jioni kama saa 12 jioni akaja sehemu tuliyomuita akiwa na kaka zake wawili.

‘Wakati huo wanakuja walikuwa na akili kwamba kila kitu kipo sawa ni kumalizia tu mazungumzo kwa kuwa kiasi cha fedha ambacho wao wanataka tulijua tutavutana nao kisha kumalizana na wao walikuwa na akili kwamba Yanga ina fedha.”

Kaka yake arusha ngumi

“Tukiwa hapo maisha yalikuwa ni kubishana kisha baadaye kila upande unaomba nafasi kujadiliana kisha tunakutana tena. Wao wanatoka nje sisi tunabaki ofisini. Ilipofika saa mbili usiku tukaitana na kuwaambia kwamba kiasi ambacho walikuwa wanataka hakijatimia kwa kuwa alikuwa anataka fedha zake zote.

“Tukamwambia mpaka muda huo kuna kiasi kama asilimia 70 na nyingine zitakamilika kesho yake. Tukamwambia tunaomba asaini fomu tuwahi kuwahisha usajili kabla ya dirisha halijafungwa hapo ndipo balaa likaanza.

“Kaka yake Sunday kama nisingekuwa mtu wa mazoezi kidogo ingekuwa shida, aliinuka na kurusha ngumi, lakini nikaiona na kumdaka mkono akilalamika kwamba tumempotezea nafasi mdogo wake ya kwenda klabu nyingine kumbe hatuna fedha na akasema mdogo wake hawezi kusaini Yanga.

“Alikuwa sahihi kulalamika kwa kuwa ukiacha uongozi mimi ni shabiki wa Yanga nisingeweza kukubali eti kuwa na majibu rahisi kwamba Yanga haina fedha kisha tumpoteze Yondani. Tukagawana sasa, mimi nikamchukua Yondani, kaka yangu Ndama naye akamchukua kaka yake (Sunday) kila mmoja akaenda kuongea na wake.

“Tukaawacha wenzetu wazee wangu Mzee Mashauri (Lucas), Marehemu Urungo na BinKleb wakibaki ndani kujipanga nao na ndugu zake wengine. Baada ya muda Yondani alikubali tumalizane na kuna wadau wetu mbalimbali huwa hawapendi kutajwa katika vyombo vya habari nao walitusaidia katika mambo mbalimbali katika usajili huo kwa kumpa zawadi Yondani baada ya kukubali kubaki.

“Mwisho wa siku kijana akasaini na baada ya kusaini kaka yake alikuwa muungwana akaomba radhi kwa yaliyotokea. Japo hakikuwa kitendo cha kiungwana tulimsamehe na kumwelewa, alikuwa anatetea haki ya ndugu yake. Nakumbuka ilikuwa kama saa nne usiku, nililazimika kuchukua bodaboda ili niwahishe fomu klabuni tumalizie usajili kabla ya dirisha halijafungwa.

WaliendeshaJE timu?

Katika msimu uliopita Yanga ilikuwa na hali mbaya kifedha. Nyika anaeleza jinsi walivyoweza kuvuka katika kipindi hicho kigumu na kuiacha timu katika nafasi salama. “Kikubwa ni umoja tuliokuwa tumeuweka baina ya viongozi na wachezaji, nakumbuka kila baada ya siku tatu tulikuwa tunakutana na wachezaji na kubadilishana nao mawazo na kuwaeleza hali halisi.

Kilichotusaidia zaidi kuna baadhi ya wachezaji walikuwa mabalozi wazuri wa jinsi maisha mazuri yalivyokuwa hapo nyuma na wao walikuwa wakiyaongea wao kwa wao, hilo pia lilitusaidia, lakini pia uamuzi wa kuwaruhusu wanachama nao kuchangia timu ulisaidia.”

Usikose Mwanaspoti kesho Jumamosi upate simulizi zaidi za kusisimua za Nyika klabuni Yanga.