Nuttal, Morocco watajwa kurithi ukocha AFC Leopards

Muktasari:

Rodolfo Zapata, aliyechukua jukumu la kukinoa kikosi cha AFC Leopards mapema mwezi Juni mwaka huu, alitimuliwa klabuni hapo kufuatia msururu wa matokeo yasiyoridhisha.

Nairobi, Kenya. Kocha wa zamani wa mabingwa mara 17 wa KPL, Gor Mahia, Mskochi Frank Nuttal, pamoja na Mtanzania, kutoka visiwa vya Zanzibar, Hemed ‘Morocco’ Suleiman ni baadhi ya wakufunzi wanaotajwa katika mbio za kurithi mikoba ya Muargentina Rodolfo Zapata aliyetimuliwa katika klabu ya AFC Leopards.

Kwa mujibu wa taarifa za kuaminika zilizoifikia Mwanaspoti ni kuwa, Nuttal ambaye aliipatia KOgalo ubingwa wao wa 15 wa KPL (2015/16), ndiye anayeongoza mbio hizo hii ikiwa ni kutokana na wasifu wake na uzoefu alionao.

Kwa Upande wake, Morocco pamoja na Kocha wa sasa wa kikosi cha U-17 cha timu ya taifa na klabu ya Mathare United, Francis Kimanzi, wanatajwa kama chaguo la pili, endapo juhudi za kumpata Frank Nuttal, ambaye inadaiwa kuanza mazungumzo na Ingwe, zitagonga ukuta.

“Kutokana na mambo yalivyo kwa sasa, usishangae kusikia Nuttal ametua AFC Leopards, viongozi wanamkubali na huenda akatua muda wowote, lakini hilo likishindikana, kuna tetesi kuwa wakubwa wanawamezea mate Kimanzi na Hemed ‘Morocco’ Suleiman,” kilisema chanzo chetu.