Noma sana! Chama kila siku Sh138, 000

Friday December 7 2018

 

By THOBIAS SEBASTIAN

ASIKUAMBIE mtu Simba wapo vizuri kinoma kiuchumi kwa sasa, hasa baada ya bilionea wao, Mohammed MO Dewji kuamua kumwaga mshiko wa maana klabu hayo, lakini sasa unaambiwa kiungo wao, Cletus Chama kila siku analipwa Sh138,000.
Chama aliyesajiliwa kutoka Zambia pamoja na Meddie Kagere na Pascal Wawa wote tangu watu Msimbazi walikuwa wakiishi katika hoteli ya Sea Scape kabla ya Kagere na Wawa kupangishiwa nyumba na kumuacha Mzambia huyo hapo.
Kama hujui ni kwamba Chama aliyetambulishwa na Simba Julai 20 siku kikosi hicho kilipokwea pipa kwenda nchini Uturuki kuweka kambi ya maandalizi ya msimu na aliporejea alifikia Se Scape anakoishi mpaka sasa.
Katika hoteli hiyo chumba kimoja sawa na kile anachoishi Chama kwa siku thamani yake ni Sh 138,000 na mpaka jana Alhamisi alitimiza jumla ya siku 140 akiishi hapo huku uongozi wa Simba ukiendelea kumtafutia nyumba kama ilivyokuwa kina Wawa.
Kwa hesabu za kawaida muda wote ambao Chama amekuwa akiishi katika hoteli hiyo uongozi wa Simba utakuwa umemlipia kiasi cha Sh 19, 320, 000 milioni.
Mbali na mkwanja huo mrefu, pia mabosi wa Simba umekuwa ukitoboka kwa kumlipia Kocha Mkuu wao, Mbelgiji Patrick Aussems anaishi hapo na gharama yake ni ndefu zaidi kuliko ya Chama.
Aussems anaishi hotelini hapo katika apatimenti iliyokuwa ghorofa ya nne yenye kila kitu na gharama yake kwa siku ni Sh 299,000.
Kocha huyo alitambulishwa na uongozi wa Simba Julai 19 siku ambayo alianza kazi ya kukinoa kikosi cha mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara.
Mpaka jana Alhamisi zinakuwa jumla ya siku 139 ambazo ameishi katika hoteli hiyo na maana yake ni kwamba Simba imemlipia kiasi cha Sh 41,561,000 milioni kwa muda wote huo kuonyesha kwa sasa Msimbazi mambo ni yale ya 'mboga saba'.

Advertisement