Niyonzima atajwa Azam, Pluijm ang’aka

Muktasari:

Licha ya taarifa kusambaa kwamba nyota Haruna Niyonzima yupo mbioni kujiunga na Azam, kocha mkuu wa Azam Hans Pluijm amemkaushia.

Dar es Salaam. Kiungo wa Simba, Haruna Niyonzima anatajwa kuwa yuko mbioni kujiunga na kocha wake wa zamani Hans Pluijm katika kikosi cha Azam Fc, baada ya mchezaji huyo kukosa nafasi ya kucheza kwenye kikosi chake cha mabingwa wa Ligi Kuu Bara.

Niyonzima alisajiliwa Simba msimu uliopita akitokea Yanga, hata hivyo ameshindwa kuonyesha makali yake ndani ya kikosi hicho kinachonolewa na kocha Patrick Aussems.

Baada ya taarifa hizo kusambaa, Mwanaspoti lilimtafuta kocha wa Azam, Hans Pluijm ambapo alifunguka kwamba hana mpango wa kufanya usajili katika kipindi hiki.

“Sizani kama nitafanya usajili hivi sasa kwa sababu naona nina kikosi kipana, sio Tshishimbi wala Haruna ambaye anaweza kutua hapa, kama nikiwafanya usajili basi ujue nitaomba bajeti na kuwaambia viongozi wangu lakini liwe jambo la muhimu sana,” alisema.

Niyonzima amebaki nchini baada ya kutoitwa kwa mara ya kwanza katika kikosi cha timu yake ya Taifa Rwanda, licha ya kuichezea timu hiyo kwa muda mrefu akiwa nahodha.