Nina deni kubwa kwa Rais Magufuli -Mwakinyo

Muktasari:

Akizungumza kabla ya kukabidhi fedha hizo,Shigela alisema mbali ya sh. 1.5 milioni zilizotolewa kwa bondia huyo, mkoa wa Tanga umeandaa mabasi mawili aina ya Coaster kwa ajili ya kuwapeleka Dar es salaam na kuwarejesha Tanga mashabiki watakaokwenda kushuhudia pambano hilo la kimataifa.

BONDIA Hassan Mwakinyo leo Jumatano amewaaga rasmi wakazi wa Tanga na kusema kuwa ana deni kubwa kwa Rais John Magufuli na Watanzania.

Mwakinyo amesema atahakikisha analipa deni hilo kwa kumtwanga mpinzani wake, Mphilipino katika pambano lao litakaofanyika keshokutwa Ijumaa uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Alisema hayo jana wakati akikabidhiwa na Mkuu wa mkoa wa Tanga, Martine Shigela sh 1.5 milioni za maandalizi ya mwisho ya pambano hilo litakalofanyika Ijumaa jijini Dar es salaam.

"Nina deni kubwa kwa Rais wangu John Magufuli na watanzania wenzangu ambao wameweka matarajio makubwa kwangu...nitalipa deni hili kwa kumtoa kwa K. O  Mphilipino.

Akizungumza kabla ya kukabidhi fedha hizo,Shigela alisema mbali ya sh. 1.5 milioni zilizotolewa kwa bondia huyo, mkoa wa Tanga umeandaa mabasi mawili aina ya Coaster kwa ajili ya kuwapeleka Dar es salaam na kuwarejesha Tanga mashabiki watakaokwenda kushuhudia pambano hilo la kimataifa.

"Tutatoa mabasi mawili,lakini yeye tunampa gari rasmi la kumpelekea na kumrejesha Tanga hatupendi apate kikwazo cha aina yoyote"alisema Shigela.

Mkuu huyo wa mkoa pia alisema atakaporejea na ushindi bondia huyo na ushindi,atakabidhiwa kiwanja cha kujenga nyumba katika jiji la Tanga.

Meneja wa bondia huyo, Mrisho Zayumba alisema Mwakinyo atasafiri leo jioni kuelekea Jijini Dar es salaam tayari kwa maandalizi ya mwisho ya pambano hilo la kimataifa.