Nguvu ya Simba SC tuione kwa Al Ahly

Muktasari:

Katika mechi za nyumbani kama hii ambayo itachezwa Jumanne huwa wanatengeneza nafasi nyingi za kufunga na hutumia chache ambazo mara baada ya kuona wanaongoza kwa mabao 2-3, wachezaji wa timu hiyo huanza kucheza kawaida kwa kuona wameshamaliza kazi.

WAWAKILISHI wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba itakuwa na kibarua kigumu Jumanne katika mechi ya marudiano dhidi ya Al Ahly ambayo itachezwa hapa nyumbani huku ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa mabao 5-0 katika mechi ya kwanza kule Misri.

Simba ipo Kundi ‘D’ na timu za Al Ahly ambayo ndio vinara wa kundi hilo wakiwa na pointi saba, AS Vita inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi nne, Simba ina pointi tatu na JS Saoura ndiyo inayoburuza mkia ikiwa na pointi mbili.

Kama Simba inataka kufuzu na kutinga hatua inayofuata ya robo fainali, lazima ihakikishe inapata ushindi katika mechi dhidi ya Al Ahly ambayo, nayo kama itashinda mechi hiyo itakuwa imeshafuzu katika hatua inayofuata. Makala haya yanakuletea mambo ambayo Simba inatakiwa kuyafanya ili kuhakikisha inashinda katika uwanja wake wa nyumbani kama malengo yake yalivyo ya kupata pointi tisa katika mechi tatu ambazo zote itacheza Uwanja wa Taifa.

SAFU YA ULINZI

Simba katika mechi tatu ambazo imecheza katika Ligi ya Mabingwa Afrika, moja ya nyumbani ilipata ushindi dhidi ya JS Soura, lakini mbili dhidi ya AS Vita na Al Ahly zote ilipoteza tena kwa kufungwa mabao matano katika kila mechi.

Katika mechi hizo ambazo ilipoteza moja ya sababu iliyochangia ni safu mbovu ya ulinzi ambayo inashindwa kukaba mpaka mwisho na kuzalisha makosa mengi ambayo yaliigharimu na kufungwa idadi kubwa ya mabao katika mechi mbili.

Mabeki wa Simba walikuwa wakishindwa kukaba vizuri na kupitika kwa urahisi, lakini walionesha udhaifu wa kutocheza mipira ya vichwa. Pengine yalitokea haya yote baada ya kukosekana kwa beki Erasto Nyoni ambaye ni majeruhi, lakini kwa soka ambalo lililochezwa na AS Vita ua Al Ahly hata kama angekuwepo labda angepunguza idadi ya mabao lakini kufungwa kulikuwa palepale.

Ili Simba ishinde katika mechi mbili katika uwanja wake wa nyumbani lazima ihakikisha mabeki wake wanapunguza au kutokufanya makosa kama hayo.

UKABAJI TIMU

Safu ya ulinzi ya Simba mbali ya kuonekana kuwa na mapungufu ya kutokukaba hadi hatua ya mwisho na kushindwa kuokoa mipira ya vichwa lakini wachezaji wa timu nzima wamekuwa na shida katika kukaba na mara nyingi ukaba kwa macho.

Wachezaji wa Simba wengi wanaonekana ni mahiri pindi timu inapokuwa na mpira lakini wanapokuwa wakishambuliwa wanashindwa kuwa bora katika kukaba jambo ambalo linawapa uhuru wachezaji wa timu pinzani kushambulia kwa urahisi.

Hatua hii ni kubwa katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwa maana hiyo mechi zake zitakuwa ngumu na ushindani mkali kwa maana hiyo ili kuweza kuwamudu wapinzani, vizuri wachezaji wa Simba wakashirikiana kuanzia kushambulia hadi kukaba.

NAFASI ZA KUFUNGA

Dakika 90, za mechi na Al Ahly, Simba ilikuwa imezidiwa kila kitu lakini katika hatua hii imekuwa ikifanya mambo mawili. Mechi ya ugenini huwa wanatengeneza nafasi chache za kufunga ambazo hushindwa kuzitumia.

Katika mechi za nyumbani kama hii ambayo itachezwa Jumanne huwa wanatengeneza nafasi nyingi za kufunga na hutumia chache ambazo mara baada ya kuona wanaongoza kwa mabao 2-3, wachezaji wa timu hiyo huanza kucheza kawaida kwa kuona wameshamaliza kazi.

Ili Simba isonge mbele lazima icheze kwa umakini na kutumia nafasi nyingi za kufunga na si kukosa nyingi kama alivyofanya John Bocco katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mwadui juzi Alhamisi. Kwani ikishindwa kufanya hivyo, Al Ahly ni timu kubwa ambayo inaweza kufanya lolote na kupindua matokeo katika mchezo huo.

HALI YA HEWA

Katika mechi ya kwanza Simba dhidi ya Al Ahly muda wa mechi ulitakiwa kuwa saa 1:00 usiku lakini wenyeji walibadilisha muda na kuuhamisha hadi saa 3:00 usiku ambapo hali ya hewa ya Misri huongezeka baridi na linakuwa kali sana.

Hueanda hiyo ni miongoni mwa sababu ambazo zilichangia Simba kufungwa mabao mengi katika mechi hiyo ni kutokuzoea mazingira ya hali ya hewa ya Misri. Katika mechi ya hapo nyumbani Simba nayo ina uwezo wa kuweka mechi hata saa 8:00 mchana ili kupata faida ya hali ya hewa na mazingira yatakavyokuwa kwani muda huo hapa Dar es Salaam jua linakuwa kali sana.

Msimu uliopita Simba katika Kombe la Shirikisho Afrika ilitoka suluhu ya kufungana mabao 2-2 na Al Masry katika Uwanja wa Taifa huku ikionekana kucheza soka safi na muda mwingi kutawala mpira na labda kama wangecheza muda wa mchana walikuwa na uwezo wa kupata ushindi.

MASHABIKI UWANJANI

Katika mechi ya kufuzu hatua ya makundi dhidi ya Mbabane Swallows ambapo Simba ilishinda mabao 3-1 katika Uwanja wa Taifa moja ya sababu ambayo ilichangia kupata ushindi huo ni wingi wa mashabiki ambao walijitokeza katika mechi hiyo. Mashabiki wa Simba walikuwa wengi ambao muda mwingi walishangilia mbali ya timu yao kuanza kufungwa bao la kuongozwa. Ili timu hiyo iweze kufanya vizuri tena katika mechi hii wingi wa mashabiki wa timu hiyo utanatakiwa kuongezeka.

Mashabiki wa Simba wanatakiwa kuwa na hamasa ya kutosha kujitokeza uwanjani kwa wingi ili kuishangilia timu yao muda mwingi, wachezaji watapata hamasa ya kupambana na kusaka ushindi.

Lakini hata kama matokeo yatakuwa tofauti na hivyo waendelee kushangilia na kukubaliana na hali halisi na si kuanza kuwazomea wachezaji.

Katika mechi ya Simba dhidi ya Al Ahly kule Misri, mashabiki wa timu hiyo walijitokeza kwa wingi na muda wote walionekana wakipiga shangwe la kuwashangilia.