Neymar ni Blaugrana

Muktasari:

Lakini, mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo ya Nou Camp, Abidal amesisitiza kwamba milango siku zote ipo wazi kwa staa huyo kurudi hasa kama atarudi kwenye ubora wake kutoka sasa hadi Mei mwakani.

BARCELONA, HISPANIA . BOSI kubwa wa Barcelona, Eric Abidal hajafunga milango ya supastaa Neymar kurudi kwenye timu hiyo, akisema uelewa wake wa falsafa za timu zinamfanya Mbrazili huyo kubaki kuwa chaguo lao kwenye orodha ya wachezaji inaowataka.

Blaugrana walitumia sehemu kubwa ya dirisha la usajili lililopita kujaribu kumrudisha Neymar kwenye kikosi chao baada ya kumuuza kwenda Paris Saint-Germain miaka miwili iliyopita kwa ada iliyoweka rekodi ya dunia ya Pauni 200 milioni.

Lakini, mpango haukutimia na Neymar aliendelea kubaki PSG mahali ambako amekuwa na mkosi mkubwa kutokana na kukumbwa na majeruhi ya mara kwa mara. Lakini, mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo ya Nou Camp, Abidal amesisitiza kwamba milango siku zote ipo wazi kwa staa huyo kurudi hasa kama atarudi kwenye ubora wake kutoka sasa hadi Mei mwakani.

Abidal alipoulizwa kuhusu Neymar alisema: “Ni mchezaji mkubwa, anayefahamu vizuri falsafa za Barcelona na anayecheza kwenye kiwango cha juu, siku zote atakuwa kwenye mipango.

“Kuanzia hapo, ndipo tunapoweza kuchukua uamuzi, lakini yote kwa yote yanategemea pesa kwa sababu kuna vitu unaweza kuvimudu na kuna vitu vingine huwezi. Muda utazungumza. Kama ataendelea kucheza kwa kiwango kikubwa kwa sababu msimu bado mrefu, sisemi kwamba atakuwa chaguo la kwanza, lakini ni chaguo linalopewa kipaumbele.”

Neymar alipata mafanikio makubwa kwa muda wake aliokuwa Camp Nou kati ya 2013 na 2017, akishinda jumla ya mataji manane, ikiwamo La Liga mara mbili na Ligi ya Mabingwa Ulaya. Amekuwa nje ya uwanja kwa muda sasa tangu Oktoba akisumbuliwa na maumivu ya paja, lakini PSG wanamini atarudi baada ya mapumziko haya ya mechi za kimataifa, ambapo timu yake itakuwa na kibarua cha kuikabili Lille Novemba 22, kabla ya kufunga safari hadi Santiago Bernabeu kwenda kuwakabili Real Madrid katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya makundi siku nne baadaye.