Neymar bishoo wa kibrazili anayemiliki ndege yake mwenyewe

Tuesday June 11 2019

 

PARIS,UFARANSA.NEYMAR da Silva Santos Junior. Brazameni wa Kibrazili huyu. Wanamwita Neymar Jr au wakati mwingine Neymar tu kavukavu. Alizaliwa katika Mji wa Mogi das Cruzes huko Sao Paulo, Brazil miaka 27 iliyopita.

Neymar anafanya sherehe yake ya siku ya kuzaliwa Februari 5 ya kila mwaka. Mama yake staa huyo wa mpira wa miguu anaitwa Nadine da Silva na baba daye ni Neymar Santos.

Asikwambie mtu na umri huo mdogo wa Neymar, hata miaka 30 hajafika, lakini ni bonge la tajiri. Taarifa zinaripoti Neymar ana kipato cha Dola 123 milioni. Forbes taarifa yao waliyotoa Julai 15, 2018, Neymar walisema ana pato la Dola 90 milioni.

Lakini, tangu wakati huo hadi sasa, karibu mwaka umepita, kipato cha Mbrazili huyo kinadaiwa kufikia Dola 123 milioni.

Jinsi anavyopiga pesa

Msingi mmoja mkubwa wa Neymar kwenye kupata pesa ni soka. Malipo yake ya mishahara yake na dili nyingine za kibiashara. Neymar analipwa mshahara wa Dola 41 milioni kwa mwaka kwa huduma yake anayotoa huko PSG, hiyo ni sawa na Euro 700,000 kwa wiki.

Advertisement

Mwaka 2016, Forbes walitoa taarifa kwamba Neymar anavuna Dola 21 milioni kwa mwaka kupitia dili zake za kibiashara. Wadhamini wanaomfanya Neymar kupiga pesa nyingi hivyo, ni pamoja na Beats Electronics, Gillette, McDonald’s, Nike, Red Bull na Gaga Milano. Neymar anadaiwa makusanyo yake kwa mwaka yanafikia karibuni Dola 70 milioni.

Usafiri na makazi

Ukiwa na pesa unafanya unachokitaka. Neymar anamiliki karibu aina zote za usafiri unaofahamu hapa duniani, huku magari ndiyo usiseme. Staa huyo anamiliki majumba ya thamani kubwa pia huko Brazil, Ufaransa na Barcelona. Jumba lake la huko Rio de Janeiro linaripotiwa kuwa na thamani za Dola 9 milioni. Anamiliki pia jina linalofahamika kama Airbnb huko Beverly Hills, ambalo thamani yake haikuwekwa wazi.

Lakini, staa huyo ana makazi ya kifahari huko Ufaransa na hata Barcelona pia, ambako anatajwa huenda akarudi kuchezea timu ya Barcelona katika dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Kwenye suala la usafiri, Neymar ni balaa. Kwanza anamiliki ndege binafsi aina ya Cessna Citation 680 yenye thamani ya Dola 9.1 milioni.

Neymar anamiliki boti pia, huku ana orodha ndefu ya magari kuanzia Audi R8 Spyder, Porsche Panamera Turbo, Volvo XC 60, Audi R8 GT, Ferrari 458 Spider, Maseratti MC 12 na nyingine kibao.

Familia na mchumba

Neymar ana mtoto mmoja, aliyemzaa katika kipindi cha ujana wake. Staa huyo bado hajaamua kuwa na familia yake binafsi, kwani mwanamke ambaye alizaa naye mtoto, alishapigana naye kibuti zamani tu. Hapo kati alikuwa kwenye penzi la mrembo Bruna Marquezine, kabla ya kupiga chini. Januari mwaka huu aliripotiwa kuwa kwenye penzi motomoto la mrembo Mari Tavares.

Lakini suala la kuwa na mpenzi na kuacha limekuwa kitu cha kawaida kwa mwanasoka huyo ghali duniani, ambaye saini yake iliyowagharimu PSG Euro 222 milioni, rekodi yake bado haijavunjwa hadi sasa.

Advertisement