Neymar akaliwa kooni ishu ya ubakaji

Muktasari:

Amedai kuwa alikuwa tayari kushiriki tendo la ndoa na Neymar, lakini kwa wakati huo hakuwa na kinga hivyo, akamwambia haitawezekana.

Paris, Ufaransa. Wakati ishu ya supastaa wa Juventus na timu ya Taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo ikianza upya kule Marekani, akidaiwa kumbaka mrembo, Neymar naye kanaswa na majanga kama hayo.

Neymar, ambaye anashikilia rekodi ya usajili na kulipwa pesa ndefu barani Ulaya, ametuhumiwa kumbaka msichana pamoja na kumtwanga.

Awali, tuhuma hizo zilianza kama utani vile huku mama wa supastaa huyo wa Brazil anayekipiga PSG ya Ufaransa, Nadine Santos akiponda madai hayo akisema yana lengo la kumchafua mwanaye.

Hata hivyo, mrembo huyo anayedai kubakwa na Neymar, Najila Trindade Mendes de Souza ameibuka kwa mara ya kwanza na kufichua mpango mzima wa tukio hilo ulivyokuwa.

Licha ya kuwa Neymar amekanusha kutenda tukio hilo kwenye hoteli moja jijini Paris, Ufaransa mwezi uliopita, lakini Najila amesisistiza kuwa supastaa huyo alimfanyia ukatili huo huku akifunguka mazito zaidi.

Najila alidai kuwa awali walikuwa wakiwasiliana na Neymar kwa simu na kukubaliana kukutana, ambapo alimtumia tiketi ya ndege na kumchukulia chumba kwenye hoteli moja ya kifahari jijini Paris.

Amedai kuwa alikuwa tayari kushiriki tendo la ndoa na Neymar, lakini kwa wakati huo hakuwa na kinga hivyo, akamwambia haitawezekana.

Akizungumza na kituo kimoja cha luninga, Najila alidai: "Nilikuwa tayari kushiriki naye tendo na nilimuuliza kama amenunua kondomu, akasema hapana. Nikwamweleza wazi kuwa hakuna kitakachofanyika kama hakuna kinga kwani, haitawezekana.

"Hakujibu lolote akanipindua kitandani huku akilazimisha kutaka kufanya uhalifu. Nilimwambia aniache, lakini hakusikia na ndio kwanza alikuwa akinipiga sehemu zangu nyeti. Nilijitahidi kujinasua pale kitandani na kufanikiwa, hicho ndio kimetokea.”

Tayari malalamiko hayo yameripotiwa na kufunguliwa jalada Kituo cha Polisi jijini Sao Paulo, Brazil, Ijumaa iliyopita.

Neymar, ambaye hataiongoza Brazil kwenye michuano ya Copa America inayotarajiwa kufanyika hapo baadaye, baada ya kuumia enka katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Qatar.

Supastaa huyo wa PSG alitolewa nje dakika ya 17 ya mchezo kwenye ushindi wa mabao 2-0.