Ndondo Cup kuibua vipaji zaidi vya soka

Dar es Salaam. Benki ya KCB imepania kuibua vipaji zaidi vya soka kupitia mashindano ya Ndondo Cup, ikufurahishwa na ushindani uliopo Ligi Kuu Bara inayoshirikisha timu 18.

Mkurugenzi Mtendaji wa KCB, Cosmass Kimario alisema wamefurahishwa na ushindani katika mashindano ya Ndondo Cup na kuona wachezaji wengi ambao wanakosa nafasi ya kucheza Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa kutoonekana.

Kimario alisema udhamini wao wa Sh50 milioni ulilenga kufanikisha mashindano hayo, ambayo yana mvuto wa kipekee katika jamii.

“Mashindano ya Ndondo yalikuwa mazuri na mvuto wa hali ya juu, benki yetu imefarijika kuwa sehemu ya jamii kwa kudhamini mashindano hayo na kujionea wachezaji wengi wenye vipaji,” alisema Kimario.

Alisema kuwa kazi kubwa ya sasa ni kuona jinsi gani vipaji hivyo vinajiendeleza na soka kuwa ajira yao kama ilivyo kwa wachezaji wa Ligi Kuu Bara na ligi nyingine duniani.

“Kuna wachezaji wengi Ulaya na Amerika wamepatikana kupitia mashindano madogo madogo ya mitaani, Tanzania ina vipaji vingi sana, lakini kushindwa kuonekana kwa timu kubwa ndiyo changamoto, Benki ya KCB itashirikiana na wadau kuhakikisha kuwa vipaji hivi vinaendelezwa,” aliongeza.

Kimario pia alisema wataendelea kudhamini mpira wa miguu nchini huku akivutiwa na ushindani wa sasa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, ambayo imesimama kutokana na majukumu ya timu ya Taifa (Taifa Stars), ambayo itacheza na Burundi Jumapili kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.