Ndemla asisitizwa kuondoka Simba

WINGA wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe amesema Said Ndemla anapaswa kuondoka ndani ya klabu hiyo kwasababu sio sahemu rafiki kwa kiwango chake.
Ulimboka amesema Ndemla anapaswa kustuka na kuchukua maamuzi  ya kuondoka hata kwa  mkopo mwishoni mwa msimu huu maana amekuwa chini ya makocha tofauti Simba lakini ameishia kukaa benchi.
"Ndemla ana uwezo wa kucheza popote lakini sio Simba tena. Unajua makocha mara nyingi huangalia wachezaji wa kikosi cha kwanza sasa anapopokea timu kutoka kwa kocha aliyepita na yeye hutoa nafasi kwa wale ambao walikuwa wakicheza hiyo ni dhana iliyopo wazi.
"Huaminika kuwa wale ndio wachezaji wenye uwezo zaidi. Ndemla anatakiwa kutambua Simba sio sehemu salama kwake afanye maamuzi, aachane na mambo ya kimaslahi yataua kipaji chake," amesema.
Ulimboka amesema kama Ndemla anaenda Azam au Yanga anaweza kuwa gumzo Ligi Kuu Bara kwa sababu atapata nafasi ya kuchezesha timu na kufunga akiwa mbali.
Upande wake nyota wa zamani wa Yanga, Ally Mayay amesema tatizo la Ndemla lipo kwa watu wanaomuongoza wanashindwa kumshauri vile inavyopaswa.
Nyota huyo wa zamani ya Yanga, amesema,"Kuna kipindi alienda nje kufanya majaribio hata kama mambo hayakwenda vizuri hakupaswa kuwa mwisho alitakiwa kwenda kwingine kutafuta nafasi pengine njia inaweza patikana.
"Ndemla ana uwezo wa kucheza nje kiwango chake sio cha kucheza Ligi Kuu tena lakini akiweka nia ya dhati. Akiendelea kukaa huenda hata timu ya Taifa isinufaike na kipaji alichinacho, " amesema