Ndanda waibeba Yanga kiaina

Muktasari:

Ushindi huo umeifanya Ndanda kupanda kwenye msimamo hadi nafasi ya sita ikifika alama 43, huku Azam ikisaliwa nafasi ya pili na pointi 66 nyuma ya Yanga inayoongoza ikiwa na alama 74 zote zikicheza mechi 32 kila moja.

BAO pekee la dakika ya 62 lililowekwa kimiani na Mohammed Mkopi wa Ndanda, limeizamisha Azam FC kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, mjini Mtwara na kuibeba kiaina Yanga katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara inayoelekea ukingoni.
Ndio, Yanga jana Jumatano walicharazwa bao 1-0 na Mtibwa Sugar mjini Morogoro, hivyo kuwa na presha kubwa kabla ya kuvaana na azam katika mechi yao itakayochezwa Aprili 29 kwani kama Azam ingeshinda Mtwara ingewafanya kupunguza alama kutoka nane hadi tano, lakini Ndanda wakatibua.
Ushindi huo umeifanya Ndanda kupanda kwenye msimamo hadi nafasi ya sita ikifika alama 43, huku Azam ikisaliwa nafasi ya pili na pointi 66 nyuma ya Yanga inayoongoza ikiwa na alama 74 zote zikicheza mechi 32 kila moja.
Kipigo cha Azam kimekuwa faida kwa Yanga kwani Wanalambalamba wameshindwa kupunguza pengo la pointi baina yao na vinara hao na kusaliwa kuwa zilezile nane na kuipa afueni Yanga ambao mechi yao ijayo itakuwa dhidi na Matajiri hao kwenye mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu msimu huu.
Katika mchezo huo uliopigwa jioni hii, Ndanda waliwakimbiza wapinzani wao na kuwabana nyota wa kimataifa Wanalambalamba akiwamo Donald Ngoma kabla ya Mkopi kufunga bao hilo kwa kichwa likiwa la tatu msimu huu akiwa na kikosi hicho. Mkopi alimalizia mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Kiggy Makassy.
Mchezo wa jana ulikuwa ni wa tatu kwa Ndanda kushinda dhidi ya Azam kati ya michezo 10 waliyokutana tangu Wanakuchele walipopanda Ligi Kuu Bara msimu wa 2014-2015.

Cheki rekodi zao hapo chini;
Apr, 18, 2019
Ndanda FC 1-0 Azam FC

Aug 27 , 2018
Azam FC 3-0 Ndanda FC

Feb 03, 2018
Azam FC 3-1 Ndanda FC

Aug  26, 2017
Ndanda FC 0-1 Azam FC

Feb 05, 2017
Azam FC 1-0 Ndanda FC

Sep 24, 2016
Ndanda FC 2-1 Azam FC

Apr 06, 2016
Azam FC 2-2 Ndanda FC

Oct 22, 2015
Ndanda FC 0-1 Azam FC

Machi 16, 2015
Azam FC 1-0 Ndanda FC

Nov 01, 2014
Ndanda 1-0 Azam FC