Napenda Hip Hop ila Soka lipo Damuni

WAHENGA hawakukosea waliposema mtoto wa nyoka ni nyoka, ndivyo ilivyo kwa beki wa Ruvu Shooting, Omary Kindamba na baba yake mzazi.

Anachokifanya nyota huyo uwanjani ni kama anaiga alichokuwa akikifanya baba yake amecheza nafasi hiyo na ndiye alivumbua kipaji chake na kukiendeleza. Mwanaspoti linakufichulia siri hiyo, ili kufahamu mambo mengi kuhusiana na mchezaji huyo, kafunguka mengi hata mambo anayofanya nje ya soka.

SOKA NI URITHI BUANA

Soka ni mchezo ambao umegeuka ajira kwa vijana wengi kwasasa na katika mchezo huo kuna nyota ambao wanacheza kutokana na vipaji walivyonavyo na wengine wanacheza kutokana na kuamini kuwa soka linaweza kuwalipa na kuwabadilishia maisha kwa upande wa beki wa Ihefu, Kindamba anabainisha kuwa mbali na kupenda soka yeye amerithi kutoka kwa mzazi wake.

“Baba yangu alikuwa mchezaji na ni kazi aliyokuwa anaipenda sana, hivyo ili kuendelea kumfurahisha zaidi nikajikuta na mimi najiingiza kwenye soka na kucheza huku nikiamua kufuata kila alichokuwa anakifanya hakuacha kuniunga mkono kwenye hilo alinipa ushirikiano mwanzo mwisho hadi anapoteza uhai wake,” anasema Kindamba.

URITHI WA SOKA

“Ukiachana na kumpa furaha baba yangu kwa kuingia kwenye soka huwezi kuamini nikajikuta na mimi nacheza nafasi kama aliyokuwa anacheza yeye, alikuwa ni beki na mimi kutokana na upendo nilionao kwake na kupenda kumfuraisha nilikomaa kucheza nafasi hiyo,” anasema.

“Hadi hapa nilipofika nimepata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa familia yangu kuanzia mama na baba wote ni wapenda soka hivyo kucheza soka halikuwa tatizo baba alikuwa beki wa kulia na mimi nacheza nafasi hiyo hiyo,” anasema.

BILA MAZOEZI KIPIGO KINAHUSIKA

Wakati wazazi wengine wakipambana kuhakikisha watoto zao wanakomaa na shule na kuhakikisha wanapata elimu bora wakitoka shule wanafanya kazi walizopewa na waalimu kwa wakati basi unaambiwa kwa upande wa wazazi wa beki wa Ihefu anabainisha kuwa asipoenda mazoezini basi wazazi wakewanamtafutia adhabu.

“Wazazi wangu wanapenda sana mpira kwa upande wa changamoto ya kunikataza kucheza sijakumbana nayo kwani kuna wakati hata nikijisikia uvivu wa kwenda uwanjani wananisisitiza ni lazima niende na nafuatiliwa wakibaini sijafika wananichapa,” anasema.

NI KIRAKA

Mbali na urithi wa baba yake kwenye nafasi ya beki wa kulia Kindamba amefunguka kuwa mbali na kucheza nafasi hiyo pia anamudu nafasi zote za beki wa kati huku akiweka wazi kuwa hadi kiungo mkabaji anafiti kucheza.

“Ni beki nakaba hivyo nafasi zote ambazo mchezaji anazuia mashambulizi ya washambuliaji naweza kucheza bila kufanya makosa japo wengi wameshazoea kuobna nacheza nafasi ya beki wa kulia ambayo ndio imenipa jina kutokana na kupangwa sana lakini naweza kufanya maajabu nikipangwa wa kati au kushoto,” anasema.

MIAKA NANE BILA KADI

Anasema ameanza kucheza soka la ushindani mwaka 2012 akiwa na Villa Squad ukiachana na michezo mingine mingi aliyocheza akiwa shule ya msingi na Sekondari anabaibnisha kuwa hadi sasa akiwa amecheza timu tano za Ligi Kuu anamshukuru Mungu ajawahi kuonyeshwa kadi nyekundu.

Kindamba anaweka wazi timu alizocheza kuwa ni pamoja na Panama FC, Dodoma, Villa, African Lyon, JKT Tanzania , Ruvu Shooting na sasa anakipiga Ihefu ambayo amebainisha kuwa ni timu ambayo inaendelea kumuongeza changamoto ya kupambana na anaamini muda wowote anaweza akatoka hapo na kwenda kujaribu sehemu nyingine.

SOKA LIMEMPA KOVU

Pamoja na wadau wengi wa soka kuamini kuwa soka ni mchezo wa burudani na sasa umegeuka kuwa ajira kwa vijana wengi wenye vipaji na wanaoamini katika mchezo huo pamoja na kuwa ajira umekuwa na changamoto zake ambazo zimekuwa zikiwaondoa kabisa mchezoni wachezaji ambazo ni pamoja na majeraha.

Kindamba anaweka wazi kuwa soka limempa mafanikio na bado analidai kutokana na namna alivyowekeza muda wake kwenye kazi hiyo huku akibainisha kuwa pamoja na mapenzi aliyonayo kwenye mchezo huo umempa jeraha ambalo ni la maisha kutokana na kushindwa kufutijka kwenye paji la uso wake.

“Nakumbuka nilikuwa nacheza Villa Squad tulikuwa na mchezo wa ligi dhidi ya Polisi Dar niligongana na mshambuliaji wa timu hiyo simkumbuki kwa jina niliopasuka katika paji langu la uso na jeraha nililolipata liliniweka nje ya uwanja miezi minne tangu hapo hadi sasa sijawahi kukutana tena na tukio lingine ambalo lingeweza kunikatisha tamaa ya kuachana na soka,” anasema.

TUKIO LA KUPASUKA LAMTOA MAMA CHOZI

“Kama nilivyosema mwanzo kuwa wazazi wangu wanapenda soka hivyo mara nyingi nikiwa nacheza walikuwa wanakuja uwanjani kushuhudia nikicheza siku naumizwa na mshambuliaji wa Polisi Dar tukiwa katika harakati za kuwania mpira wa kona mama alikuwepo aliumia sana,” anasema.

NAMBA YA JEZI IMEBEBA MAANA

Wakati wanasoka wengi wakiwa na jezi zenye namba migongoni unaambiwa kila mchezaji anakuwa na maana na namba hizo huku wengine wakivaa kutokana na mapenzi na wachezaji waliowatangulia kwenye soka Kindamba anabainisha kuwa yeye anavaa jezi namba tatu mgongoni kama ishara ya tarehe ya kuzaliwa mama yake mzazi.Anasema anamshukuru Mungu jezi hiyo kila anakoenda amekuwa akikikuta haina mtu hivyo ameitumikia ndani ya misimu nane na anapenda kuendelea kuitumikia ili kumpa faraja mama yake baada ya kutimiza ahadi ya kucheza soka kama baba yake alivyokuwa anataka,” anasema.

NI MJASILIAMALI

“Mbali na soka mimi kwa upande wangu nimewekeza kwenye ufugaji wa kuku nina kuku zaidi ya 230 wa kisasa na wa kienyeji wote ni wa mayai huwa najiingizia kipato kwa kuuza ayai sambamba na kuku wenyewe,” anasema.

NI MWANA HIP HOP

Ukiachana na mapenzi yake kwenye soka beki huyo amefunguka kuwa ni mpenzi wa muziki wa kufoka ‘HipHop’ ambao amekuwa akiuimba mara nyingi anapokuwa mapumziko nje ya kazi yake ya soka.

‘Sijawahi kutusha mashairi wala kuimba wimbo wowote lakini ni mfuatiliaji mkubwa wa kazi hiyo na mara nyingi nikiwa mapumzikoni nyumbani huwa natumia muda mwingi kuimba hizo nyimbo za wasanii mbalimbali kama Chid Benz na wasanii wengine wengi naamini nisingekuwa mchezaji basi ningetumbukia huku,” anasema.

MZUNGOKO WA SITA NJE MWEZI MMOJA

Beki huyo tegemeo kikosini anatarajia kukaa nje ya uwanja wiki nne kutokana na kupata majeraha ya mbavu kwenye mchezo wa Ligi Kuu mzunguko wa sita dhidi ya Biashara United.

“Sitakuwa uwanjani kwa muda wa mwezi kwa mujibu wa daktari nilipata majeraha kwenye mbavu nikiwa uwanjani kwenye majukumu yangu tulikuwa tukicheza mchezo na Biashara siwezi kuelezea tukio lilikuwaje kwani nilichoambiwa ni majibu tu sikumbuki kitu.”