Nani zaidi Team Messi au Team Ronaldo?- 1

Muktasari:

  • Kujua nani zaidi na mengine mengi ungana nasi katika uchambuzi wa Kitabu Messi VS Ronaldo the Greatest Rivalry kilichoandikwa na Luca Caioli. Endelea…

NANI zaidi Messi au Ronaldo? Bila shaka kila shabiki wa soka amewahi kuulizwa, kujiuliza au kushiriki mjadala wa mastaa hao wanaotamba duniani.

Kujua nani zaidi na mengine mengi ungana nasi katika uchambuzi wa Kitabu Messi VS Ronaldo the Greatest Rivalry kilichoandikwa na Luca Caioli. Endelea…

Team Messi au Team Ronaldo? Kuchagua timu moja kati ya wachezaji hao wawili kwa sasa inaonekana kama ni wajibu usioepukika, si jambo rahisi kuamua nani yupo juu ya mwenzake.

Vitaangaliwa zaidi vikombe na idadi ya mechi alizocheza Messi au Ronaldo, pia mapenzi ya kindakindaki na hamasa inayotokana na wachezaji hao wawili ni vitu ambavyo huwezi kuviepuka.

Ni aina ya mjadala unaobebwa na hamasa na mapenzi ya kweli katika soka kuliko takwimu na sababu nyingine za msingi. Kila kitu kidogo kinafanyiwa tathmini na kulinganishwa, yakiwamo matukio mengine madogomadogo zikiwamo ishara, tabia zao za ndani ya uwanja.

Pia, zimo mbinu za kupiga chenga, adhabu, pasi zilizozaa mabao, mabao waliyofunga, idadi ya mechi, ubingwa, zawadi, kauli zao na matukio ya karibu pamoja na utafiti wowote wa karibuni.

CR7 na Messi wamejijengea heshima na kuwa na nafasi yao kama aina nyingine ya derby. Soka linaendeshwa na uwepo wa mahasimu baina ya wanamichezo, timu na nchi pamoja na mlinganio katika kipindi fulani katika historia zao.

Kumbukumbu ni kitu kimoja muhimu katika mchezo na ushindani wa mtu mmoja na mwingine ni tukio la kufurahisha ambalo wakati wote imekuwa sababu ya kuleta mawazo tofauti kwenye vyombo vya habari duniani kote.

Mabondia Ali (Muhammad) na Foreman (Goerge), madereva wa mbio za magari, Prost na Senn, mastaa wa tenisi, Borg na McEnroe, wachezaji wa mpira wa kikapu, Magic Johnson na Larry Bir, madereva wa mashindano ya pikipiki, Valentino Rossi na Marc Marque, wanariadha Carl Lewis na Ben Johnson na wengineo wengi.

Hata hivyo, katika soka ni vigumu kumpata mchezaji anayeweza kutajwa kuwa yuko juu ambaye pia anaweza kuwafunika kabisa wenzake. Kumekuwa na kina Pele, Cruyff, Diego Maradona na Di Stefano hawakuwahi kuvuka katika suala zima la kuwa juu katika zama zao.

Katika hali tofauti kabisa kwa sasa kuna vita ya watu wawili mastaa, vita ambayo imekuwa ya mtu mmoja na mwingine tangu mwanasoka staa wa Ureno (Ronaldo) alipotua katika Ligi Kuu Hispania au La Liga. Na hao ndio wanaotuingiza katika swali linaloulizwa zaidi au mara kwa mara katika soka, nani ni bora kumzidi mwenzake kati ya Ronaldo na Messi?

Ni swali ambalo limekuwa likijirudia mara kwa mara katika magazeti, redio, TV, blogs, na kila mmoja kuanzia, makocha, wanasoka, wachambuzi hadi mashabiki wa sasa na wa zamani wote wamebebwa katika mjadala huu na kila mmoja ana mtazamo wake.

Enzi zake akiwa kocha wa Timu ya Taifa ya England, Fabio Capello alipata kusema: “Ni vigumu kuamua nani bora kumzidi mwingine, wote ni bora lakini katika namna tofauti, Messi hatabiriki hakuna anayeweza kufanya mambo ayafanyayo, lakini Ronaldo ana nguvu na kasi ya ajabu. Lakini alipoulizwa yupi angemchagua katika kikosi chake, Capello alitania, “Cristiano anazungumza Kiingereza, Messi anazungumza soka.

Kocha wa zamani wa Argentina, Sergio ‘El Checho’ Batista anakubaliana na hoja ambayo pia iliwahi kutolewa na jarida moja, “Kwangu mimi Messi ndiye bora lakini wote wako katika orodha ya walio juu.

“Leo ana kipaji cha ajabu, ana kipaji cha kipekee na ana mguu wa kushoto anaomudu kuutumia vizuri kiasi baadhi ya wachezaji wenzake wanamuonea wivu, Cristiano anapiga mashuti vizuri na anakimbia kwa kasi ya aina yake.”

Pep Guardiola kwa upande wake aliamua kuwa wazi zaidi akisisitiza Leo ni mwanasoka bora katika historia.

“Hakutakuwa na mchezaji kama yeye na sidhani kama atatokea mwingine kama Messi,’’ hiyo ndiyo kauli ya Pep, kocha aliyewahi kumuongoza Messi akiwa Barcelona kabla ya kuhamia Bayern Munich na sasa yuko Manchester City ya England.Pia, kuna wale ambao hawataki kujiingiza katika mjadala huu, “Wote ni wachezaji wa kiwango cha juu,’’ anasema kocha wa zamani wa Ureno, Paulo Bento.

“Kama wangekuwa hawachezi katika nchi moja kusingekuwa na mjadala wa nani zaidi ya mwenzake.”

Itaendelea Jumamosi ijayo…