Nani ni Nani UEFA? Kujulikana leo

GENEVA, USWISI. DROO ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya makundi kwa msimu huu wa 2020/21 inatarajiwa kuchezeshwa leo Oktoba Mosi huko Geneva nchini Uswisi saa 12:00 jioni kwa ukanda wa Afrika Mashariki.

Jumla ya timu 32 ndizo zitakazohusika kwenye droo hiyo, zikiwemo nne katoka kwenye kila Ligi za mataifa manne bora zaidi kwa sasa barani Ulaya ambayo ni England, Hispania, Ujerumani na Italia.

Timu hizo 32 ambazo zitakazohusika kwenye droo hiyo huko Geneva ni  Real Madrid, Barcelona, Atlético de Madrid, Sevilla za Hispania, Liverpool, Manchester City, Manchester United na Chelsea za England, Italia, Juventus, Internazionale Milano, Atalanta, Lazio za Italia.

Nne za Ujerumani ni Bayern, Dortmund, RB Leipzig, Borussia Mönchengladbach, tatu kutoka Ufaransa ni Paris Saint-Germain, Marseille na Rennes, kutoka Russia ni Zenit, Lokomotiv Moskva, Krasnodar, mbili kutoka Ukraine ni Shakhtar Donetsk na Dynamo Kyiv.

Kuna klabu moja moja kutoka kwenye Ligi  nyingine za mbalimbali ambazo ushindani wao unaonekana kuwa mdogo kwenye michuano hiyo ambazo ni Porto, Club Brugge, Ajax, Salzburg, Istanbul Basaksehir,  Midtjylland, Olympiacos na Ferencváros.

Droo itachezeshwaje?

Timu 26 zilizojikatia mapema tiketi ya moja kwa moja kuanzia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, zimeungana kwenye hatua hiyo na timu sita ambazo zimetinga hatua hiyo baada ya mechi za mchujo ambazo zimechezwa siku chache zilizopita.

Timu hizo zitagawanywa katika vyungu vinne. Chungu cha kwanza kitahusisha mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na Europa na mabingwa wa msimu uliopita kutoka kwenye Ligi za mataifa sita yenye viwango vya juu vya soka barani humo

Chungu cha pili hadi nne zitawekwa timu kulingana na ukubwa wake. Katika hatua ya makundi ambayo itachezeshwa hakuna klabu ambayo itakutana na timu ambayo wanatoka kwenye ligi moja.