Nani anabisha Manula Tanzania One?

Thursday May 16 2019

 

By Olipa Assa

NADRA sana kukuta beki na kipa wanapewa sifa na mashabiki kama ilivyo kwa viungo na washambuliaji ambao ndio maarufu zaidi Duniani kama Cristiano Ronaldo wa Juventus na Lionel Messi wa Barcelona, lakini pia Mtanzania Mbwana Samatta (KRC. Genk).

Kwa ligi ya hapa nyumbani wanaotikisa zaidi utamsikia Meddie Kagera (Simba), Heritier Makambo (Yanga), Donald Ngoma (Azam FC) na Salimu Aiyee (Mwadui) hao wote kwa sababu nafasi yao ni ya kushambulia, wengine ambao angalau wapo midomoni kwa mashabiki na viungo.

Kuna makipa ambao waliwahi kujiwekea ufalme wao kutokana na uwezo wa hali ya juu uliowalazimisha mashabiki kuwazungumzia kama Juma Pondamali (kocha wa makipa Yanga),Idd Pazi (kocha wa makipa wa zamani wa Simba), Mohamed Mwameja (kipa wa zamani wa Simba), Manyika Peter (Kocha wa makipa wa Taifa Stars) hao ni baadhi tu, lakini wa hivi karibuni yumo Juma Kaseja (KMC).

Manula alitambua wazi kwamba nafasi yake ya ukipa haitazamwi sana na wadau, aliamua kufanya jambo la kipekee ambalo limemtofautisha na wengine mpaka kufikia hatua ya kutazamwa na jicho la umakini na Watanzania.

Kuitwa Tanzania One kwa Aishi Manula, kipa namba moja ndani ya kikosi chake cha Simba pia kuwa tegemeo kwa kocha wa Timu ya Taifa Stars, Emmanuel Amunike, kumethibitishwa na ubora wa kiwango chake na huduma yake kuwa muhimu.

Amecheza ndani ya miaka mitano kwa mfululizo, tangu yupo Azam FC na sasa Simba, hilo limethibitishwa mwenyewe Manula, wakati akifichua siri ya mafanikio yake kuwa ni kujituma.

Mwanaspoti limefanya utafiti juu ya kipa huyo namna ambavyo anatikisa kwa sasa ikiwemo kucheza mechi nyingi, rekodi za tuzo za Ligi Kuu, pia limekusanya maoni ya wadau na matabibu wa afya.

Manula kabla ya kucheza Azam FC kikosi B, aliichezea Mtibwa Sugar timu ya vijana, kisha akajiunga na Wanalambalamba kikosi B mpaka alipopandishwa kucheza Ligi Kuu Bara mwaka 2012.

MSIMU WA MWISHO AKIWA AZAM FC

Kabla ya kutua Simba, msimu wa 2017/18, Manula alikuwa kwenye kiwango cha hali ya juu ambacho kiliwavutia matajiri wa Msimbazi kuhitaji huduma yake iliyowafaa kwani ndiye kipa namba moja tangu ajiunge nao.

Hakuondoka bure Azam FC kwani tayari alishawaachia rekodi mbili ambazo zimeshindwa kuvunjwa na makipa wenzake mpaka sasa.

Manula aliingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania tuzo za mchezaji bora msimu wa 2016/17 kipindi hicho ikiitwa VPL kabla ya Vodacom kujitoa kwenye udhamini, alikuwa amedaka mechi 28 (sawa na dakika 2,520) kati ya 30.

Katika mechi hizo 28, Manula ambaye ni mmoja wa kipa tegemeo wa Timu ya Taifa, Taifa Stars, alifanikiwa kuiongoza Azam FC kutoruhusu wavu wake kuguswa katika mechi 15, akifungwa michezo 13 ikiwa ni rekodi nzuri kuliko kipa mwingine kwa msimu huo.

Kwa msimu huo aliikosa mechi moja dhidi ya Mbao FC, iliyokuwa imepigwa Uwanja wa CCM Kirumba, mzunguko wa kwanza, Manula alidaka mechi 28.

REKODI ZA TUZO

Msimu wa 2015/16 Manula alitwaa tuzo ya kipa bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kipindi hicho ikiitwa VPL kabla haijawa TPL, alikuwa anawania na Beno Kakolanya akiwa na Tanzania Prisons.

Msimu huo alicheza dakika 4628 sawa na wastani wa mechi 51 mechi hizo zilihusishwa na za kirafiki kabla ya kuanza kwa msimu huo.

Katika msimu wa 2016/17 Manula alinyakua tuzo nyingine ya Ligi Kuu Bara, akiidakia Azam FC mechi 28 akiikosa mechi moja ya mzunguko wa kwanza dhidi ya Mbao FC ambayo ilipigwa Uwanja wa CCM Kirumba.

Rekodi hiyo ameiendeleza baada ya kutua Simba, msimu wake wa kwanza msimu wa 2017/18 ambapo Manula alinyakua tuzo ya Ligi Kuu Bara akimtupa nje tena Beno Kakolanya akiwa Yanga, alidaka mechi 28 alikosa mbili tu dhidi ya Kagera Sugar na Majimaji, alizokuwa amemwachia Said Mohamed ‘Nduda’ baada ya timu hiyo kujulikana bingwa.

Mbali na tuzo ambayo aliipata msimu uliopita ya TPL, pia aliibuka kidedea kwenye tuzo ambazo ziliandaliwa na klabu yao zilizokuwa zinajulikana kama ‘Mo Simba Award’, akimshinda Said Mohamed ‘Nduda’ ambaye yupo Ndanda FC.

MSIMU HUU

Bado Manula ameendelea kuwa kipa namba moja ndani ya kikosi cha Simba, ambapo ni mechi chache zilizodakwa na mpinzani wake Deogratius Munishi ‘Dida’ dhidi ya Mbao FC, Simba ikiibuka na ushindi wa mabao 3-0,JKT Tanzania, ikiibuka na ushindi wa bao 1-0, Biashara wakishinda mabao 2-0.

Bado Manula anaonekana ndiye kipa tegemeo ndani ya Simba kwani ndiye alicheza mechi zote za Ligi ya Mabingwa Afrika na pia ndiye panga pangua kwenye kikosi cha Taifa Stars cha Kocha Emmnauel Amunike.

ANAHITAJI NINI

Manula anafunguka kwamba amecheza kwa miaka mitano kwa mfululizo na anaheshimu makipa ambao wanacheza Ligi Kuu Bara, hasa wale ambao amecheza nao timu moja.

“Ubora wa kipaji changu ulianza nikiwa na Azam B kabla ya kupandishwa 2012, aliyekuwa Kocha wa Taifa Stars wakati huo Kim Poulsen, alikuwa ananiunganisha na timu hiyo, kikubwa alikua anaelekeza nijifunze kutoka kwa Juma Kaseja ambaye ndiye alikuwa anaitwa Tanzania one kipindi hicho.

“Baadae nilipoanza kucheza Azam ya wakubwa nikaanza kupata nafasi kwenye Timu ya Taifa Stars, lakini kama kipa namba mbili, niliongeza juhudi ilionifikisha hapa nilipo.

“Kutumika kwa muda mrefu kumeniimarisha kuwa imara zaidi kwenye kupambana ili kuendelea kuwa mfano dhidi ya wengine kwenye ligi yetu, ila wanaonifuatilia wajue nafanya sana mazoezi,” anasema.

NDUDA MBISHI KINOMA

Said Mohamed ‘Nduda’ ndiye alikuwa msaidizi wa Manula msimu wa 2017/18 aliambulia kucheza mechi mbili tu za Ligi Kuu dhidi ya Kagera na Majimaji na tayari Simba ilikuwa haina cha kupoteza kwani ilishakuwa imetawazwa mabingwa.

Anasema hakuzidiwa uwezo wa Manula, akidai alipata bahati ya kuaminiwa kwenye kikosi cha kwanza cha Simba chini ya kocha Patrick Aussems, aliyepokewa timu hiyo kwa Mfaransa Pierre Lechantre.

“Kiwango cha Manula hakijatofautiana na cha kwangu, sema ilikuwa ni wakati wake kuondoka kwangu Simba na kucheza Ndanda FC, hakuna maana kwamba nimeishiwa uwezo ipo siku nitarudi kuichezea Taifa Stars,” anasema.

IDD PAZI AMCHAMBUA

Kocha wa makipa ambaye amewahi kuifundisha Simba, Idd Pazi amemchambua Manula kwamba kadri anavyocheza ndivyo anamuona anazidi kuwa bora, ingawa alienda mbali kwamba anahitaji mshindani kwa madai anaoitwa nao kwenye Timu ya Taifa Stars sio saizi yake.

“Angalau Beno Kakolanya ndiye kipa ambaye nilikuwa namuona anakuja kushindania namba moja na Manula kwenye tTimu ya Taifa ila hao wengine ataendelea kuwaburuza kwani bado hawajafika kwenye kiwango chake.

“Ili mchezaji awe na uzoefu lazima awe anacheza mechi nyingi na sio mladi anacheza awe kwenye kiwango cha juu, hicho ndicho ninachokiona kwa Manula, sioni shida ya yeye kucheza mechi nyingi, hii pia inaonyesha kwamba anajitunza”anasema.

YUKO FITI BALAA

Daktari wa Azam FC, Mwanandi Mwankemwa ameelezea kinaga ubaga juu ya afya za wachezaji kwamba hakuna athari zozote kwa mchezaji anayecheza mechi kwa mfululizo akidai kuwa kama anazingatia vyema mapumziko baada ya mechi.

“Kama mchezaji hajaumia kutokana na kucheza mechi nyingi, kiafya ni jambo zuri zaidi kwani anakuwa anaimalika tofauti na yule ambaye anakuwa hana mazoezi ya kutosha hata kwa hali ya kawaida ndio maana tunasisitiza kwamba kufanya mazoezi ni afya.

“Mfano mzuri Juma Kaseja akiwa kwenye ubora wake aliitwa Tanzania One kwa sababu alikuwa anacheza mechi kwa mfululizo na alikuwa msaada kwa timu yake ndivyo ilivyo na kwa Aishi Manula.

“Kuna wachezaji wengine kama Peter Shilton,Dino Zoff, Buffon, Peter Schimical na wengine wengi wafuatilie kwa umakini utajua kwa nini walikuwa bora.

“Taratibu za mpira wa miguu kila baada ya masaa 48 unaweza kucheza mechi nyingine, kila msimu ligi inapokwisha mchezaji anapaswa kupumzika siku 45 na pia anapaswa kufanya mazoezi ya mbinu, ufundi na ufiti vyote vinampa mchezaji utimamu wa wa mwili” anasema.

Kikosi B cha Azam kilimchukua Manula kutoka timu ya vijana ya Mtibwa Sugar na amekuwa kwenye muendelezo wa kiwango cha ushindani tangu hapo mpaka sasa moto wake haujapoa na unazidi kuwa mkali zaidi.

Advertisement