Nane kutemwa Namungo, Kichuya atajwa

Muktasari:

NAMUNGO FC itaachana na wachezaji wake nane, huku ikiwa na uhakika wa kusajili wengine nane kwaajili ya msimu ujao ambao watashiriki Kombe la Shirikisho Afrika.

NAMUNGO FC itaachana na wachezaji wake nane, huku ikiwa na uhakika wa kusajili wengine nane kwaajili ya msimu ujao ambao watashiriki Kombe la Shirikisho Afrika.

Mwenyekiti wa timu hiyo, Hassan Zidadu alisema wanafanya hivyo kutokana na ripoti ya kocha, Hitimana Thierry aliyoiwasilisha mezani.

“Kwa sasa wachezaji wapo mapumziko na wataanza kuingia kambini tarehe 12 na tarehe 15 wataanza mazoezi, hivyo hakuna kitakachoharibika.

“Tayari tumeanza kusajili kulingana na yale mapungufu ambayo kocha ameeleza kwenye ripoti yake, akisistiza zaidi kuangalia eneo la beki na kiungo ikiwa pamoja na kutafuta kipa,” alisema Zidadu.

Kuhusu Hitimana kubaki ndani ya timu hiyo alisema, mazungumzo yatafanyika baada ya Hitimana kurejea nchini kwa maana amepatwa na msiba wa mdogo wake. “Siku ile ya fainali alifiwa na mdogo wake, tulipomaliza mchezo tuliomba tuongee naye, lakini naye akatuomba itakuwa sio vyema kuanza kulizungumzia jambo hilo wakata kuna msiba, hivyo akasema akirudi tutakaa na ametuhakikishia kubaki hapa.

”Namungo tayari ime-anza kuimarisha kikosi chake baada ya kufanikiwa kuinasa saini ya Fredy Tangalo kwa mkataba wa miaka miwili.

Mchezaji huyo alikuwa akikitumikia kikosi cha Lipuli FC kilichoshuka da-raja na sasa kitashiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao.

Tangalo anayecheza nafasi ya kiungo atafanya kazi sambamba na Lucas Kikoti aliyemaliza msimu akiwa na kiwango bora na kuingia kwenye nafasi ya kuwania kiungo bora wa msimu sambamba Clatous Chama wa Simba.

 “Namungo FC tunayo furaha kubwa kuwataarifu kuwa tumekamilisha usajili wa aliyekuwa kiungo wa Lipuli FC, Fredy Tangalo, kwa mkataba wa miaka miwili,” ilieleza taarifa iliyotolewa na timu hiyo.

Juzi kocha wa timu hiyo, Hitimana alisema kutokana na muda kuwa mfupi wa kufanya usajili asilimia kubwa ya wachezaji watakaopewa nafasi ni wazawa.

Hata hivyo, Hitimana amesema endapo watafanikiwa kumpata mchezaji wa Simba, Shiza Kichuya itawasaidia sababu ana uzoefu na michezo ya kimataifa.