Namungo yaanza na Tangalo

Muktasari:

Tangalo anakuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa na Namungo Fc kwenye dirisha kubwa la usajili kwa ajili ya msimu ujao, akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake Lipuli FC.

Timu ya Namungo tayari imeanza kuimarisha kikosi chake baada ya kufanikiwa kuinasa saini ya Fredy Tangalo kwa mkataba wa miaka miwili.

Mchezaji huyo alikuwa akikitumikia kikosi cha Lipuli FC kilichoshuka daraja na sasa kitashiriki Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao.

Tangalo anayecheza nafasi ya kiungo atafanya kazi sambamba na Lucas Kikoti aliyemaliza msimu akiwa na kiwango bora na kuingia kwenye nafasi ya kuwania kiungo bora wa msimu sambamba Clatous Chama wa Simba.

"Namungo FC tunayo furaha kubwa kuwataarifu kuwa tumekamilisha usajili wa aliyekuwa Kiungo wa Lipuli Fc, Fredy Tangalo, kwa mkataba wa miaka miwili," ilieleza taarifa iliyotolewa na timu hiyo.

Jana kocha wa timu hiyo, Hitimana Thierry alisema kutokana na muda kuwa mfupi wa kufanya usajili asilimia kubwa ya wachezaji watakaopewa nafasi ni wazawa.

"Kusajili wachezaji wa nje inapaswa muda wa kuwatazama na sio kukurupuka, kama nitaendelea kusalia hapa kwa msimu ujao, basi wazawa watapa nafasi kubwa zaidi," alisema Hitimana.