KMC impe imani Mbwana atawabeba

Muktasari:
- Maana kocha Kally aliondoka huku timu hiyo ikiwa imebakiza mechi nne ngumu huku ikiwa haipo katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu maana ilikuwa nafasi ya 11.
WAKATI KMC inaamua kufikia makubaliano ya kuachana na Kocha Kally Ongala, wasiwasi mkubwa ulitanda hapa kijiweni tukifikiria hatima ya timu hiyo.
Maana kocha Kally aliondoka huku timu hiyo ikiwa imebakiza mechi nne ngumu huku ikiwa haipo katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu maana ilikuwa nafasi ya 11.
Maana yake ingefanya vibaya katika mechi hizo nne ilizobakiza katia kipindi inaachana na Ongala hali ingekuwa tete zaidi na ingeangukia kucheza mechi za mchujo za kuwania kubaki Ligi Kuu.
Mechi hizo nne zilizobaki siku Kally alipokuwa anapewa mkono wa kwaheri ni dhidi ya Simba, Tabora United, Mashujaa na Pamba Jiji FC.
Wasiwasi mwingine ukawa ni uteuzi uliofanywa wa kocha wa viungo wa timu hiyo, Adam Mbwana kuwa kaimu kocha mkuu maana hakuwa na uzoefu wowote wa kusimamia benchi la ufundi na mechi za mbele yake zilikuwa ngumu.
Lakini mchezo wake wa kwanza ambao ulikuwa dhidi ya Simba, Mbwana licha ya kupoteza, aliifanya KMC kucheza soka la mbinu na nidhamu ya hali ya juu jambo lililoifanya kuipa presha kubwa Simba kwenye mechi hiyo.
Jamaa mechi ya pili akaiongoza timu hiyo kupata ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Tabora United, matokeo ambayo yameifanya ifikishe pointi 33 na kusogea hadi nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi.
Kijiwe hakijui KMC ina mipango gani ya baadaye kuhusu benchi lao la ufundi lakini kinashauri iamue tu kubaki na kocha Mbwana kama mkuu wa benchi lake la ufundi maana kijana ameonyesha kitu.
Soka la sasa linahitaji makocha vijana hivyo akijitokeza wa kuonyesha kama alivyofanya Mbwana, basi aaminiwe tu.