Nahodha, kocha JKT wapiga hesabu kali Ligi ya Mabingwa Afrika

Muktasari:

 Bingwa wa mashindano hayo atafuzu moja kwa moja kucheza NBL Afrika itakayofanyika baadae mwakani.

Dar es Salaam.Baada ya kutinga raundi ya pili ya Ligi ya Afrika (BAL), nahodha wa JKT, Baraka Athuman na kocha mkuu, Alfred Ngalaliji wameanika mikakati yao katika mashindano hayo.

JKT iko kundi moja na timu za City Oilers ya Uganda, Patriots ya Rwanda na Cobra ya Sudan timu mbili za juu zinafuzu kucheza mashindano ya NBA Afrika yanayasimamiwa na NBA na Fiba.

Timu hiyo pekee ya Tanzania iliyosalia katika mashindano hayo itaanza kambi kesho jijini Dar es Salaam.

Kocha Ngalaliji na nahodha wake Athuman kwa nyakati tofauti wameeleza mipango ya timu kuelekea katika mashindano hayo makubwa.

"Tulibaini udhaifu wa kikosi changu katika mechi za raundi ya kwanza, napaswa kuongeza nguvu kwa kusajili wachezaji wanne watakaosaidiana na hawa waliopo katika mechi za raundi ya pili," alisema kocha Ngalaliji.

Alisema kanuni za mashindano zinawaruhusu kuongeza nguvu, akibainisha wachezaji wengine walibebwa na maumbo makubwa kulinganisha na timu yake.

"Tutasajili watu wa aina hiyo ili twende sawa," alisema kocha huyo ambaye hivi karibuni aliiongoza JKT kutwaa kombe ubingwa taifa (NBL).

Nahodha wa timu hiyo, Athuman alisema kilichowaponza katika mechi za raundi ya kwanza ya BAL ni kuchelewa kufanya mazoezi ya pamoja.

"Tulichelewa kufanya mazoezi ya pamoja, lakini katika kipindi ambacho tumeshiriki mashindano ya raundi ya kwanza timu imekuwa na muunganiko na bila shaka tutafanya vizuri," alisema Baraka anayeshikilia tuzo ya mfungaji bora wa mashindano ya Afrika ya kanda ya tano msimu huu na MVP wa NBL.

Akizungumzia kikosi chake, kocha Ngalaliji amesema wataanza kambi kesho Jumatano kwani lengo ni kuhakikisha wanafuzu na kuiwakilisha nchi kwenye NBA Afrika.

"Nina wafungaji wazuri akiwamo Baraka ambaye licha ya umbo lake dogo, lakini anafanya mambo makubwa uwanjani, katika mechi za raundi ya kwanza wapinzani wetu walitumia maumbo yao kumdhibiti.

"Kila alipokuwa akijaribu kufunga alikuwa akibanwa, kabla ya mechi za raundi ya pili tumepewa nafasi ya kusajili, nitaboresha kikosi kwa kuongeza nguvu, sina shaka tutafanya vizuri," alisema.