Nado amnasa Bocco kiulaini

Sunday July 5 2020

 

By Mwandishi Wetu

MABAO mawili aliyoyatupia mpaka sasa kwenye mchezo wao dhidi ya Singida United, imemfanya winga wa Azam FC, Idd Seleman 'Nado' kufikisha jumla ya mabao saba katika Ligi Kuu Bara na kumnasa nahodha wa Simba, John Bocco katika orodha ya wafungaji.

Nado aliyesajiliwa na Azam msimu huu akitokea Mbeya City, alifunga bao la kwanza dakika ya 2 kabla ya kuongeza jingine dakika ya 15 na kuipa uongozi timu yake ambayo imepanda hadi nafasi ya pili kwa sasa ikiishusha Yanga kwa kufikisha pointi 62.

Yanga iliyolazimishwa suluhu mjini Musoma na Biashara United ina pointi 61, huku timu zote zikiwa zimeshacheza mechi 33, zikichuana kumaliza nyuma ya Simba waliotwaa ubingwa huo mapema na leo walitoka suluhu na Ndanda mjini Mtwara.

Nado hajamnasa Bocco tu kwenye orodha ya wafungaji wenye mabao saba, bali amewafikia nyota wengine sita akiwamo Deo Kanda na Hassan Dilunga 'HD' pia wa Simba.

Wengine wenye mabao hayo ambayo Nado ameyafikia wakatin mchezo wao na Singida iliyoshuka daraja ukiendelea ni Sixtus Sabilo na Marcel Kaheza wote wa Polisi Tanzania na Samson Mbangula anayekipiga Tanzania Prisons.

Kinara wa orodha hiyo bado ni Meddie Kagere wa Simba ambaye licha ya kushuhudia leo akitimiza siku 116 bila kufunga bao tangu alipofanya hivyo mara ya mwisho Machi 11 dhidi ya Singida bado amewaacha mbali wenzake kwani ana mabao 19 mpaka sasa.

Advertisement

Kagere ndiye aliyekuwa kinara wa msimu uliopita wakatui Simba ikitwaa taji lao la pili mfululizo na la 20 tangu mwaka 1965, Ligi ya Bara ilipoasisiwa, akifunga jumla ya mabao 23.

Azam FC hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza anaongoza kwa mabao 4-0 na mawili yakiwekwa wavuni na Nado.

Advertisement