NYUMA YA PAZIA: Kesi za Auba na Pogba mezani kwangu

Sunday June 07 2020
MANE PIC

NIMEKAA katika kiti kama hakimu. Nina kesi mbili mezani. Zinahitaji hukumu. Kila mtu ananitazama. Ukumbi wa mahakama umetulia. Ni mimi ndiye mwenye maamuzi ya mwisho. Usishangae sana ni kesi za soka. Kesi ya kwanza inamuhusu mtu anayeitwa Pierre-Emerick Aubameyang. Kesi ya pili ni ya mtu anayeitwa Paul Pogba. Huyu wa kwanza amebakiza miezi 12 katika mkataba wake na Arsenal.

Huyu wa pili naye mkataba amebakiza miezi 12 pale Old Trafford. Lakini, klabu yake ina kipengele kinachoipa nguvu ya kumuongezea mkataba mwingine wa mwaka mmoja na hivyo, mkataba wake umalizike mwaka 2022.

Tunaanza na kesi ya Auba. Ni kelele kila mahala. Mara leo atakiwe na Real Madrid, kesho auhusishwe na Barcelona, keshokutwa auhusiwe na Manchester United. Ili mradi Arsenal wanakosa usingizi. Kila mmoja katika klabu yao angependa Auba abakie.

Auba ni mtambo wa mabao wa Arsenal, lakini Arsenal ina matatizo mengi ya msingi. Kwa hali ilivyo sasa ni afadhali Auba afunge mabao 15 tu ya msimu, lakini Arsenal iimarike maradufu katika safu ya ulinzi na eneo la kiungo. Ni afadhali Auba afunge mabao 15, lakini Arsenal iwe ngumu kufungika, lakini pia icheze kitimu zaidi mara mbili ya sasa. kwa hali ilivyo sasa mabao ya Auba hayaisaidii sana Arsenal. Msimu uliopita alikuwa mfungaji bora sambamba na mastaa wa Liverpool, Sadio Mane na Mohamed Salah. Hata hivyo, Arsenal hawakuingia Top Four.

Arsenal wana kocha mpya ambaye anawapa matumaini makubwa, Mikel Arteta. Anatazamiwa kuitengeneza Arsenal walau ya nusu ya vile ambavyo bosi wake wa zamani, Pep Guardiola ameisuka Manchester City.

Arsenal waendelee kumbakiza Auba kwa msimu mmoja ujao kama atagoma kusaini mkataba mpya. Inatazamiwa msimu ujao wataimarika zaidi. Mlinzi wao, William Saliba waliyemnunua kutoka Saint-Ettiene msimu uliopita na kisha kumuacha huko kwa mkopo anaonekana kuwa dili halisi.

Advertisement

Kama Pablo Mari akiizoea Ligi Kuu ya England na kisha Saliba akaonyesha kiwango chake moja kwa moja, kuna uwezekano safu ya ulinzi ya Arsenal ikabadilika. Lakini, hapo hapo Arsenal wamekuwa wakihusishwa na walinzi wengine wa kati.

Arsenal pia wanatazamiwa kuingia sokoni katika maeneo mengine. Wakati Arteta alipotakiwa na Arsenal kwa mara ya kwanza mara baada ya kutimuliwa kwa Arsene Wenger alitoa masharti ya kupewa pesa ili akisuke kikosi chake upya.

Mabosi wa Arsenal walikataa masharti yake ya pesa na badala yake wakampa kazi, Unai Emery. Inawezekana Arteta ameishi na ahadi kwamba, atapewe pesa katika dirisha hili. Wote tunafahamu kuwa dirisha la Januari makocha hawapendi kununua mastaa na dirisha linakuwa gumu.

Arsenal wanalazimika kusubiri kuona Arteta akienda katika kambi ya maandalizi ya msimu mpya kwa mara ya kwanza kutekeleza falsafa zake. Kumbuka kwamba hajawahi kupata fursa hiyo kwa sababu aliikuta timu njiani. Huenda akaibadili Arsenal kiuchezaji na kuimarisha nidhamu ya ulinzi. Ni wakati huo ndipo mabao ya Auba yanaweza kuwa na tija zaidi kuliko anayofunga sasa. Kama mabao hayo yataonyesha umuhimu wake huenda hata Auba akabadili mawazo yake na kuamini kuwa yupo katika klabu sahihi.

Kitu cha msingi za kuzingatia kwamba thamani ya Auba sio kubwa sana kwani mkataba wake umebakiza miezi 12, lakini pia dunia ilikumbana na janga la corona na hivyo, klabu nyingi hazina pesa.

Pauni 40 milioni unachoweza kumuuza Auba unaweza kuachana nacho na kisha msimu ujao akifunga mabao mengi huku timu ikiwa imeimarika basi Arsenal wataingiza pesa hiyo Top Four.

Tuhamie kwa Pogba. Ni kesi inayotatanisha kidogo ingawa Manchester United haijabanwa sana kwa sababu wana uwezo wa kuongeza kipengele chao cha mwaka jana. Waliwahi kufanya hivyo kwa David de Gea.

Mkataba wa Pogba unaweza kumalizika mwaka 2022. United ni tofauti na Arsenal. Wameshika mpini katika suala la Pogba. Kitu ambacho wanaweza kufanya kwa sasa ni kuangalia mpaka mwisho wa msimu kama kombinesheni yake na Bruno Fernandes inaweza kukubali.

Achilia mbali hilo, kupitia kwa Fernandes ni wazi United wameshapata mrithi wa Pogba kabla hajaondoka. Ni tofauti na kesi ya Auba pale Arsenal. Ninachoona United wanaweza kumuuza Pogba na kutafuta pacha wa Fernandes.

Ni rahisi kupata kiungo mwingine kuliko straika mwenye uwezo wa Auba. Hawa akina Auba wapo wachache. Lakini, United wanaweza kumuuza Pogba na kumnunua Kai Havertz wa Bayer Leverkusen au Miralem Pjanic kutoka Juventus.

Pogba kuendelea kuwepo United ni tatizo. Anajiona mkubwa kuliko timu na kauli aliyoitoa kule Japan akiwa katika promosheni ya Adidas ilikera. Hakuonekana kuiheshimu United. Yeye na wakala wake, Mino Raiola ni virusi pale United. Haiwezekani kila wiki mchezaji akatoa kauli za kuashiria kuondoka. Hili ni tatizo. Kama Bruno ameshaonyesha kile ambacho anaweza kuwapa United, halafu kama United wanaweza kutumia vema pesa ya mauzo ya Pogba nadhani litakuwa jambo sahihi kuachana na Pogba sasa.

Pogba ni bonge la kiungo. Inawezekana Liverpool hawana Pogba, lakini mbona wana timu bora kuliko United? Pogba hatengenezi timu yenye umoja pale Man United.

Katika hili kesi yake inakwenda tofauti kabisa na Auba, ambaye haongei ovyo kuhusu timu yake na wala hajapeleka mgawanyiko katika timu kiasi kwamba, hata Arsenal wenyewe wanaridhika aendelee kuwa nahodha wao kutokana na kujielewa vizuri.

Advertisement