NEYMAR AMTAKA POGBA HUKO PSG

Muktasari:

Man United jana Jumamosi ilitarajia kumenyana na Newcastle uwanjani Old Trafford kwenye mchezo wa EPL. Pogba hayupo kwenye wakati mzuri huko Man United akitibuana na Kocha Mourinho jambo linaloathiri kikosi kizima na kuishia kupata matokeo mabovu kwenye mechi zake.

NDIYO hivyo. Supastaa, Neymar amefanya mawasiliano na Paul Pogba kuzungumzia uwezekano wa kwenda kuhamia kwenye kikosi cha Paris Saint-Germain wakapige kazi.

Kumekuwa na ripoti staa huyo wa Kibrazili, Neymar amempigia simu Pogba wa Man United mwezi uliopita baada ya Mfaransa huyo kutibuana na kocha wake Jose Mourinho huko Old Trafford.

Pogba hayupo kwenye wakati mzuri huko Man United akitibuana na Kocha Mourinho jambo linaloathiri kikosi kizima na kuishia kupata matokeo mabovu kwenye mechi zake.

Hali ya mambo imekuwa ya ushindani mkubwa na huenda mmoja kati ya wawili hao, Pogba na Mourinho ataachana na maisha ya Old Trafford kama si wote.

Lakini, Neymar anataka kuutumia ugomvi huo kama fursa ya kumshawishi Pogba aende akajiunge na mabingwa hao wa Ufaransa ili wakafanye mambo yao kwenye ligi ya ndani na Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Wachezaji hao wamekuwa marafiki kwa miaka kadhaa sasa na Neymar aliwahi kumshawishi Pogba akajiunge na Barcelona miaka miwili iliyopita wakati alipokuwa huko Nou Camp, lakini Pogba aliamua kurudi zake Man United wakati alipoamua kuihama Juventus.

Lakini, ugumu unakuja sehemu moja tu, Man United hawapo tayari kumpoteza kiungo wao huyo na kama watamuuza basi itakuwa kwa pesa ambayo PSG itakuwa ngumu kulipa kutokana na kubanwa na sheria ya Uefa ya usajili kutokana na kuwa na wachezaji wa bei mbaya kwenye kikosi chao, Neymar na Kylian Mbappe.

Man United jana Jumamosi ilitarajia kumenyana na Newcastle uwanjani Old Trafford kwenye mchezo wa EPL.