N-card, kukomesha ujanja ujanja wa upigaji kwa Mkapa

MFUMO mpya wa kuingia viwanjani wakati mechi zinachezwa umeanza hivi karibuni na mashabiki wanaingia kwa kutumia kadi maalumu ambazo zimesajiliwa kwa namba zao za simu.

Usajili huo unahusisha namba za simu ambazo zimesajili kwa kutumia vitambulisho vya Taifa na kila mtu namba yake wakati wa usajili wa kadi hiyo itapaswa litokee jina lake na sio mtu mwingine.

Mfumo ulianza rasmi wakati wa sherehe za Simba Day na kuendelea tamasha la Azam ‘Azam Festival’, Wiki ya Mwananchi na mechi zote zilizochezwa kwenye viwanja vya Mkapa, Uhuru na Azam Complex uliopo Chamazi.

Katika mahojiano maalumu yaliyofanywa kati ya Mwanaspoti na injinia wa mauzo kutoka Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data kwa Njia ya Mtandao (National Internet Data Centre ‘N-Card’), Geofrey Mlewa(aliyeshika kadi pichani) anaeleza mambo mbalimbali juu ya mfumo huo ikiwemo matumizi ya kadi hiyo.

“Hiki ni kituo cha serikali, namna ya kufanya shughuli za kiserikali za kila siku, serikali ilifanya juhudi kubwa kuwekeza kwenye teknolojia hii kama nchi za wenzetu zilizoendelea.

“Kuna vitengo mbalimbali vya kufanya kazi na ndani ya hivyo kuna Reserch and Development ambayo ndiyo imezaa N-Card.

“Kilianzishwa makusudi kutoa mifumo mbalimbali yenye tija kwa watu mbalimbali, kuna miradi tofauti inayofanywa kwa njia ya mtandao kwa wanaokata tiketi za mabasi, kama kuomba leseni online na taasisi kama Brela, Wizara ya Elimu - Tanzania Bara na Zanzibar upande wa ukusanyaji kodi TRA.

“Dhana kubwa ya N-Card ni kuondoa watu kutembea na pesa mkononi, badala yake wanaweka kwenye kadi,” anaeleza.

VIWANJA VITATU

Mfumo huo umeanza kutumika kwenye viwanja vitatu ambavyo miundombinu inafaa ambavyo ni Uwanja wa Benjamini Mkapa, Uhuru vinavyosimamiwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Azam Complex ulio chini ya Azam FC huko Chamazi, vyote vya jijini Dar es Salaam.

Mlewa anafafanua juu ya kuanza na viwanja hivyo na mipango ijayo: “Ukiangalia hivi viwanja miundombinu yake ni mizuri hivyo ni rahisi mfumo huu kutumika, ingawa hata viwanja vya mikoani hasa vinavyomilikiwa na chama tawala, tutafanya mazungumzo na uongozi wa ngazi ya juu ya chama hicho kuona namna gani mfumo huo utatumika hata huko.

“Huu ni mfumo mzuri hasa katika ukusanyaji wa mapato na wakikubali utawasaidia kwenye mapato, ingawa sasa itachukua muda ili kufanya marekebisho ya miundombinu kuweza kutumia.

“Mapato mengi ya serikali na hata timu husika yanapotea kutokana na ukusanywaji mbovu, ukusanyaji wa kodi ulikuwa na walakini, pesa nyingi kupotea kwenye mageti, zilipotea kwa watu wasiokuwa waaminifu maana zilipita mikononi mwa watu, timu zilikosa mapato.

“Sasa hivi mapato yatakusanywa kwa uhakika na umakini mkubwa, pesa itapatikana kihalali na walengwa watanufaika nayo,” anaeleza Mlewa.

CHANGAMOTO

Mlewa anasema wanakumbana na changamoto kubwa kutoka kwa wadau wa michezo, kwani asilimia kubwa hawana elimu sahihi juu ya kadi hiyo.

“Hii kadi itakuwa na matumizi mengine mbali na kuingia uwanjani, ingawa elimu sahihi ya N-Card haijawafikia kwa kiwango kikubwa watumiaji, wananchi na wapenzi wa mpira.

“Changamoto nyingine ni watu wengi wanachelewa kukata tiketi na hawajazoea kutumia kadi kwa sababu ni kitu kigeni, wananunua kadi na kuweka pesa lakini zinakuwa hazina tiketi ndani. Wakifika getini wanataka kuingia wakati hawajakata tiketi kisa tu ana kadi, hapo panahitajika elimu kubwa ya matumizi ya kadi maana matumizi ya hiyo kadi ya hatua zake ili kupata tiketi.”

HATUA ZA KUPATA TIKETI

Mlewa analeza: “Mtu akisajili kadi inakuwa ni hatua ya kwanza, halafu ataweka pesa kwa wakala ama kupitia mtandao wa simu anaotumia ambayo ni hatua ya pili, ndipo atafanya hatua ya kununua tiketi.

“Kwa wale ambao wana simu janja wanapakua apps ya Ncard Tanzania yenye picha ya twiga, kuna mwongozo ambao upo pale unaopaswa kufuatwa kujisajili ili mtumiaji apate urahisi wa kununua tiketi kwa njia ya mtandao kupitia simu yake ya mkononi.

“Kwa wale ambao hawana simu janja wanapaswa kwenda kwa wakala wetu katika vituo tulivyovitangaza watawasajili na watanunua tiketi kupitia mashine zetu, ndipo wataingia uwanjani.

“Shabiki akiingia geti kubwa akifika ndani atakutana na watu ambao watakuwa na mashine hizo na ataingiza kadi kwenye mashine kujua tiketi iliyokatwa ni ya shilingi ngapi na atamwelekeza sehemu ya kukaa.”

NAMBA MAJINA TOFAUTI

Bosi huyo anasisitiza mtu yeyote anayesajili kadi ni lazima jina liendane na jina litakalotokea baada ya usajili,” anasema.

“Kwanza hairuhusiwi kadi moja kusajiliwa na zaidi ya mtu mmoja, utaratibu wa kusajili ni kila mtu anatumia simu moja iliyosajiliwa na namba ya Nida.

“Ni kosa la jinai mtu kutumia jina la mtu mwingine kusajili kadi ya ncard na hairuhusiwi kisheria kabisa.

“Ili upate kadi lazima uwe umesajili namba ya simu, ni utaratibu wa kisheria, tunategemea atakayesajili kadi atatumia namba yake ya simu, atakayetumia namba ya rafiki yake ni kosa la kisheria.

“Likitokea tatizo lolote atatafutwa yule mwenye jina la kadi yake, hivyo tunatoa rai kwa wananchi wote, kwani tukiingiza linatokea jina la mtu husika, ukisajili Ally na jina lako ni Asha lazima tutakuwa na maswali ya kumuuliza kiusalama, hivyo kila mtu atumie namba yenye jina lake halisi.”

UPANDE WA WATOTO

Kuhusu watoto anasema walikutana na changamoto hiyo wakati wa maandalizi ya mfumo huu. “Hivyo tunaangalia umri na huwezi kumzuia kuingia (mtoto), ila kuna wale wa kidato cha nne tunategemea wana simu zilizosajiliwa hata kama hawazitumii, ila wale wa darasa la saba hao wanaruhusiwa kwa utaratibu unaowekwa.”

MITAMBO KUSUMBUA

Katika tamasha la Simba Day kulitokea tatizo la ukatishaji wa tiketi na baadhi ya mashabiki walilazimika kununua tiketi pasipo kutumia mfumo huu mpya.

“Uongozi wa klabu ndio ulitoa utaratibu huo kuuza tiketi kwa mfumo ule, lengo ni wale wanaokwenda kukaa (uwanja wa) Uhuru endapo (wa) Mkapa ungejaa, viingilio vilikuwa Sh2,000 tu kama ilikuwa ni zaidi hapo, basi ni ujanja wa baadhi ya watu na hatuwezi kulidhibiti maana kuna wengine wananunua tiketi nyingi na kulangua watu,” anasema.

“Kuna watu wanaingia uwanjani na kuwapa kadi wenzao ili waingie, hii sasa ni ngumu kwani mtu mmoja akitumia basi haitasoma tena na itaonyesha kuwa mtu ameingia ikiwemo muda alioingia.

“Kuna watu tumewakamata wanauza kadi feki kwa Sh10,000 ambao ni utapeli mkubwa, hii kadi ina vitu vingi vya tofauti na inauzwa Sh1,000 tu, wengi wanaumizwa kwa sababu wanachelewa kupata huduma wanasubiri siku ya mechi. Mfumo kusumbua ulikuwa unatokana na ule ujanja wa watu kutaka kuingia ila sasa tumedhibiti. Tunakusanya mapato ya serikali, ukinunua kadi feki ni uhujumu unakamatwa uliyenunua na aliyekuuzia.”

VIWANJA VYA MIKOANI

Kuhusu viwanja vya mikoani ambavyo asilimia kubwa vinalimikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), bosi huyo anasema: “Uwanja wa Mkapa, Uhuru vipo chini ya Wizara ya Michezo, mikoani vipo chini ya chama tawala, utaratibu wa utoaji huduma hii unakuwa na changamoto kidogo, tumefikiria kwenda kuzungumza na uongozi wa juu wa chama, kuingia kwenye makubaliano ya maboresho ili mfumo huu uingie.

“Utawasaidia pia kupata mapato, ingawa utachukua muda maana kuna mambo ya matengenezo ya teknolojia - nina maana viwanja hivyo vinajulikana vilivyo mazingira yake.”

MKATABA

Kuhusu suala la mikataba anasema: “Tuna imani kwa sababu malengo ni kuangalia mbele zaidi na tunaamini tutafanya kazi nao kwa muda mrefu. Huu ni mkataba ambao una makubaliano na tukifikia malengo basi tutaangalia inakuwaje, tunaamini kutimiza malengo lipo ndani ya uwezo wetu.”

VITI, MASHABIKI

Kuhusu mpango wa kila shabiki kukata tiketi yenye namba ya kiti chake, Mlewa anasema viti vina namba na mara ya kwanza walikaa na Manispaa ya Temeke waliwapa hoja hiyo ili mtu akikata tiketi ionyeshe anakwenda kukaa kiti namba ngapi. “Sasa changamoto ni pale ambapo watu wanaingia uwanjani kwa kuchelewa na wanakuwa wengi kwa wakati mmoja ni vigumu kuwamudu, ila tutajaribu.”

Viwanja hivyo vitatu vina uwezo wa kuingiza mashabiki kwa idadi tofauti ambapo Mkapa ni 60,000, Uhuru 23,000 na Azam ni 10,000.

“Kila mechi wahusika huwa wanatuambia wanahitaji watu wangapi kwa kila mzunguko, hivyo tunakuwa na watu wetu ambao wanafanyakazi ya kuruhusu watu kwenda kukaa sehemu wanayohusika, hivyo tunalisimamia kwa karibu zaidi,” anasema Mlewa.

OKTOBA 18, 2020

Ni siku ambayo Simba na Yanga zitakutana katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara, mechi ambayo inaingiza mashabiki wengi Mlewa anaelezea kuwa maandalizi yameanza. “Kwanza tutaanza maandalizi ya kukagua mitambo wiki moja kabla ya mechi, maana tunafahamu ukubwa wa mechi hiyo na wingi wa mashabiki wao, lakini kikubwa tunawaomba mashabiki kukata tiketi mapema wasisubiri siku ya mechi.”

WAANDISHI WA HABARI

Mfumo huo pia unawahusu Waandishi wa Habari anaokwenda uwanjani kuandika habari za michezo ambapo Mlewa ameelezea kuwa: “TFF watatupa utaratibu wa namna ambavyo wanatoa vitambulisho kwa waandishi wa habari za mich ezo.”

Imeandikwa na Mwanahiba Richard, Oliver Albert na Thomas Ng’itu