Mzuka kambi ya Yanga balaa

Muktasari:

“Tumepania kushinda mechi ya Simba ili kuweka rekodi nzuri dhidi ya timu hiyo, lakini kujisogeza kwenye tiketi ya kufuzu Afrika, ni mechi muhimu sana,” alisema Eymael ambaye katika mechi mbili dhidi ya Simba msimu huu kabeba pointi nne

KOCHA wa Yanga, Luc Eymael amesisitiza kwamba wachezaji wake wana mzuka wa aina yake na walichopania mbele yao ni kushinda dhidi ya Simba Jumapili ili kuweka rekodi.

Simba na Yanga zinakutana katika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA).

“Tumepania kushinda mechi ya Simba ili kuweka rekodi nzuri dhidi ya timu hiyo, lakini kujisogeza kwenye tiketi ya kufuzu Afrika, ni mechi muhimu sana,” alisema Eymael ambaye katika mechi mbili dhidi ya Simba msimu huu kabeba pointi nne.

“Wenzetu watakuja kwa ajili ya kufuta matokeo ya nyuma, lakini tunataka mwendelezo na wachezaji wangu wamepania hilo.

Eymael amewasisitiza mashabiki na wanachama wao kusahau yaliyopita kwa kiungo mshambuliaji, Bernard Morrison ambaye baada ya kuripoti kambini jana amesema yupo tayari kuitumikia klabu hiyo.

Morrison alisema hayo jana kwa njia ya simu akiwa njiani kuelekea Mwanza na baadaye Kàgera kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Kaitaba dhidi ya Kagera Sugar.

“Nipo vizuri kwa ajili ya mechi za ligi na Kombe la Shirikisho, ndiyo maana nimejiunga na wenzangu, kwa kifupi nimerejea,” alisema Morrison ambaye Mwanaspoti linajua kwamba ishu yake ya mkataba na Yanga imetupwa kapuni mpaka ligi imalizike.

Naye Eymael alisema: “Ishu ya Morrison tuachane nayo kwa sasa, kila kitu kimeshawekwa sawa tuangalie hizi mechi mbili kwanza dhidi ya Kagera na Simba.” Habari za ndani zinasema Yanga wamekubaliana na Morrison wayamalize kwanza kuhusiana na tofauti zao mpaka mechi za wiki hii zipite ambazo ndizo zilizoshikilia uhai wa timu.

Makamu mwenyekiti wa klabu hiyo, Frederick Mwakalebala alisema kuwa wametatua matatizo dhidi ya Morrison baada ya kuomba radhi.

“Tukitoka huku (Kagera) tutapata siku mbili tu kabla ya kucheza na Simba, kutokana na hilo, tumeamua kuua ndege wawili kwa jiwe moja. Hivyo mbali ya kujiandaa na mechi ya Kagera Sugar, pia tutajiandaa na mechi dhidi ya watani wetu,” alisema Mwakalebela.

Alisisitiza kuwa lengo la Yanga ni kumaliza katika nafasi ya pili na kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho.

“Mipango yetu ipo kamili, tunatarajia maombi yetu kutumia. Tunajua kuwa Simba wanataka kulipiza kisasi, sisi tunataka kuendeleza rekodi na kupata nafasi ya kuiwakilisha nchi kimataifa.”