Mzee Haaland analamba midomo taratibu tu

Saturday November 9 2019

Mzee- Haaland -analamba -midomo- taratibu-RB Salzburg-Erling -Haaland-Manchester City-Mwanasport-MwanaspotiSoka-MwanaspotiGazeti-

 

KUNA kijana anatupia mabao pale RB Salzburg kama hana akili nzuri. Anaitwa Erling Haaland. Kwa sisi tunaofuatilia soka la England tangu zamani tunamjua baba yake,. Alf Inge Haaland. Staa wa zamani wa Manchester City.

Kama unamkumbuka vema Mzee Haaland utakumbuka jinsi alivyoingia katika kasheshe na Roy Keane. Wakati huo Mzee Haaland alikuwa anachezea Leeds United. Katika pambano la United dhidi ya Leeds Keane akaumia lakini Haaland hakujua kama Keane ameumia kweli au vinginevyo. Akaenda kumwambia anyanyuke akijua kwamba Keane alikuwa anadanganya.

Keane alikuwa ameumia kweli na akakaa nje msimu mzima. Baadaye Haaland akahamia Man City. Keane aliporudi akaamua kulipiza kisasi katika pambano la watani wa jadi kati ya City na United huku akimchezea rafu mbaya Haaland huku mashabiki wengi wakishangaa. Alipewa kadi nyekundu.

Yote haya yamepita na sasa Haaland ana mwanae huyu hapa Erling ambaye anatupia mabao balaa pale Salzburg. Erling ambaye alizaliwa Leeds wakati baba yake anacheza Leeds United anatakiwa na klabu za Manchester United, Liverpool, Arsenal, Barcelona, Real Madrid, JUventus na nyinginezo.

Juzi mzee wake, Haaland ametoa kauli kwamba mwanae anatamani kucheza Ligi Kuu ya England siku za usoni. Huu ni mwanzo wa kuchangamkia noti. Kuanzia sasa na kuendelea Mzee Haaland atakuwa akitoa kauli nyingi tofauti kwa sababu anajua kwamba mwanae ni dili.

Zaidi ya kwamba mwanae ni dili, mzee Haaland anajua kwamba na yeye lazima ana kiasi chake katika dili za mbele za mwanae. Hii ndio faida ya kuzaa kipaji. Ananikumbusha tu baba yake Neymar, baba yake Ozil, baba yao akina Serana na Venus Williams na wazee wengi duniani ambao walibahatika kupata watoto ambao wana vipaji.

Advertisement

Katika umri wa miaka 19 wa Erling, mzee Haaland namuona akisubiri pesa za kutosha katika kila uhamisho ambao utakuwa unafanyika kwa mwanae. Yeye mwenyewe amecheza mpira kwahiyo anajua dili za mpira zinavyofanyika. Hana papara.

Sio kila mchezaji wa zamani amefanikiwa kupata mtoto ambaye katika umri wa miaka 19 ni lulu Ulaya. Huwa Napata wivu kila ninapokutana na simulizi za akina Haaland. Jinsi wanavyosubiri pesa za watoto.

Advertisement