Mwendwa: safari ya AFCON bado mbichi

Muktasari:

Mara ya mwisho Kenya kupata tiketi ya kufuzu michuano ya Kombe la mataifa ya Afrika, ilikuwa ni mwaka 2003, ikiwa chini ya ukufunzi wa Jacob ‘Ghost’ Mulee, baada ya kuifunga Cape Verde 1-0, mfungaji akiwa ni Deniss Oliech, katika dimba la kimataifa la Moi Kasarani.

Nairobi, Kenya. Wakati joto la mchezo wa leo, kusaka tiketi ya kufuzu michuano ya kombe la Mataifa ya Afrika, 2019 AFCON, likiendelea kushika kasi, Rais  wa shirikisho la Soka nchini (FKF), Nick Mwendwa amewataka wachezaji wa Harambee Stars, kuwa na utulivu kwani safari ya kuelekea Cameroon, bado mbichi.
Baada ya kulazimisha sare ya 0-0, dhidi ya Ethiopia katika mchezo wa kwanza uliopigwa Bahir Dar, Jijini Addis Ababa, katikati mwa juma lililopita, Harambee Stars, itashuka dimbani, Moi Kasarani, Jijini Nairobi, kuanzia saa 10 alasiri, kurudiana na Wahabeshi hao, ambao wameapa kutoa dozi.
Kenya iko katika nafasi nzuri ya kufuzu michuano hiyo kwa mara ya kwanza baada ya kuikosa kwa zaidi ya miaka 14, ambapo wanahitaji kuifunga Ethiopia leo ili kujiweka pazuri zaidi, lakini Mwendwa, anasema bado kuna kazi kwa hiyo, wakenya hawapaswi kuanza kushangilia mapema.
Akizungumza na wanahabari jana jioni, Mwendwa alisema kuwa kinachotakiwa sasa hivi ni utulivu na umakini, kwa wachezaji na mashabiki kwani bado tuna mlima mkubwa wa kupanda ikizingatiwa bado hatujarudiana na Ghana ambao wana machungu ya kufungwa 1-0, ugani Kasarani.
Kitendawili kikubwa  na ambacho kinaonekana kuwa ni kikwazo mbele ya Kenya kuelekea Cameroon ni kitendo cha Sierra Leone, kufungiwa na CAF pamoja na FIFA, kwa kile kilichodaiwa kuwa ni serikali kuingilia maswala ya soka, kinyume cha sheria za soka.
Kama Sierra Leone, itafanikiwa katika rufaa yao, watarudishwa kundini na hapo ndipo matatizo yatakapoanzia hata kama tutafanikiwa kuifunga Ethiopia baadae leo. Hii inatokana na ukweli kwamba kuifunga Ghana nyumbani kwao ni ngumu, huku pia mchezo wao dhidi ya Sierra Leone, ukionekana kuwa mteremko endapo, Sierra Leone wataruhusiwa kucheza.
"Mchezo wa Jumapili (leo) ni mgumu sana. tunahitaji kushinda. Kama tutashinda, ni lazima tuanze kusali ili Sierra Leone wasifanikiwe katika rufaa yao, maana wakirudishwa kundini tutakuwa na mlima mkubwa sio kidogo. Kwa sasa tuwe watulivu kwanza,” alisema Mwendwa.