Mwanzo, mwisho wa ndoa ya Samatta Dar

Muktasari:

Mwanaspoti halikuwa nyuma kufuatilia tukio hilo mwanzo mpaka mwisho na linakuletea matukio mbalimbali yaliyojiri katika usiku wa wawili hao.

Alichokifanya Mbwana Samatta, kufunga ndoa na mpenzi wake wa muda mrefu, Naima Mgange si kigeni. Hilo lilifanywa na staa wa FC Barcelona, Lionel Messi miaka mitatu iliyopita.

Messi alivunja ukimya Juni 30, 2017 ambapo aliamua kumuoa Antonella Roccuzzo, ambaye alikuwa katika dimbwi zito la mahusiano naye angali akiwa mdogo, nchini kwao Argentina.

Kama vile ambavyo Messi na Antonella walivyoungana huko Rosario, Argentina, ndivyo Samatta naye alikutana na Naima, Mbagala katika jiji la kibiashara la Dar es Salaam.

Kwenda kwa Messi nchini Hispania ambako ulikuwa mwanzo wa soka lake haukuwa mwisho wa mahusiano na Antonella, ndivyo ilivyokuwa pia kwa Samatta ambaye baada ya kuwika Simba alienda TP Mazembe ya DR Congo na kisha kutua zake Ulaya kwenye klabu ya KRC Genk iliyopo Ubelgiji.

Katika kipindi cha mapumziko, Messi alikuwa akiponda raha na mrembo huyo ambaye amepata naye watoto watutu ambao ni Thiago, Ciro na Mateo. Kupenda kwa Samatta maisha yake binafsi kuwa siri ni wachache ambao wanaweza kujua kuwa ana watoto wawili na Naima ambaye amefunga naye ndoa, juzi usiku.

12

Mwanaspoti halikuwa nyuma kufuatilia tukio hilo mwanzo mpaka mwisho na linakuletea matukio mbalimbali yaliyojiri katika usiku wa wawili hao.

NDOA KIMYAKIMYA

Kwa ukubwa wa jina la Samatta ndani na nje ya nchi tukio hilo lingehudhuriwa na viongozi wa Serikali na mastaa mbalimbali, lakini hakutaka makubwa na kuamua kufunga ndoa yake kimyakimya.

Samatta aliamua kufunga ndoa usiku, siku ya Alhamisi nyumbani kwa wazazi wake na Naima huko Mtongani Kijichi. Hta hivyo, alijikuta lengo lake la kufanya tukio kimyakimya likifeli baada ya nyoni ya watu kujaa.

MSAFARA ULIVYOKUWA

Msafara wa Samatta kwenda kufunga ndoa Mtongani maeneo ya Kichangani ulianzia nyumbani kwake Kijichi, ambapo aliongozana na baba mzazi, kaka zake, ndugu wa karibu pamoja na marafiki.

Pamoja na kwamba ndoa yake ilikuwa ya kimyakimya, msafara wa magari ya watu ambao walimsindikiza kwa vyovyote ilikuwa rahisi kufahamu kwamba kuna jambo linakwenda kufanyika mahali.

Kaka waliyefuatana Mohamed, mchezaji wa KMC alikuwa miongoni mwa ndugu ambao walishuhudia ndoa ya mdogo wake, ambapo sura yake ilionyesha bashasha muda wote.

NYOMI YA WATU

Jambo la heri halijifichi buana! Licha ya Samatta kutohitaji makubwa kwenye tukio la kufunga ndoa yake, kaswida na magari ya kifahari yaliyokuwa yamepaki nje ya nyumba ya wazazi wa mkewe, Naima yaliwashitua wakazi wa Kichangani ambao walianza kujisogeza taratibu karibu na eneo hilo.

Walianza kufika wachache ili kujua ni nini kinaendelea kwenye nyumba hiyo, na ilipogundulika Samatta anafunga ndoa na Naima watu waliitana na kujaza eneo hilo.

Shughuli za baadhi ya wakazi wa Kichangani zilisimama ikiwamo magenge yaliyopo karibu kufungwa na maduka huku waendesha bajaji wakizipaki ili kushuhudia tukio hilo.

Licha ya kwamba ndoa ilikuwa inafungwa ndani watu hawakuchoka kusubiri mpaka dakika ya mwisho wakimngoja Samatta atoke nje.

HAWAKUWA NA MUDA NA CHAKULA

Imezoeleka kuona shughuli za mtaani watu kupapatikia chakula, lakini haikuwa hivyo kwenye ndoa ya Samatta na Naima kwani nyomi iliyofika ilikaribishwa chakula, lakini ikaonekana kutokuwa na muda na jambo hilo, badala yake kelele zilisikika kutaka kumuona Samatta.

“Hatujaja kwa ajili ya kula, tunataka kumuona Samatta, hatuamini staa wetu tuliyekuwa tunamuona anacheza Ligi ya Mabingwa anaoa dada yetu, ni jambo la heri na ametuheshimu,” alisikika mmoja wa watu waliofika kushuhudia tukio hilo.

MASTAA WATIA TIMU

Ingawa Samatta alionekana kuwa na jamaa zake wengi kwa harakaharaka Mwanaspoti liliwaona mastaa wa soka wawili; Himid Mao na Thomas Ulimwengu ambao walikuwa mstari wa mbele kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa.

Ulimwengu na Mao walikuwa mstari wa mbele kuhakikisha kila kitu kinafanyika kwa umakini mkubwa.

HIMID AFUNIKA

Mao anayecheza soka la kulipwa nchini Misri katika klabu ya ENPPI, ndiye jina lake lilitajwa zaidi na watu hao kwamba, ni kati ya wachezaji wenye nidhamu ya hali ya juu na atafika mbali zaidi.

“Samatta amefanya jambo la maana kwenye ndoa yake kuchukua wachezaji wenye nidhamu kama Mao, anajua kusalimia watu, hajisikii, kiukweli ni kijana mstaarabu na ndio maana ndoa yake inadumu,” alisema shuhuda ambaye alikuwepo eneo hilo.

URAFIKI WAKE NA ULIMWENGU

Urafiki wa Samatta na Ulimwengu haukuanza jana wala leo, tangu wanacheza TP Mazembe wamekuwa karibu na hata wakija kuichezea timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ ni watu ambao hawaachani.

Ulimwengu alishuhudia ndoa ya rafiki yake kipenzi na alikuwa mstari wa mbele kwa kila jambo.

ATOKEA MLANGO WA UANI

Baada ya tukio la kufunga ndoa kumalizika na nyimbo za kaswida kuacha kupigwa, watu walijiandaa kumlaki Samatta, lakini baadaye walitoka vijana wengi na watu wake wa karibu.

Hata hivyo, bado watu walijipa moyo, akaja akatolewa mkewe Naima ambaye alifunikwa nguo nyeupe ili asionekane na Ulimwengu alikuwa ameishikilia nguo hiyo kwa nyuma.

Lakini buana mambo hayakuishia hapo, kwani kuna wajanja ambao walikwenda kukaa mlango wa nyuma, uani, baada ya kushitukia jambo kwamba Samatta asingetokea pale ambapo walikuwa wanamsubiria. Ilichukua takriban dakika 20 Samatta kutokea mlango wa uani, hapo tayari baadhi ya magari ya marafiki zake yalikuwa yameondoka eneo hilo na lile ambalo alipakiwa bibi harusi.

Baada ya muda watu walionekana wakikimbiza gari la Samatta ambalo alipanda kwa shangwe wakimtaka ashuke angalau awasalimie na kumpongeza kwa ustaarabu wa kufunga ndoa bila makuu.

VIKAO VILIANZA MUDA TU

Mwanaspoti halikuwa nyuma kujua undani wa jambo hilo kufanyika kwa kushitukiza jamii, kwani ukweli ni kwamba ndugu wa karibu wa mwanamke walisema walianza kufanya vikao vya ndoa hiyo muda mrefu.

Licha ya kutoweka majina yao wazi, mmoja alisikika akisema, “vikao vilianza kufanyika muda mrefu sana, Samatta hapendi mambo ya kujionyesha, ndio maana hakutaka kufanya iwe kubwa, anaamini hilo ni jambo la heri analotakiwa kujua Mungu wake.”

Mmoja wa kaka zake na Naima,alisema sherehe hiyo ni sawa na trela katika filamu, kwani sherehe mbili zinakuja kwa upande wao na wa Samatta. “Alitaka ndoa ifungwe kimyakimya, ila itafanyika sherehe kubwa sana, kwetu na kwa mwanaume,” alisema kaka huyo bila kutaja jina lake.

“Hakuna mtu asiyependa jambo la heri, tunajisikia faraja mdogo wetu Naima kutupa heshima kubwa hii, Samatta ana jina kubwa lakini ni kijana mwenye hekima na anajishusha.”

BABA ATOBOA SIRI

Kama ulikuwa hujui uhusiano wa Samatta na mkewe Naima haukuanza hivi karibuni, wamekuwa wote kwa muda mrefu na baba mzazi wa supastaa huyo, Ally Pazi Samatta anasema mwanawe ilikuwa aoe muda mrefu tangu alipojiunga na TP Mazembe akitokea Simba, lakini alizuia jambo hilo akitaka acheze mpira kwanza. “Najua uhusiano wa Samatta na Naima upo muda mrefu, takribani miaka sita sasa, alitaka kuoa mapema nililizua jambo hilo,” anasema mzazi huyo.

“Kwanza umri wake ulikuwa haujakomaa, sababu ya pili ilikuwa ndio anaingia kwenye mafanikio ya soka, asingeweza kushika mambo mawili yakaenda kwa wakati mmoja, nilikataa na akanisikia.

“Nimeona umri wake umekomaa ndio maana nimemwambia aoe na amenitii kaoa, sikutaka kila mtu ajue kwa sababu ndoa yake napenda imhusishe Mungu zaidi kuliko kitu chochote.”

ATOA CHOZI LA FURAHA

Baada ya kuona gari la mwanawe linakimbiliwa na nyomi ya watu huku wakiimba

“Samatta, Samatta”, mzee huyo alibubujikwa na machozi akimsindikiza kwa macho huku akitamka maneno “Mungu aendelee kumfungulia milango zaidi”.

Lakini baadaye alisema, “nalia kwa furaha, hili ni jambo ambalo nilitamani nilishuhudie kwenye maisha yangu, nilitaka kumuona mwanangu akitabasamu kutoka moyoni anapopata mwenza wa siri za maisha yake.

“Ndio maana nimesema hii ni shughuli yangu, nilitaka niozeshe mwanangu mimi mwenyewe huku nikimtamkia maneno ya baraka, namshukuru sana Mungu, Samatta ni msikivu.”

Kisha, mzee huyo alisema, “(Samatta) amefuata maadili ya dini yetu ya Kiislamu. pia amewaheshimu kaka zake waliomtangulia nao wamefunga ndoa, hii siku sitaisahau katika maisha yangu.

“Ameniletea wajukuu wawili, Karimu wa kiume na wa kike (hakumtaja jina) ambaye ni mdogo zaidi, hii ni baraka kwangu, nampa baraka zote, sikutaka afanyie sehemu kubwa hapana (akimaanisha ukumbi mkubwa), nimependa aishi maisha ya kawaida.”

ANASUBIRI KUMPA MAFUNZO YA NDOA

Pamoja na mzee huyo kufurahia mwanawe kufunga ndoa, pia anasema amemtengea muda maalumu wa kumfundisha namna ya kuishi maisha mapya na mkewe.

“Bado ni kijana ambaye anatakiwa kufundishwa maisha ya ndoa yalivyo, hajui, nitakaa naye, nitamuelekeza kila kitu ili ajue mke anatakiwa kuchukuliwaje,” alisema.

“Ninachokipenda kwake pamoja na jina lake kuwa kubwa, ana heshima, anapenda kujifunza na kusikiliza ukimwambia jambo, nitakachokuwa namfundisha hatakipuuza kwani nilikuwa staa kama yeye miaka ya nyumba.

“Nimecheza Simba na Stars kwa namna anayovaa, nimechukua tuzo ya Afrika kwa miaka hiyo, hivyo hakuna geni nisilolijua kwenye ustaa, ndio maana huwezi kumuona anajikweza kwani hakuna kigeni kwake.”