Ukweli ndivyo ulivyo: Kiuhalisi tu Yanga hesabu zimekataa

Muktasari:

Hata kiakili wachezaji walikuwa wakitulia na kucheza kwa ari kubwa na kujiamini, ndio maana walikuwa wakipata matokeo mazuri nyumbani kwa asilimia kubwa

UKWELI ndio huu. Inahitaji roho ngumu kuamini kuwa, Yanga inaweza kutinga makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mbele ya Pyramids ya Misri usiku wa leo Jumapili.
Kwa soka la kisasa inawezekana kabisa Yanga wakaifunga na hata kuing’oa Pyramids ikiwa mjini Cairo. Inawezekana kwa sababu soka ni mchezo wa kikatili sana. Hata hivyo, kwa rekodi za Vijana wa Jangwani kwenye viwanja vya Afrika Kaskazini na kuteleza kwa hesabu zao kwa mchezo wao wa awali nyumbani, ndio tatizo.
Huko nyuma kulikuwa na nadharia moja katika soka, kwamba timu kupata ushindi ugenini ilikuwa ni jambo gumu. Wengi waliamini timu hupata ushindi nyumbani na kufungwa ugenini. Hii ni nadharia iliyofanya kazi miaka ya nyuma na hata sasa baadhi ya wadau wa soka wanaiamini, lakini kwa soka la kisasa linalochezwa sidhani kama bado kuna ukweli huo.
Hata kiakili wachezaji walikuwa wakitulia na kucheza kwa ari kubwa na kujiamini, ndio maana walikuwa wakipata matokeo mazuri nyumbani kwa asilimia kubwa. Ni sawa na ule msemo wa mbwa hubwekea kwao. Hali hiyo na imani hizo za kujiamini zikiwa nyumbani ziliziathiri pale zilipokuwa zinatoka nje ya maeneo yao ya kujidai. Wachezaji walikuwa wakiathirika kisaikolojia na kupoteza mchezo.
Wala usibishe kuwa nadharia hiyo imekuwa ikiwaharibu kisaikolojia wachezaji na makocha ambao kwenye akili zao wamekuwa wakiamini hilo.
Hata klabu kubwa duniani zilikuwa zikiamini hivyo na baadhi zinaendelea kuamini mpaka leo, kama ambavyo baadhi ya makocha wakubwa walikuwa wakiamini. Kuna baadhi ya timu kama Manchester United ilipokuwa chini ya Sir Alex Ferguson waliamini ni ngumu kufungika nyumbani.
Wachezaji wake waliamini hivyo na matokeo uwanjani yakawa hivyo. Mashabiki wa klabu hiyo nao wakaamini hivyo, ndio maana baada ya kocha huyo kustaafu na kina David Moyes, Louis Van Gaal na hata Jose Mourinho kama sio Ole Gunnar Solskjaer kila wanapopoteza Old Trafford, hawakuamini na waliwaona wanakiuka misingi ya Mashetani Wekundu. Kumbe ni yale mazoea tu!
Yapo mambo mengi yanayochangia timu kupoteza ugenini ikiwamo hali ya hewa, uwanja, mashabiki na hata uchovu wa safari kwa wachezaji, lakini bado kwa soka la kisasa linaloamuliwa penalti na kukubali ama kulikataa bao kwa kutumia teknolojia lolote linatokea.
Hata Yanga inaweza kufanya maajabu ugenini, lakini kwa kuangalia rekodi zake kwenye michezo yao nchini Misri na hata nchi nyingine za Ukanda wa Afrika Kaskazini, zinaigomea mapema Cairo.
Kipigo cha mabao 2-1 nyumbani wala sio ishu sana, kwani kwa wanaokumbuka Simba mwaka 1979 ilifungwa nyumbani mabao 4-0 na Mufulira Wanderers ya Zambia, kila mtu aliamini ilishatolewa kwenye Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa), lakini si mnajua kilichotokea.
Simba ilikwenda kule na kushinda mabao 5-0 na kuvuka ikiwaacha wenyeji mbele ya Rais wao enzi hizo, Kenneth Kaunda wakipigwa na butwaa bila kuamini kilichowakuta. Hata hivyo, hiyo ni Simba. Simba yenye rekodi zake kwenye mechi za kimataifa ikitofautisha na watani wao, Yanga.
Mashabiki wa Yanga kwa sasa wanaamini timu yao itashinda ugenini kwa kurejea ilichokifanya mjini Gaborone, Botswana walipoing’oa Township Rollers kwa kuifunga 1-0 baada ya sare ya 1-1 jijini Dar es Salaam, sio mbaya. Hata mimi naamini Yanga inaweza kupindua meza ugenini kama itajipanga vyema, kwa vile Pyramids haitishi sana miongoni mwa timu za Misri.
Lakini mashabiki hao wa Yanga ni kama wamesahau kuwa timu yao imetoka kulala 2-1 mjini Ndola, Zambia mbele ya Zesco United hivi karibuni baada ya sare ya 1-1 nyumbani?
Ieleweke kama mdau wa soka napenda sana Yanga isonge mbele, lakini sioni cha kuivusha hasa kama itawakabili Pyramids kwa aina ya soka walilochezwa CCM Kirumba wiki iliyopita. Sioni Yanga ikivuka mbele ya Wamisri kama Kocha Mwinyi Zahera hatafanya mabadiliko hasa kwenye eneo la mbele ambalo amekuwa akishindwa kumchezesha Juma Balinya kama straika. Kama Balinya atachezeshwa pembeni ama kuanzia benchi sambamba na Patrick Sibomana kama ilivyokuwa Kirumba, basi Zahera ajiandae tu kubeba mzigo wa lawama.
Pia, akumbuke kuwa Kelvin Yondani hatakuwepo uwanjani kuwakumbusha wenzake majukumu ya kukaba nafasi. Hakuna anayebisha mechi iliyopita, Yondani aliyeibeba Yanga isibebeshwe kapu la mabao, licha ya kipa Farouk Shikhalo kufanya kazi yake kwa ufanisi.
Najua kuna watu watachukia kwa kulisema hili, lakini ukweli ndivyo ulivyo. Yanga ina mlima mrefu wa kuupanda Cairo. Kama nilivyoeleza wiki iliyopita kwamba umakini na nidhamu ndivyo vinavyoweza kuivusha Yanga, bado wakomalie hilo. Umakini mdogo wa mabeki wa Yanga pale Kirumba na uzembe uliofanywa na Mrisho Ngassa ndivyo vilivyoigharimu timu.
Kama Ngassa asingeupuuza mpira ulioonekana kama unatoka nje Mohammed Farouk asingeupata na kupiga krosi iliyomalizwa kimiani kwa kichwa na nahodha, Abdalla El Said.
Hata hivyo, ukiacha mipango ya Zahera na kukosekana kwa muunganiko wa timu, lakini rekodi zinaiangusha Cairo, kwani tangu mwaka 1982 walipoanza kucheza na timu za Misri, Yanga haijawahi kushinda zaidi ya kuambulia sare ya 1-1 mwaka 1992 dhidi ya Ismaily.
Rekodi zinaonyesha hii ni mara ya tisa kwa Yanga kuvaana na timu za Misri na katika mechi nane za awali zikiwamo saba za Ligi ya Mabingwa ilizopoteza mara sita na kupata sare moja, huku ikilala pia kwenye Kombe la washindi mwaka 2000 kwa kuchakazwa 4-0 na Zamalek. Mwaka 1982 ilichakwaza 5-0 mjini Cairo na Al Ahly ambao pia waliwatungua 1988 (4-0), 2009 (3-0), 2014 (1-0) na 2016 (2-1), huku pia ikilala 1-0 kwa Zamalek na sare ya 1-1 dhidi ya Ismaily 1992, pia wakiwa hana rekodi ya ushindi kwenye nchi nyingine za Afrika Kaskazini kuanzia Sudan, Libya, Algeria mpaka Morocco.
Ni dhahiri Yanga leo inahitajika maajabu kusonga mbele, lakini kama wataamua kuwavaa wenyeji wao wa mipango tofauti na ile ya CCM Kirumba.
Kwa namna Pyramids inavyocheza ni wazi Yanga inahitaji kujituma zaidi ili isonge mbele na mbaya ni kwamba, rekodi zinaonyesha Pyramids haijapoteza nyumbani katika michuano ya CAF kwani, iliifunga Etoile du Congo ya Congo Brazzaville kwa mabao 4-1 na kutoka sare ya 11 na CR Belouizdad ya Algeria.
Muhimu kwa sasa ni kuiombea Yanga ili igeuze jiwe kuwa mkate, lakini mwishowe ni kumuachia Mungu tu afanye miujiza yake. Tofauti na hivyo ni kuanza kujipanga mapema kwa msimu ujao kama itapata nafasi ya kufuzu.