Mjue hata Wolper anawashangaa hivyo

Muktasari:

Hivi karibuni katika mitandao ya kijamii kumekuwa na video za ngono za watu maarufu zikisambaa na wahusika kuitwa sehemu za sheria na kuhojiwa, huku wengine wakiomba radhi na utetezi mwingi kuwa simu ilipotea au walirekodiwa bila kujijua.

WAKATI wapenzi wa burudani wakiendelea kujiuliza kitu gani kimewakumba baadhi ya wasanii wa kike kiasi cha kukubali kujidhalilisha kwa kupigwa picha na hata kurekodiwa video za utupu, kisha kuziachia mtandaoni, kumbe hata mrembo wa tasnia ya filamu, Jackline Wolper naye anashangaa.
Wolper ambaye anajishughulisha pia na ujasiriamali amesema anakerwa mno na kitendo cha baadhi ya wanawake kupenda kukubali kupigwa picha za utupu au video pindi wanapokuwa kwenye mahusiano.
Kauli ya mwigizaji huyo nyota imekuja wakati wimbi la mastaa kuhusishwa na kuvuja kwa video na picha zao za utupu likiendelea kuwa gumzo mitandaoni, huku baadhi yao wakikumbana na adhabu kali kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (Basata).
Akizungumza na Weekend Vibe, Wolper alisema mara chache sana kutokea wanawake kurekodiwa bila kujijua ila asilimia kubwa huwa wanakubali na hii ndio inawadhalilisha baada ya mahusiano kumalizika.
Wolper alisema ifike wakati wanawake wajisikie aibu na kujithamini utu na heshima yao kwa kuepuka mambo hayo yanayodhalilisha hadi familia zao na kuwaachia doa baya mbele ya jamii.
Hivi karibuni katika mitandao ya kijamii kumekuwa na video za ngono za watu maarufu zikisambaa na wahusika kuitwa sehemu za sheria na kuhojiwa, huku wengine wakiomba radhi na utetezi mwingi kuwa simu ilipotea au walirekodiwa bila kujijua. Jambo hilo na utetezi huo ndio uliomfanya Wolper kueleza hisia zake akidai anakerwa na hiyo tabia na kuwataka wanawake wenzake kuepuka michongo hiyo ya kurekodiwa ama kupigwa picha za utupu kwani inawaaibisha wao na jamii nzima ya Kitanzania.
“Unajua mtu ukiwa kwenye mahusiano chumbani unakuwa sio wewe, hivyo utakuta mtu unayemwamini akikwambia ufanye kitu huwezi kumkatalia na ukiangalia unampenda, ukishajirekodi ndio yanakuja majuto baadaye mkigombana mambo yanaachiwa hadharani,” alisema Wolper.
Aidha kisura huyo aliwageukia wanaume wanaofanya hivyo waache na kuwataka waonyeshe ukomavu wa akili na utu huku akisisitiza kuwa mwanaume yeyote atakayekuwa naye kwenye mahusiano asithubutu kumwambia suala la kujirekodi video za aina hiyo, kwani anaweza kumfanyia kitu kibaya.
“Natahadharisha mapema, akitokea mwanaume niko naye kwenye mahusiano halafu ananiambia habari za kujirekodi ukweli nitamfanyia kitu kibaya sana, maana upuuzi sitaki kuusikia kabisa na kama hakutakuwa na ulinzi au jamaa hana silaha, aisee patachimbika. Mwanamke ni kujiheshimu na sio chombo cha kudhalilishwa au kujidhalilisha kwa sababu ya mahusiano,” alisema.
Hata hivyo, Wolper anakiri kuwa miaka minne iliyopita aliwahi kukumbana na kisanga kama hicho cha kupigwa picha na mwanamme aliyekuwa naye kutoka Kongo, lakini aliwahi kuzifuta kwenye simu iliyotumika kwa kuhofia kuja kudhalilika.
‘’Ila haya mambo wewe yaache tu na uyasikie kwa mtu, kama usipokuwa makini unaweza kujuta sana, mimi yananikumbusha kuna kipindi nilikuwa nalewa sana kutokana na ‘stresi’ za maisha, kuna siku nilikuwa ‘location’ nilikuwa nimelewa hadi nikazima, akapigiwa simu mpenzi wangu,” alisema na kuongeza:
“Mpenzi wangu huyo alinifuata na kunipeleka nyumbani, kisha akanivua nguo zote akaanza kunirekodi na kunipiga picha, lakini nashukuru nilipozinduka na wakati nachezea simu yake nilizibaini na kufanikiwa kuzifuta bila mwenyewe kujua, kama utani baada ya wiki mbili alinitumia meseji akinitishia kitu atakachonifanya Watanzania watafunga macho na sintoamini.”
Wolper alisema kitu kinachomtia simanzi mpaka leo ni kwamba mwanaume huyo aliyetaka kumdhalilisha alikuwa ameshamvisha pete ya uchumba na kwenda kumtambulisha nyumbani kwa wazazi wake kwa ajili ya kumuoa.
“Kitu ambacho nawataka wanawake wenzake hasa wenye majina yao, wawe makini. Hata wanapokuwa kwenye mahusiano waepuke mambo haya na hasa kuwa makini kama wanatumia pombe, wanatakiwa kujichunga kwa sababu wanaweza kufanyiwa lolote na kuumbuka.”
Wolper alisema anajua wale waliofanyiwa kwa bahati mbaya wanajisikiaje, lakini asilimia kubwa kuna wanaokubali kwa sababu ya kutaka kulinda penzi na hata kujiwekea kumbukumbu, lakini simu ni kitu kinachoweza kumtoka mtu ghafla na kufika katika mikono isiyo salama na kuwaumiza.
Hivi karibuni wasanii kadhaa wa filamu na muziki wa kizazi kipya nchini wamejikuta matatani kwa sababu ya picha na video zisizo za maadili ambazo zimekuwa zikisambazwa mitandaoni na kuibua hisia mbaya, kwamba huenda wanafanya hivyo kwa makusudi kwa nia ya kutafuta kiki au kujiuza.