Usajili gani kufunika wa Niyonzima Yanga, Luis Simba leo

Muktasari:

Timu nyingi zimefanya marekebisho katika maeneo machache kulingana na mahitaji husika kwani dirisha hili.

Dar es Salaam. Wakati dirisha la usajili kwa klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara linafungwa leo saa sita usiku wadau wanasubiri kuona usajili utakaofunika ule wa Haruna Niyonzima kwenda Yanga na Luis Misquissone kwenda Simba.

Hadi mchana huu Yanga imesajili wachezaji watano wapya wakati watani zao Simba wakiwa wamesajili mchezaji mmoja wanaonekana kutokuwa bize na kusajili kwa sasa.

Mbali ya Niyonzima na Luis waliosajiliwa kwa kishindo na miamba hiyo ya Tanzania pia timu nyingi zimefanya usajili katika dirisha hili wakiwemo Singida United na Azam pamoja na Polisi Tanzania wamekuwa bize katika dirisha hili.

Hivi ndivyo ambavyo usajili ulivyofanywa kupitia dirisha hili dogo katika klabu mbalimbali.

SIMBA

Katika kikosi cha Simba katika dirisha dogo wameachana na mshambuliaji wao Wilker Da Silva huku wakiingiza Luis Misquissone akitokea UD Songo.

YANGA

Walianza ligi kwa kusuasua kutokana na kutokuwa na pesa, lakini baada ya dirisha dogo mdhamini wao GSM kuamua kuwekeza nguvu zaidi wameanza kukisuka kikosi chao.

Yanga katika dirisha hili wamewasajili Ditram Nchimbi, Yikpe Gnamien, Adeyum Saleh, Haruna Niyonzima na Tariq Seif, huku wanaotarajia kutolewa kwa mkopo nyota wake Ally Ally, Said Makapu na Rafael Daud.

AZAM

Klabu hii imemtoa kwa mkopo mshambuliaji Paul Peter kwenda Prisons lakini katika upande wa uimalishaji kikosi chao wameangalia katika upande wa ushambuliaji tu.

Azam wamesajili Never Tigere kutoka FC Platinumz ya nchini Zimbabwe pamoja na Khleffin Hamdoun kutoka Mlandege Zanzibar hawa wote wakicheza nafasi ya kiungo.

SINGIDA UNITED

Timu hii ilianza Ligi kwa kusuasua huku wakiwan hawana nyota yoyote mwenye jina katika klabu yao. Uongozi ulikaa na baadaye walimchukua kocha mwenye uzoefu Ramadhan Nswazurwimo kwaajili ya kukisaidia kikosi hiko kiweze kubaki Ligi Kuu.

Katika dirisha hili wamewasajili Athuman Idd ‘Chuji’, Haruna Moshi ‘Boban’, Ame Ali, Muharami Issa ‘Mkopo’, Haji Mwinyi, Tumba Lui na Six Mwakasega.

KAGERA SUGAR

Kikosi cha Meck Maxime hakina mbwembwe kwani licha ya kuwa na mshambuliaji Yusuph Mhilu mwenye magoli sita waliamua kumuongeza Kelvin Sabato katika nafasi hiyo akitokea Gwambina inayoshiriki Ligi Daraja la kwanza huku wakiwa hawajaachana na yoyote.

POLISI TANZANIA

Kuondoka kwa kocha wao msaidizi Seleman Matola na mshambuliaji wao Ditram Nchimbi ni kama imewavuruga kwani wamefanya usajili mfululizo katika dirisha dogo huku mwanzo kulikuwa hakuonekani kama wana mahitaji makubwa.

Timu hii katika dirisha hili wameanza kufanya usajili kuanzia golini baada ya kumsajili Peter Manyika huku maeneo mengine wakiwasajili Athanas Mdamu, Pius Buswita, Matheo Anthony na Jimmy Shoji.